Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Utukufu aliyeniwezesha kusimama hapa leo. Jambo la pili niwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Ruvuma ambao walinipa kura nyingi sana za kishindo zilizonisababisha mimi kuingia ndani ya Bunge na kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikishukuru chama changu cha Mapinduzi, lakini pia niishukuru familia yangu. Nasema ahsante sana wote walioshiriki kuniwezesha, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, lakini pia Mpango wa Maendeleo wa Mwaka Mmoja. Ili tuweze kujenga uchumi ni lazima tushirikishe uchumi wa viwanda pamoja na masuala mazima ya kilimo, bila kuhusianisha hivi vitu hatuwezi kufika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa viwanda unategemea sana sekta ya kilimo kwa asilimia 80. Kwa hiyo, vyovyote vile iwavyo lazima tuweke mkakati wa makusudi kuhakikisha kwamba kwenye eneo la kilimo tunakaa sawasawa. Ni lazima tuhakikishe kwamba pembejeo na zana za kilimo zinapatikana kwa urahisi ili kuweza kufanya mageuzi makubwa sana katika sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani nao pia kuanzia vitongoji, vijiji, kata, wilaya kwenda mpaka mkoa ni lazima kuhakikisha kwamba wanakuwa ni wale ambao wanaweza kwenda mpaka chini na kutoa mafunzo mazuri kuhusiana na masuala ya kilimo ili wananchi wetu waweze kufanya uwekezaji wa kilimo wenye tija. Badala ya hivi ilivyo sasa wananchi wanalima kiholela na wala udongo haupimwi kwamba kwa udongo huu sasa mnaweza kulima migomba au pamba, wanalima tu kwa kubahatisha. Kwa hiyo, wataalam wakisimama makini kabisa na wakaweza kupima udongo ni imani yangu kwamba tutatoka hapa tulipo na tutasonga mbele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo na umwagiliaji. Nilidhani pia kwenye eneo hili tuhakikishe kwamba Serikali inaweka fedha nyingi katika kuandaa miundombinu ambayo itawezesha suala la ulimaji wa umwagiliaji ili wananchi au Tanzania yetu tuweze kuwekeza kwenye kilimo na tuweze kuvuna mara mbili kwa mwaka au zaidi. Hapo ndipo tutakapoweza kuviwezesha viwanda vyetu viweze kufanya kazi na viweze kuzalisha na hatimaye kuleta ajira nyingi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia suala la mbegu lizingatiwe. Nashauri Serikali ione namna gani itaweza kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumzie suala la masoko. Hivi sasa tunazungumza masuala ya kilimo lakini wananchi wanapokuwa wamevuna mazao yao masuala ya masoko ni kubahatisha, hawana masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti,nikizungumza hapa wale ambao wanazalisha mazao ya nafaka katika Nyanda za Juu Kusini ukiangalia zao la mahindi wananchi bado wana mahindi ya mwaka jana na yakakutana na mwaka huu. Kwa hiyo, ni wazi kwamba, mwananchi hapo hawezi kufanya uwekezaji wenye tija na wala hatuwezi kufikia malengo tunayoyatarajia. Kwa hiyo, nilidhani kwenye eneo hilo basi, liwekewe mkakati wa makusudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Benki ya Kilimo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imegonga Mheshimiwa, ahsante.

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenikatili. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)