Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa dakika tano kwa kweli kuchangia ni chache nitakwenda moja kwa moja katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajielekeza katika Sehemu ya Tatu ya Mpango huu wa Tatu inayozungumzia kukuza ushiriki wa sekta binafsi kwenye maendeleo ya kiuchumi. Mipango yetu ni kutengeneza ajira milioni 8 na katika kutengeneza hizi ajira asilimia karibu 80 tunategemea zitoke katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika Taarifa ya World Bank na ambayo imo katika Mpango huu ambao Serikali imeuwasilisha, hiyo Ripoti ya Easy Way of Doing Business, sisi Tanzania tuko nafasi ya 141. Pamoja na kuwa kuna kasentensi pale kanasema kwamba tumefanya vizuri kutoka 144, lakini kwangu mimi if we are serious kutengeneza ajira milioni nane mimi naona hatujafanya vizuri, lazima ilenge kwenda katika digits mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika East Africa sisi tumeshindana tu na Burundi. Katika SADC sisi tunashindana tu na Zimbabwe. Sasa katika hii hali ya kuvutia uwekezaji na kutengeneza ajira milioni nane bila kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara, naona ajira milioni nane zitakuwa ni ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yako mambo ambayo lazima tufanye. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba amesema tutengeneze mabilionea na tusiogope. Jambo la kwanza ambalo tunatakiwa tusiogope ni kusema uhalisia sahihi lakini suala la pili tusiogope hata sisi wenyewe kuthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya kutengeneza mabilionea mimi nasikitika sana, kule Mafinga unakuta mtu kauza miti yake, milioni 300, 400, sisi kule uchumi tunamshukuru Mungu, inakuja sijui Task Force, I don’t know whatever you call it, akaunti inafungwa. Mimi nilitarajia niulizwe kwamba wewe Cosato Chumi mfanyabiashara, kwa nini unafanya biashara akaunti haina hata milioni tano, lakini don’t ask me kwa nini nina milioni 500. Wewe tafuta mbinu zako za Kiserikali, angalia je, hii milioni 500 ya Chumi ni safi au siyo safi? Ukinifungia akaunti you cripple me down, tutatengenezaje mabilionea na hizo ajira milioni nane? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pale Mafinga tozo katika Sekta ya Mazao ya Misitu ziko 13, viwanda vitano vimefungwa. Imagine kama kiwanda kimoja kinaajiri watu 300, tayari watu 1,500 hawana ajira. Pia umekosa SBL na PAYE; tutatengeneza kweli ajira milioni nane katika mazingira haya? (Makofi)

Kwa hiyo, katika kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali, ni lazima kwanza tuwe wakweli wa nafsi. Ukweli wa nafsi ni lazima kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara. Mimi nasema ni wajibu wetu Wabunge na Serikali kwa ujumla kwa sababu wakati mwingine kweli tutasema TRA lakini mimi nimekwenda TRA wananiambia hii SBL ukiwa hujalipa zaidi ya tarehe 07, penati yake kwa kampuni ni 225,000, kwa individual 75,000. Pia hata kama umelipa ila hujafanya online filing kuna penati yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa angalia nimelipa lakini bado kuna penati, namuuliza Afisa wa TRA anasema bwana, Mkuu hii ni sheria tena na wewe ni Mbunge mlipitisha wenyewe. Kwa hiyo, wao at some point wanatekeleza sheria. Kwa hiyo, kuelekea blueprint na kutengeneza mazingira bora ya biashara yako mambo ni kisheria yaleteni humu turekebishe. Yako mambo ni Kanuni, Mawaziri wenye dhamana elekeeni huko ili lengo la kutengeneza ajira milioni nane iwezekane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelekea huko, pamoja na kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara yako masuala ya miundombinu. Pale Mafinga kwenda Mgololo wakati wa mvua unakuta semitrailer kumi zimepaki wiki nzima zimekufa barabarani haziwezi ku-move; umesimamisha uchumi. Yale malori yangesafiri kwenda na kurudi ungejaza mafuta, Serikali ingepata fuel levy maisha yangeendelea, lakini zipo zimesimama siku tano. Sasa kati ya mambo ambayo tunatakiwa tufanye ni pamoja na suala zima la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mafinga ukishajenga barabara ya Mafinga – Mgololo kama alivyosema asubuhi ndugu yangu Mheshimiwa Kihenzile na barabara ya Mtwango – Nyololo, una-speed up uchumi. Kama Serikali ilikuwa inapata shilingi bilioni 10 matokeo yake utapata shilingi bilioni 50 mambo mengine yataendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho katika suala hili la kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara ni suala la umeme. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kalemani, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kazi nzuri angalieni umeme ni huduma, at some point ni biashara. Kule ambako kuna viwanda vingi watu wanataka kuzalisha mtapata pesa kama Mafinga, leta huo umeme. Leta umeme watu wawekeze, tulipe bili zikawapelekee watu umeme sehemu nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho nakuomba kwa ridhaa yako…

NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono hoja, naomba tuwe wakweli wa nafsi na Mungu atusaidie. (Makofi)