Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie Mpango huu wa bajeti wa miaka mitano 2021/2022 mpaka 2025/2026 pamoja na mwaka mmoja wa 2021/2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vipaumbele vyote ambavyo vimeainishwa, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na wataalamu wake kwa ujumla kwa maana nimeshiriki katika kuuona Mpango ulivyowasilishwa kwenye Kamati, kama Mjumbe wa Kamati na nimechangia kwa kina. Kwa sasa nijielekeze katika maeneo mawili tu. Eneo la kwanza ni master plan ya Dar es Salaam kwa ujumla, lakini la pili, jinsi gani tutatumia usimamizi na ufuatiliaji katika miradi, hasa ya kimkakati na mingine kwa maana ya monitoring and evaluation katika miradi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wachache wa Dar es Salaam wamezungumza kwa ujumla juu ya master plan ya Dar es Salaam na hasa katika maeneo ya miundombinu kama mafuriko na upimaji wa ardhi. Nipongeze sana huu mpango wenyewe, katika page ya 97 wameeleza juu ya mkakati wa kuboresha maeneo hayo ya mabonde, lakini kuboresha pia maeneo ya miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwa Dar es Salaam ambayo tuna population yenye makadirio takribani milioni sita kwa kufikia mwaka 2020, lakini tukiwa tunajua hata tax collection haipungui asilimia 80 na hata mchango katika GDP Dar es Salaam inachangia zaidi ya asilimia 75. Kwa msingi huo, tunataka kuona Dar es Salaam inakuwa kama sehemu ya kimkakati sana katika kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko hapa kutafuta fedha siyo kuangalia fedha zinakwenda wapi, tutakuja kwenye bajeti. Hapa mimi naona kama mkakati ukiwekwa vizuri Dar es Salaam inafaa sana kwenda kwenye housing building strategy. Wakati niko Diwani Manispaa ya Kinondoni tulikuwa tuna mpango wa kuondoa nyumba kongwe za Magomeni, takribani nyumba 605, ni mpango wa zaidi ya miaka 8 kuanzia 2012, leo nyumba zimejengwa. Naona mpango huo ungeendelea Dar es Salaam; tuna maeneo kama Tandale, Magomeni, Manzese, tukafanye mipango ya kujenga nyumba ambazo zitatusaidia kuinua uchumi wa watu, lakini tutaweza kuwa ni sehemu ya mapato sasa kwa jinsi ambavyo tutaingia makubaliano na wale wakazi ambao wana ardhi za msingi au ardhi zile ambazo ni za kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili kwa haraka ni upimaji wa ardhi. Mpango umesema vizuri una nia ya kupima ardhi nchi nzima, sasa waende kweli kimkakati wapime ardhi. Waipime ardhi ya Dar es Salaam kutokana na population niliyosema, makadirio ni watu milioni sita, tukipima ardhi kwa watu wote hawa, kama Mheshimiwa Waziri alivyosema nia yake ni nzuri kwenye hili, basi tutaweza kuona jinsi gani mapato tunayapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko eneo hili la usimamizi na ufuatiliaji. Tutakubaliana hapa miradi mingi hata hii ya kimkakati bado item au component ya ufuatiliaji haipo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nivumilie dakika moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti …

MWENYEKITI: Nina orodha ndefu Mheshimiwa. Uniwie radhi, ahsante sana.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)