Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika siku ya leo. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai wake na leo tuko hapa tunaendelea kuwakilisha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kuchangia kuhusu mpango huu kwanza nikigusa suala la uwekezaji wa ndani ya nchi. Tumekuwa tukitarajiA mengi kutokana na utajiri wetu wa rasilimali nyingi zilizomo ndani ya nchi. Mipango na maneno, wenzetu Chama Cha Mapinduzi mnaongea sana, mnapanga sana, mipango hii ukichukua toka ilivyoanza mpaka leo kwa hakika tungekuwa hatupo hapa tulipo lakini tunapanga hatutimizi mipango yetu, sijui kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, toka sijaingia katika Bunge hili tumekuwa tukisikia suala la Liganga na Mchuchuma. Nilipoingia ndani ya Bunge hili nilibahatika kuwepo kwenye Kamati ya Uchumi, Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ni kati ya mmoja wa mwanakamati tuliokwenda kutembelea maeneo yale. Kwa kweli katika kutembelea maeneo yale tuliiona shani ya Mungu ilivyo kubwa ya utajiri mkubwa wa chuma ambacho Mwenyezi Mungu ametujalia katika nchi yetu. Yamepangwa, yamepangwa lakini hadi leo tumeshindwa kutumia Mradi ule wa Chuma cha Liganga na Mchuchuma katika kuwaletea wananchi maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nchi yetu iko katika ujenzi wa miundombinu ya nguvu kweli kweli, nimshukuru Rais wetu kwa kusimamia ujenzi wa miundombinu katika nchi hii. Laiti mipango tuliyoipanga, Chuma cha Liganga na Mchuchuma kingeanza kuzalishwa leo hii ingekuwa hatuagizi chuma kutoka nje katika kujenga reli ambayo tunaijenga ndani ya nchi yetu. Waheshimiwa pigeni makofi kwa maneno haya mazuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imebaki ni story lakini hatutashiba maneno, Watanzania wanataka vitendo, tuliyoyapanga tuyaoneshe kuyatenda kwa vitendo. Mradi ule wenzetu nchi jirani wanaulilia na kutuona sisi Watanzania ni watu wa ajabu sana kwamba tunajaliwa rasilimali ambayo ni mali kubwa kweli kweli duniani, ilitegemewa leo Tanzania tunaiuzia Afrika nzima chuma kutoka Liganga lakini matokeo yake imekuwa tunaletewa story kila mwaka. Nataka nimuombe Rais wangu, viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi, isimamieni Serikali yetu itekeleze mradi huu muhimu kwa uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu mnyonge mnyongeni haki yake mpeni na anayetenda jema msifu mchukie kwa sura yake na mengine lakini katika suala la kuchukua maamuzi magumu kwa maendeleo ya nchi Mheshimiwa Rais amefanya vema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Rais ni Waziri wa Ujenzi alitamani kupanua barabara kutoka Ubungo mpaka Kibaha, lakini bahati mbaya hakufanikiwa. Alipoingia madarakani ametekeleza mradi ule mpaka nikajiuliza laiti leo ingekuwa wazo lile hakulifanyia kazi, basi kutoka Chalinze mpaka Dar es Salaam tungetumia saa ngapi? Bila shaka tungekesha, tungelala Kibaha lakini limetekelezwa. Sasa nimuombe Mheshimiwa Rais maamuzi magumu aliyoyachukua kwa kutekeleza mradi ule wa Kibaha mpaka Ubungo achukue maamuzi magumu pia kutekeleza Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa wafanyabiashara. Kama tunataka nchi yetu tuendelee lazima wafanyabiashara wetu wasaidiwe. Tatizo kubwa linalowakwaza wafanyabishara hasa wadogo wadogo ni utitiri wa kodi zinazowekwa na TRA katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunasema wafanyabiashara wakubwa wanaondoka lakini hata hawa wadogo nao watapotea kwa sababu kodi zimezidi ukubwa wa biashara zao. Ukiacha kodi, makadirio yasiyo na ukweli ni mengi. Wafanyabiashara wengi wanaofunga biashara ni mfanyabishara amefanya biashara yake anapelekewa makadirio anaambiwa wewe unadaiwa milioni 500, ukiangalia biashara haifiki milioni 300, mfanyabiashara huyo kweli atakaa? Lazima atatafuta namna ya kuacha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuunge mkono sana Mheshimiwa Musukuma jana kwa jinsi alivyoyaona haya na akayaweka wazi. Kwa yale aliyoyazungumza na Kanuni zetu zinatukataza kurudia, nitaishia hapo lakini tuangalie utitiri wa kodi uliopo kwa wafanyabiashara wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano hai tu, toka hapo nje, utaona hao wajasiriamali wanaouza nguo, vitenge na mashuka, wanakwamba mashuka kutoka Uganda, why not kutoka Kariakoo Dar es Salaam? Yameshuka bandari ya Dar es Salaam, yamesafiri yamekwenda Uganda, wafanyabiashara wetu imekuwa ni nafuu kwao kwenda kuchukua Uganda wakarudisha hapa kuliko kuchukua Kariakoo wakaleta hapa Dodoma, why? Bado hatukai tukajiuliza kuna tatizo gani? Tatizo nchi zilizotuzunguka wameweka kodi zinazolipika, sisi tunataka utajiri kwa wafanyabiashara hao kumi waliojikusanya, haitawezekana, tupanue wigo wafanyabiashara walipe kodi inayolipika ili wawe wengi nchi yetu ipate kodi nyingi na tuweze kuendelea. Nadhani hiyo imeingia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala utawala bora, katika ukurasa wa 40, kifungu 2.6.3.3, naomba ninukuu kidogo: “Utawala bora, uwajibikaji na utoaji wa haki. Katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Pili, Serikali iliendelea kupambana na rushwa, kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kujenga miundombinu ya utoaji wa haki kudumisha utawala bora”. Naishia hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nimsifu Rais kuwashinda nyie CCM. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake kwa kuiheshimu Katiba ya nchi hii. Kabla yetu alitangulia kuapa kuilinda na… malizia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameendelea kuwa ni mlinzi wa Katiba. Uamuzi wake wa kumtuma Mheshimiwa Humphrey Polepole (Mwenezi) awaambie wana CCM kwamba hataongeza kipindi cha utawala, ni ishara ya Rais wetu ya kuilinda na kuienzi Katiba. Atakuwa ni Rais wa kwanza katika ukanda wetu wa nchi za Afrika ambaye baadhi ya Wabunge wake wanamwomba aongeze muda lakini tayari ameweka msimamo wa wazi na alimtuma Mheshimiwa Polepole.

