Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Nawashukuru wapiga kura wa Jimbo la Bunda kwa kunipa nafasi hii. Naishukuru Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kufanya kazi nzuri sana kwa Awamu hii ya Tano iliyopita na kusema kweli wamefanya vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa, lakini moyo wake wa kutufanya sisi tuwe humu ndani kwa kuwa na kauli moja tu ya kusema corona ipo na itaendelea kuwepo lakini sisi tutaendelea kufanya kazi. Kwa heshima yake na kwa Mwenyezi Mungu, tutafika huko tunakokwenda. Niwaambie, hili suala la corona halitaisha, litaendelea kuwepo, kwa hiyo, mkiendelea kuogopa, mtaogopa mpaka mnaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze habari ya viwanda. Nimesikia wenzangu wengi wanazungumza kuhusu viwanda. Katika karne hii ya viwanda na teknolojia kubwa hatutegemei huko tunakokwenda kuwa na viwanda ambavyo vitaajiri watu wengi. Kwa sababu duniani kote kuna aina mbili za viwanda ukiacha mambo ya cherehani na vitu vingine. Kuna capital intensive industry na kuna labour intensive industry. (Makofi)

Mhshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, viwanda hivyo viwili, capital intensive ni kiwanda chenye kutumia mitaji mikubwa, lakini wafanyakazi wachache; na labour intensive iliyokuwa inatumika kwenye karne ya 19 kurudi nyuma inatumia mtaji mdogo lakini wafanyakazi wengi. Huko tunakokwenda hatutakuwa na viwanda vya labour intensive, kwa sababu teknolojia yenyewe inakataza kuwa na viwanda vingi kwa eneo moja kwa maana ya climatic change. Greenhouse gases inakuwa kubwa na watu wanaleta matatizo mengine ya mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukubali huko tunakokwenda, kwenye nchi yetu tuwe na viwanda hata vya kanda tano vikubwa ambavyo vinaweza kufanya kazi nzuri. Mtu mmoja aliniambia ukileta kiwanda cha nyanya hapa ukawa unasaga tani 500 kwa siku, hakuna nyanya hapa Tanzania. Hakuna sehemu wanalima nyanya za kutosha kwa kiwanda hicho. Kwa hiyo, labour intensive ni kiwanda kikubwa kinachojengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna Kiwanda cha Ngozi cha Arusha, tunataka kiwe kikubwa, lakini stores zake zijengwe Mara, Shinyanga na Mwanza. Stores zile ziwe za kutunza ngozi na kusafirisha kupeleka kiwandani. Hivyo ndivyo viwanda tunavyovitaka sasa hivi. Viwanda ambavyo ajira yake ni Watanzania ambapo watoto wetu wanaotoka mashuleni wawe wanaajiriwa kufanya kazi ya kukusanya ngozi, kuwa agents wa ngozi na mazao. Kwa hiyo, hivyo ndiyo viwanda. Tunataka kuwa na kiwanda kikubwa cha capital intensive, tunaweza kukiweka hata Singida au Mwanza Kiwanda cha Alizeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna yale mambo ya kilimo tuliyazungumza sana, lakini nashangaa sijui kuna giza gani limetokea Tanzania. Tunazungumza mazao ya mafuta Tanzania, lakini alizeti inalimwa kila mahali. Yaani tumeshindwa kutamka tu kwamba tunataka tani ngapi za alizeti na soko liwepo tuweze kufanya kazi hiyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunasema viwanda vya sasa kusema kwamba vitaajiri watu wengi, itakuwa ndoto. Kwa hiyo, tutengeneze mazingira ya viwanda vinavyofanya kazi, lakini ajira yake iwe wajasiriamali, siyo kwenda maofisini kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze habari ya maji; na hili Waziri wa Maji anielewe na Waheshimiwa Wabunge wanielewe vizuri. Itakuwa ni ndoto kusema kwamba tutapeleka maji vijijini kwa style tuliyonayo. Lazima maji tuyafanye kama REA. Lazima twende tukajifunze REA ilifanyaje ikapeleka umeme? Tunaposema Kijiji A kina umeme, inawezekana kuna kaya 200 ndiyo zina umeme, kaya 600 hazina umeme, lakini tunasema kijiji kina umeme. Mtu anaweza kwenda kwenye friji akapata umeme pale; kufanya welding akapata umeme; tufanye maji kama umeme, yapite mabomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa natoa mfano mmoja pale kwangu Bunda. Kutoka Bunda kwenda Nyamuswa kwangu ni kilometa 25. Hesabu iliyopigwa kwa force account inakuwa ni shilingi milioni 800 badala ya shilingi bilioni mbili. Ukinunua mabomba mita 112, ukinunua yale matenki, ukiweka DP; tunataka mabomba yapitie barabarani, ukifika kwenye kijiji waweze DP tatu au nne au sita, yanaendelea hivyo hivyo. Kama yanakwenda Dar es Salaam kutoka Dodoma, kila kijiji barabarani kinapata umeme. Mabomba yaende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya mabomba ni ndogo sana, lakini ukipeleka kwa sasa tulivyo tunavyotumia manunuzi hatuwezi kupeleka maji vjijijini, lazima maji tubadilishe. Hata hiyo tunayoita RUWASA, muundo wake ni shida. Kwa sababu gani? Mkoani mtu aende kupata fedha kutoka wilayani, lazima DP tenda yake ifanyike mkoani. Kuipata hiyo hela kutoka mkoani ni ndoto. Kwanza ukiongeza hela, hakuna kitu kinachoendelea hapa ndani. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima niishauri Serikali, Waziri wa Maji anafanya vizuri sana…

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiri Mheshimiwa Rais anamteua kijana mzuri sana, anafanya kazi nzuri, nawapongeza wote. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, mnielewe, marafiki zetu humu ndani ni Mawaziri, huko nje ni kesi. Waziri akikupindisha, umeshaanguka huko pembeni pembeni huko. (Makofi/ Kicheko)