Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon Toufiq Salim Turky

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpendae

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala kwa kunijalia kufika hapa, lakini pia kumtakia Rehema mzee wangu aliyekwishakutangulia mbele ya haki Mheshimiwa Salim Turky, Mr. White. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue fursa hii nikishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi kwa kuona ninafaa na kuweza kuwakilisha wananchi wetu wa Jimbo la Mpendae. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze na kuunga mkono hoja, kwa kweli Mpango huu ni mpango kazi. Kusema kweli nchi yetu inavyoelekea imetuletea hamasa kubwa mno ndani ya miaka mitano hii. Mheshimiwa Rais wetu kafanya makubwa sana, ile hamasa imekuja mpaka Visiwani. Kwa mara ya kwanza katika historia CCM kushinda kwa asilimia 74 Zanzibar, imeonesha kwa namna gani Awamu ya Tano ilivyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la uchumi, nataka kuongelea masuala mawili tu, hatuwezi kuongelea uchumi kama hatuongelei mtaji. Mtaji tukisema inaingia katika masuala ya ajira, lakini muhimu sana namna gani unaweza kuipata ile capital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la ajira tunatafuta ajira milioni 8, namna gani tutazipata hizi ajira? Ni kwa kupitia private sector lakini pia watu kuweza kujiajiri wenyewe. Tukitizama mabenki yetu wanawapatia mtaji matajiri zaidi kuliko wanyonge, sasa namna gani wale wanyonge wanaweza kupata mtaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuitazame katika taswira mbili; uchumi wa pande hizi mbili uko tofauti, tukifuata uchumi wa Bara uko tofauti na wa Zanzibar. Zanzibar kitu gani tunaweza tukafanya ambacho kinaweza kusaidia kwa pande zote mbili, kupitia Benki Kuu (Bank of Tanzania), tunaweza tukaongeza wigo wa kuanzisha offshore banking. Hii off shore banking itasaidia vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia visiwa vyote vilivyoendelea duniani, mfano Singapore, Dubai, Hongkong, Mauritius, Panama masuala yote wanayofanya ni offshore banking, wanahakikisha watu wanaleta fedha ndani ya nchi zao. Sasa zikipatikana zile hela ndipo yale mabenki wanakuwa na excess funds za kuweza kuwapatia wajasiriamali wadogowadogo watakuwa na appetite. Sasa kwa kwa nini tusianzishe offshore banking katika kusaidia uchumi wa Zanzibar lakini BoT ikawa ni msimamizi mkuu kupitia Bank of Tanzania branch ya Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kuhusu Zanzibar kuendelea katika real estate. Uchumi wa visiwa ni fedha na real estate, hiyo ndiyo ukitizama karibu visiwa vyote vilivyoendelea. Sasa tukitizama katika suala la real estate kuna changamoto moja kubwa nayo ni suala la immigration. Dubai leo ukitaka kununua nyumba zaidi ya milioni 1 Dirham, sawasawa na Dola 270,000 unapatiwa resident permit ya miaka mitatu. Leo kuna nyumba ya Dola 600,000 imejengwa pale na Mzee Bahresa, wako wengine wamejenga hata resident permit ya mwaka mmoja hupati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukitizama ule mradi wametumia tayari almost 150 million dollars, lakini hauwezi ku-take off. Miradi ya namna ile iko mingi sana Zanzibar. Zanzibar kuendelea ni suala zima la tourism na real estate, sasa ni namna gani tunaweza kusaidia? Tunaweza kutizama katika wigo huo, namna gani immigration kupitia Zanzibar ikawa na wigo fulani sasa wa kuwawezesha Wazanzibar kule katika uwekezaji wao. Tutaweka cealing, mtu aki-invest dola laki tatu anaweza kupata resident permit, pengine inamruhusu kubakia Zanzibar au akitaka kuja mpaka Bara kuwe na namna fulani ya kuweza kuwekeza watu wasiweze kutumia vibaya ile mianya ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana tufanye hivyo kama kweli tunataka maendeleo yafanyike, hususan kwa uchumi wa Zanzibar. Tukitizama rasilimali zetu sisi zaidi ya uchumi wa blue ambapo tunaongelea bahari ni mdogo mno tofauti na Bara; kuna rasilimali watu, rasilimali nguvu na minerals. Kwa hivyo, naombeni sana tulitizame suala hili na muhimu suala la BoT kwenda offshore na immigration hususan katika masuala ya resident permit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja. Ahsanteni sana. (Makofi)