Mheshimiwa Polepole waambie CCM Mheshimiwa Rais hana shida ya kuongeza muda. Alikutuma na video zinatembea tunaziona kwa nini unawaacha kina Mheshimiwa Sanga hapa wanaendelea kupotosha, kwa nini hamheshimu mawazo ya Mheshimiwa Rais? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita nilimwambia Mheshimiwa Ally Keissy, alinyanyuka na kujipendekeza hivi hivi, nyi nyi nyi nyi! Nikamwambia nchi hii ni ya kidemokrasia na Rais anaheshimu Katiba na Rais wetu ameshasema hataongeza muda. Kama mna wasiwasi hamna mtu wa kuwa Rais sisi wapinzani tunao. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, why Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni mzuri sana…

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Khatib, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Humphrey Polepole.

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia nafasi hii kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge ambaye alikuwa anaendelea kuzungumza kwamba masuala ya Chama cha Mapinduzi yanazungumziwa kwenye vikao vya Chama cha Mapinduzi. Hapa Bungeni Wabunge wana uhuru wa kutumia uhuru wa Bunge kuzungumza lakini kinachozungumzwa huku ndani hakiathiri msimamo wa Chama cha Mapinduzi ambao tumekwishakuutoa. Msemaji wa Chama ni Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli na kama si yeye mimi husema kwa niaba yake, Mheshimiwa Rais hataongeza muda lakini isizuie watu kuzungumza huku Bungeni. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khatib, nadhani umeipokea taarifa hiyo?

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea si ni nzuri! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale wenzangu ambao wanadhani kuja hapa wakasema Rais atake asitake, hataki sasa, mwamtafutia nini? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na utawala bora, Mahakama imejenga majengo mengi lakini kujenga majengo ya mahakama, shule na hospitali lengo ni kutoa huduma kwa wananchi. Ili huduma zipatikane, ni lazima iambatane na mambo mengine, watendaji na vifaa ni muhimu katika kukamilisha majukumu ya Mahakama. Mahakama ni industry na ili iweze kuwa productive ni lazima ipate material. Material ya Mahakama ni Waendesha Mashtaka kupeleka ushahidi kwa wakati ili kuzifanya Mahakama ziweze kutenda kazi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa mahabusu si utawala bora, nchi yenye utawala bora…

Mheshimiwa Mwenyekiti, unanipa dakika tatu za nyongeza?

MWENYEKITI: Hapana. (Kicheko)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Ahsante sana.