Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu anavyoendelea kutulinda na kutubariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Kagera walionichagua kwa kura nyingi. Nakishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua na leo hii ni Mbunge katika Bunge la Kumi na Mbili. Ahadi yangu kwao ni kwamba nitaendelea kuwatumikia wananchi wote kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ulioletwa ni mzuri, tunachangia ili tuboreshe; na kwa sababu ya muda nitajikita kwenye eneo moja la kilimo. Lengo moja la Mpango huu ni kuchochea maendeleo ya watu. Kama tunataka kuchochea maendeleo ya watu, basi inabidi tuwekeze nguvu nyingi katika maeneo ambayo yana watu wengi na katika Tanzania tuna maana ya kilimo, uvuvi na ufugaji. Hatuwezi kupata maendeleo yanayotarajiwa kama tutaendelea kulima kwa jembe la mkono na kwa kutegemea mvua, ambacho ni kilimo cha kujikimu inabidi sasa twende kwenye kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza, ili tuweze kunufaika na Mpango huu, kwanza, kila mkoa uhakikishe kwamba unatenga maeneo makubwa kwa ajili ya kilimo, watafutwe wawekezaji wa nje na ndani waweze kuwekeza kwenye mashamba makubwa ya kilimo. Vilevile wananchi wawezeshwe kupata mitaji kwa bei nafuu. Kwa maana kama wanapata mikopo kutoka benki, basi riba isizidi asilimia 10, iwe chini ya asilimia 10 kusudi waweze kuzitumia hizo hela kutafuta zana za kilimo bora na waweze kulima kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta zana nyingine ni ghali sana, kwa mfano, matrekta makubwa, excavators, vesta, weeder na vitu kama hivyo. Ingekuwa ni vizuri kila Halmashauri ikawa na mfuko wakanunua vifaa hivyo; vikundi vidogo vidogo na watu binafsi wakawa wanakodishwa kutoka kwenye Halmashauri, nao wakaweza kulima kilimo kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanya kilimo kikubwa inabidi vilevile tuwe na kilimo cha umwagiliaji. Kuna schemes mbalimbali humu katika Tanzania ambazo nyingine zilishakufa, tuzifufue lakini vilevile tunaweza kuanzisha nyingine mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Vituo vya Utafiti kama TARI, TACRI na vile vya usambazaji mbolea, lazima watusaidie kuhakikisha kwamba tunakuwa na mbegu bora. Kwa sababu hata ukilima shamba kubwa namna gani, kama mbegu uliyokuwanayo siyo bora, huwezi kupata tija yoyote. Kwa hiyo, tunaomba wapewe bajeti ya kutosha kusudi waweze kuzalisha mbegu zilizo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafute wawekezaji, tuwashawishi, tuwatengenezee mazingira mazuri waweze kuwekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani ili kusudi yule mkulima wa Kahawa kutoka Mkoa wa Kagera asiuze kahawa ghafi; akaange, apaki, auze au asage auze; mkulima wa pamba atengeneze nyuzi auze, au atengeneze nguo ndiyo ziuzwe. Kwa namna hiyo, tutaweza kumfaidisha mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna tatizo kubwa la soko la mazao yetu. Naomba idara za Serikali ambazo zinahusika katika kutafuta masoko, waende nchi za nje, waingie mikataba, watu walime wakijua kwamba soko liko wapi. Natoa mfano wa Botswana. Wao wamefaidika sana na mifugo yao kwa sababu hata kabla hujaanza kufuga nchi inaaenda kuingia mikataba na nchi nyingine, unajua kwamba unafuga kwa standards zipi, ukisha-produce yale mazao inakuwa ni rahisi kuuza kwa sababu unajua unalenga soko gani. Isije ikawa kama ile story ya mbaazi ambapo watu walilima lakini wakakosa masoko.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Serikali kwa ajili ya…

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Ooh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)