Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo awamu ya tatu na Mpango wa Mwaka mmoja. Nitaanza kwa kuchangia kuhusu kukuza uchumi wa nchi pamoja na pato la nchi na hasa kukuza uchumi wa viwanda. Nikianza kuchangia kwenye uchumi wa viwanda siwezi nikasema viwanda vitakua bila ya kilimo, uvuvi, ufugaji, maji pamoja na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia zaidi ya 66 ya wananchi wamejikita kwenye kilimo. Kwa hiyo, lazima tuangalie kwa undani kuhusu kilimo ndiyo tutaweza kukuza pato la Taifa na pato la mwananchi yeye mwenyewe mfukoni mwake. Kwa hiyo jambo la muhimu sana hapa la kuangalia ni kuhusu kilimo kiwe rafiki, kiwe cha kisasa, kilimo kiweze kuvutia kwa wananchi na hasa kwa vijana na kiwe kilimo cha maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubali kuwa Mawaziri wa Kilimo, Uvuvi pamoja na Mifugo, wanafanya vizuri sana. Pamoja na mikakati iliyowekwa, inabidi tuweze kutimilika vizuri sana. Kwa upande wa vijana wanapata shida, lazima tuone jinsi ya kuwavutia vijana na watu wazima, wote waone kuwa kilimo ni rafiki ili kila mmoja avutiwe kuingia kwenye kilimo. Tufanyaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza tuangalie zana za kilimo. Nakumbuka zamani yalikuwepo matrekta ya vijiji ambayo yalikuwa yanasaidia wananchi kulima kwenye mashamba yao. Kwa hiyo, kama hiyo inawezekana naamini hata vijana wanaotoka vyuo vikuu wanaweza wakaingia kwenye kilimo, hata vijana wanaomaliza VETA, hata vijana ambao hawajasoma, wote wanaweza kuingia kwenye kilimo kwa sababu hawatatumia nguvu, watatumia zana za kilimo ambazo zinapendekezwa kama matrekta na kadhalika ili kusudi tuepukane na jembe la mkono ambalo linatoa jasho kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linavutia kwa vijana hasa kuwekeza kwenye kilimo waweze kukopesheka na watakopeshekaje? Tuweze kupata wawekezaji binafsi na hasa kilimo cha mkataba. Kilimo cha mkataba ni kizuri sana kwa sababu hicho kilimo wataweza kulima na baada ya kuvuna na kuuza wataweza kukata zile hela ambazo watakuwa wameingia pamoja na mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la muhimu sana kwa hawa vijana pamoja na kilimo kuwa rafiki na kukibadilisha kilimo lazima tuwe na mbegu bora. Tuwe na mbegu za mafuta, ni kweli kila mmoja sasa hivi anasema bei ya mafuta ni ghali. Unajiuliza kwa nini, Tanzania tuna ardhi nzuri, tuna wasomi wazuri, tuna kila kitu kwa nini iwe hivyo? Kwa hiyo tuangalie hata michikichi hiyo sio lazima izalishwe Kigoma peke yake, hata Morogoro tunazalisha mchikichi, hata Kagera wanaweza wakalima mchikichi, hata Mbeya hata Kilimanjaro. Kwa hiyo ni kiasi cha kuweka uzito kuona tutafanyaje tuweze kuondokana na umaskini kwa kupitia kilimo hasa kwa kuangalia pamoja na masoko. Kabla hujaanza zao uweze ku-focus kwenye soko, ukiwa na soko bila shaka utaweza kuzalisha kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la viwanda, lazima tuweze kuwa na ufugaji. Kwenye ufugaji tufuge mifugo ambayo ni ya kisasa, sio bora kufuga. Ni kufuga kwa kisasa na kuzalisha kwa kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye uvuvi, tuwe na blue economy, tuone kuwa tunafanyaje kwenye uvuvi kusudi tuweze kuwa na viwanda ili wananchi wote waweze na wenyewe kunufaika kwenye mambo ya kilimo, uvuvi, mifugo na kwenye ufugaji wa nyuki pia, asali ipo lakini hatuna soko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi, lakini naamini imeeleweka. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)