Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii. Hata hivyo nianze na kuchangia machache katika sekta hii ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara na Serikali kuzifanya High Schools zote nchi nzima ziwe chini ya Wizara ya elimu na TAMISEMI ibaki na Primary Schools na „O‟ Level Secondary Schools tu. Hii itasaidia sana Halmashauri za Wilaya na Miji yetu kujikita zaidi kuboresha shule tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2006/2007 Serikali iliamua kwa maksudi kusaidia Mikoa, ambayo ipo nyuma kielimu. Mikoa hiyo ni pamoja na Kigoma, Singida, Mtwara, Lindi na Katavi. Mikoa hii ilikuwa inapata fedha za ziada kila mwaka shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia kujenga madarasa, mabweni ya wasichana na nyumba za walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zilisaidia sana na kwa Mkoa wa Kigoma hali ilianza kubadilika, ajabu ni kwamba, baadaye 2011/2012 fedha hizo zilisitishwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri sana fedha hiyo, irejeshwe ili Mikoa iliyobaki nyuma kielimu iweze angalau kupiga hatua. Huu ulikuwa mpango maalum ni lazima Serikali iangalie hali hii ili kuweka uwiano mzuri katika nchi yetu na baina ya Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha Ukaguzi wa Shule; kitengo hiki kimezorota sana na sehemu nyingine shule za msingi na sekondari hazikaguliwi kabisa! Ni vizuri kitengo hiki kiwe kitengo huru na kisimamiwe na Wizara moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu malipo ya Walimu katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu; malipo ya walimu yahakikiwe vizuri na walipwe stahili zao za matibabu, likizo, likizo ya uzazi, kupanda vyeo na kadhalika. Walimu wengi wanalalamika sana, Wizara ya Elimu na TAMISEMI harakisheni uhakiki ili walimu hawa walipwe fedha zao mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Ujenzi wa Maktaba ya Wilaya Kasulu; Halmashauri ya Mji wa Kasulu tulijenga jengo la maktaba lenye ukubwa wa ghorofa mbili. Tulishirikisha wadau mbalimbali wa elimu kama vile TANAPA na UNHCR tukafika ujenzi wa asilimia 65. Tafadhali Wizara au Serikali saidieni juhudi za wananchi hawa, tupeni nguvu. Tukipata shilingi milioni 200 zitasaidia sana kukamilisha jengo hili na litaanza kutumika. Ni matarajio yetu mwaka 2016/2017, Wizara itaangalia namna njema ya kufanikisha na kukamilisha mradi huu muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ujenzi wa Kasulu Science Grand School; Mkoa wa Kigoma wenye Halmashauri Nane tumeanza mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari ya Sayansi. Mkoa wa Kigoma ulianza kazi hii kutuma Suma JKT, kazi imeanza na hadi sasa shilingi milioni 600 zimetumika. Tunaomba Serikali na Wizara ya Elimu isaidie mradi huu muhimu kwa wakazi wa Mkoa wa Kigoma. Tumeanza tusaidieni kukamilisha ndoto yetu ya kujenga shule hii muhimu ya sayansi. Matarajio yetu ni kwamba, shule hii baadaye tutaifanya ni Chuo Kikuu cha Sayansi na kitaitwa Kigoma University of Science and Technology.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Kasulu tumetoa eneo la ekari 115 kwa ajili ya ujenzi wa shule hii. Eneo hili limepimwa na sasa tuna – process hati ya kumiliki ardhi hiyo. Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Kigoma tumeanza, tunahitaji msaada wa Wizara ya Elimu ili ndoto yetu iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.