Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Yahya Ally Mhata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Mpango huu, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wapiga kura wangu wa Jimbo la Nanyumbu kwa kura nyingi walizonipatia katika Uchaguzi Mkuu uliopita. Nami nawaahidi wasiogope, niko hapa kwa ajili yao na nitawawakilisha kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze moja kwa moja katika kuchangia Mpango huu wa Mwaka Mmoja na wa Miaka Mitano uliowasilishwa jana. Kwanza naomba nijielekeze katika sekta ya afya, jinsi gani itakavyoweza kuongeza mapato yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa medical tourism. Tumeona jinsi gani sekta ya afya ilivyoweza kupiga hatua katika miaka mitano iliyopita. Tumeona zahanati karibu 1,198, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya 99, Hospitali za Rufaa 10 na Hospitali za Kanda tatu. Sasa hospitali hizi zinawezaje kuongeza uchumi wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukulia mfano wa India, wameweza kutumia sekta ya afya kuongeza mapato katika nchi yao. Tunajua wagonjwa wengi walikuwa wanakwenda India. Ni wakati wetu sasa hivi nasi kutumia hospitali zetu kuwavutia wagonjwa kuja katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna balozi zetu katika Afrika. Tutumie balozi zetu kutangaza huduma bora za hospitali zetu. Hawa wakija, watakuja na dola, wataacha katika nchi yetu. Wakija kutibiwa watafanya shopping, wata-stimulate uchumi wetu. Kwa hiyo, ni vizuri balozi zetu zitumike kikamilifu katika kuitangaza nchi yetu hasa huduma za afya ambazo tumeziboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nishawishi, katika zile wilaya ambazo ni pembezoni, mfano Wilaya yangu ya Nanyumbu tumepakana na Msumbiji, nilitarajia kabisa Hospitali yetu ya Wilaya ikapatiwa vitendea kazi vizuri ili wagonjwa wale wa mpakani waje kutibiwa katika nchi yetu. Wakija watakuja na dola, wataziacha ndani ya nchi yetu na halikadhalika uchumi wetu unaweza kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni upande wa madini; tumeona jinsi gani Serikali yetu ilivyofanya katika kuhakikisha kwamba katika miaka mitano ijayo inafufua Shirika letu la STAMICO ili kuwawezesha wachimbaji wadogo waweze kujikwamua kiuchumi. Hili eneo la madini ni zuri sana endapo litatumika katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Nanyumbu tunayo madini, lakini nina masikitiko makubwa kwamba yameachwa bila kuendelezwa. Wizara ya Madini imefungua duka la ununuzi wa madini, lakini nikawa najiuliza, duka hili linamnufaisha nani? Kwa sababu madini yapo, lakini kuna mgongano mkubwa kati ya Wizara ya Madini na Maliasili. Vijana wanataka kwenda kuchimba madini, wakienda wanakutana na PFS, wanaambiwa hakuna kuingia msituni. Wakienda wanakutana na TAWA, hakuna kuingia. Sasa kuna contradiction hapo, madini yapo lakini hizi Wizara mbili zinagongana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hizi Wizara mbili zitusaidie vijana wetu ili waweze kufanya shughuli zao, wafuate taratibu gani mahali ambapo pana madini lakini yapo ndani ya msitu? Madini yale lazima yakachimbwe, kwa sababu madini hayapatikani kiholela, hayapatikani barabarani, yapo ndani ya msitu au mbuga. Kwa hiyo, naomba hizi Wizara mbili, nami nawashauri sana, madini haya yasipochimbwa, yatachimbwa kwa njia ya udanganyifu. Kule kwetu mpakani tusipoangalia, wale majirani zetu watakuja kuyachukua na hatutapata chochote. Naomba sana tutumie nafasi hii kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata ajira kwa hizi Wizara mbili kufanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kilimo. Kilimo chetu sisi watu wa Kusini hasa Wilaya yangu ya Nanyumbu tunalima sana korosho. Mwaka 2020 tumeathirika sana na uzalishaji wa zao la korosho, lakini Wizara haijaja na majawabu kwa nini zao la korosho halikuzalishwa? Nilitegemea Wizara ya Kilimo itueleze uzalishaji umepungua kwa sababu ya moja, mbili, tatu; vinginevyo tunawavunja nguvu sana wakulima wetu. Wamefuata taratibu zote lakini korosho hazikuzaa na Wizara imekaa kimya. Kwa hiyo, tunategemea Wizara itusaidie.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni ufuta. Tumeuza ufuta kwenye vyama vya msingi, hatujalipwa fedha zetu. Wakulima hawajalipwa. Wizara itusaidie, vyama vya ushirika vinatuangusha. Tunaomba wakulima wale walipwe fedha zao ili iwa-motivate mwakani walime tena.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nashukuru sana. (Makofi)