Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa namna ya pekee kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo. Nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai kurudi hapa tena leo kwenye Bunge la Kumi na Mbili. Nikishukuru chama changu cha Mapinduzi, Chama ninachokitumikia sasa hivi ambacho ndicho chenye Ilani na walinikabidhi Ilani wakati wa uchaguzi mkuu na nilishinda kwa kishindo Jimbo la Ndanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana pia ushirikiano ninaoupata kutoka kwa Wabunge wenzangu wa Chama cha Mapinduzi. Nimesimama hapa nikiwa na furaha kwa sababu kati ya mambo ambayo nilikuwa nayatamani siku zote ni kusimama na kuitetea Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mipango mizuri ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri sana ndugu zangu wa upande wa pili, Waheshimiwa Mawaziri pia ikiwezekana tuwagawie wale ndugu zetu Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuna mambo mengine wanayabishia kwa sababu hawajayaona, hawajasoma na hawayafahamu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ya msingi ambayo napenda kuyachangia leo kwenye Mpango huu. Suala la kwanza kabisa ni kuhusu reli ya Kusini. Tunataka hapa Waziri wetu aje kutueleza nini mpango madhubuti wa Serikali kuhusu reli ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumesikia wengi wanaongea, suala la Liganga na Mchuchuma, kama ambavyo nimesema toka mwanzo kwamba liko hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Tunaomba sasa likafanyiwe kazi na litekelezwe kwa ajili ya kuongeza uchumi wa watu wa Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna suala la barabara. Barabara ya Mtwara – Newala – Masasi – Nachingwea – Liwale na kipande cha barabara ambacho huwa hakitajwi kinaenda kuunganisha Malinyi ili kuwafanya watu wa Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara, Lindi na Ruvuma kufika kirahisi Makao Makuu ya nchi badala ya kupita njia ndefu ya Dar es Salaam. Kuna barabara pia ya Nanganga - Nachingwea – Ruwangwa mpaka Liwale pia na yenyewe tunaomba ifanyiwe kazi na tupate hapa majibu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la wastaafu, limeongelewa hapa ndani na Wabunge wengi sana, wa ngazi mbalimbali wakiwemo wanajeshi, walimu kuhusu stahiki zao na haki zao za msingi na kumekuwa na ucheleweshwaji mkubwa sana wa malipo yao wakati huu. Kwa hiyo, tunaomba Serikali kwa kina kabisa ije itueleze mikakati yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nataka nijikite hasa kwenye suala la kilimo. Sisi kule kwetu ni wakulima wa korosho na ni zao la kimkakati la Kitaifa katika yale mazao matano makubwa. Niombe sana Serikali izingatie sasa kuona tunawasaidia hao wakulima wa korosho ili waweze kusaidia kuongeza uchumi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo makubwa ambayo huwa yanajitokeza kila mara wakati wa kilimo. Msimu uliopita wa korosho tumeona wakulima wanahangaika sana kupata magunia. Katika karne ya leo kunakuwa na shida ya vifungashio vya korosho yetu tunayotaka kuiuza. Kwa hiyo, niombe sana Serikali iweke msisitizo na Waziri wa Kilimo aje kutueleza hapa mikakati yao ya kuhakikisha magunia na pembejeo kwa maana ya sulphur inapatikana kwa wakati kwa ajili ya wakulima hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka mwaka juzi katika mjadala hapa iliondolewa ile pesa kwa ajili ya tozo ambayo ilikuwa inakwenda kusaidia kufanya utafiti pamoja na kuongeza mambo mengine kwa wakulima. Tuiombe sasa Serikali kutafakari upya kama ambavyo imefanya kwenye kurejesha ile pesa ambayo ilikuwa inakusanywa na TRA kwa ajili ya mabango imekwenda tena kusaidia halmashauri. Kama inawezekana basi, waone namna ya kuwasaidia wakulima, hii pesa ingeweza kurudi kwenda kulipa yale madeni ya zamani ambayo wanadai watu wengi waliotoa huduma kwenye zao hili la korosho na sekta nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia hapa Mbunge mmoja anasema zao la korosho limeshuka kidogo uzalishaji wake, ni kwa sababu ya kukosa utafiti, kukosa dawa kwa wakati na uwezo mdogo wa wasimamiaji. Mazao haya ya kimkakati yanasimamiwa na vyama vya ushirika. Sisi kimsingi tulichoka, pamoja na nia njema ya Serikali kutaka kuboresha, lakini tuone sasa unapatikana mfumo thabiti kabisa utakaokwenda kupata viongozi bora, waadilifu na waaminifu kwenye vyama vyetu vya msingi na kwenye vyama vikuu ili kuweza kuwasaidia wakulima. Tumeona sasa hivi chaguzi mbalimbali zinafanyika ndani ya vyama hivi, lakini kimsingi watu wa COASCO hawajafanya kwa uhakika kabisa mahesabu kwa sababu, wanapobadilishana uongozi kwenye vyama hivi kumekuwa na utaratibu wa kurithishana madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madeni makubwa sana ya wakulima sisi tumeyakuta. Tumetoka kwenye Bunge lililopita tumeingia kwenye Bunge hili bado madeni hayo yapo. Kwa hiyo, niiombe Serikali au Waziri wa Kilimo awaagize watu wa COASCO kabla viongozi hawa hawajamaliza kukabidhiana madaraka yao pale, basi kimsingi wahakikishe kabisa wanafanya ukaguzi, ili kuweza kukabidhiana ripoti zilizo safi, lakini tufahamu watu wa kuweza kuwawajibisha pale panapotokea upungufu katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema kwamba, kwenye zao la korosho kuna mambo mengi sana, kwa hiyo, tunahitaji kabisa kimsingi, sisi kama wakulima tunaotokea eneo la wakulima wa korosho, tukutane na Mheshimiwa Waziri katika sekta hii ili tuweze kumshauri vizuri kwa sababu, mambo mengi tunayafahamu kule nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa mara ya kwanza toka niingie kwenye Bunge hili, kwa sababu huko nyuma nilikuwa siwezi kuunga mkono kwa sababu tulikuwa tuna ilani ambayo tunaitekeleza. Ahsante. (Makofi)