Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Mpango wa Mwaka Mmoja na Mpango wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo amewasilisha mafanikio ambayo yamefikiwa kwa miaka mitano iliyopita na matarajio ya miaka mitano ijayo. Inatupa faraja kwamba nchi hii tutasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere huko nyuma alitangaza Kilimo cha Kufa na Kupona, wengine sasa wamekuja na slogan nyingi. Kusema ukweli wananchi wengi walioko vijijini wanahusika na kilimo, lakini kilimo chetu hiki ni cha kutegemea mvua wakati Mungu ametupa ardhi yenye maji chini. Ni vizuri Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo zikaja na mpango wa kila eneo kuliko na shamba tuchimbe visima virefu, tusafishe maji, tusukume, tutengeneze miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima wetu waweze kulima kwa awamu karibu tatu kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri sana wakulima kulima miezi minne wanapumzika miezi nane, kibiashara haikubaliki. Mfanyabiashara halisi hupenda kufanya biashara kila siku bila kupumzika. Tumpeleke mkulima wetu afanye biashara, kwa sababu kilimo ni biashara, ndipo tutafikia kipato cha juu kwa kila mwananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni mawazo ambayo yanapaswa yaanze sasa. Kwa sababu tumezungumza sana miaka mingi, Bunge hili litaisha, Bunge lijalo litaisha na mengine. Ni vizuri mipango hii ikaanza kutekelezwa kwenye uongozi wako, tukaacha legacy kwenye kilimo cha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote ili Mpango wa Maendeleo ufanikiwe, ni lazima wananchi na viongozi wake wawe tayari. Kwa nchi yetu ya Tanzania viongozi wako tayari na wananchi wako tayari kwa sababu wakati wote wanawajibika kikamilifu, kwa hiyo, ni mambo tu ambayo tunatakiwa tufanye. Tulipokuwa tunaandaa mazao matano ya kimkakati, ni vizuri tukaandaa na viwanda vya kimkakati ili kuhakikisha kwamba tunakuza uchumi wa kilimo na kukuza ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la pamba. Kulikuwa na Mpango wa C2C (Cotton to Clothes). Mpango huu hauwezi kufanikiwa kama Serikali haitaamua yenyewe kuwezesha sekta binafsi kama dunia ilivyoweza kuwezesha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, unapotaka kutengeneza kiwanda cha majora, yaani vitambaa vya aina mbalimbali kama kitambaa cha suti, kitenge, kanga, jeans, t-shirt au shati, unahitaji uwekezaji usiopungua Dola milioni 100, kwa sekta binafsi haiwezekani. Dola milioni 100 tunazungumzia shilingi bilioni 230, benki zinaweza ku-collapse.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea ziliwezesha sekta binafsi. Ukienda Bangladesh, pamba yetu ya Tanzania inaliwa na kiwanda kimoja tu. Kweli tunavyo viwanda vidogo vidogo hivyo vya nyuzi, vitambaa, haviwezi kumaliza raw material tuliyonayo hapa. Kwa hiyo, ili tukuze uchumi ni lazima Serikali iweke guarantee kwa sekta binafsi ziweze kukopesheka duniani ili tuweze kuwekeza na tutoe majora ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa majora, kwanza tutakuwa na uhakika wa bei halisi ya pamba. Kwa sababu mnyonyoro wa thamani tutaujenga vizuri ili kuhakikisha kwamba mkulima huyu ananufaika. Ndipo tutakapokwenda sasa kwenye viwanda vya nguo ambavyo vilikuwa vinazungumzwa hapa na wenzangu, kwamba mtu mwenye cherehani tano au nne, hivyo ni viwanda. Ukienda Vietnam, kila familia ina kiwanda nyumbani kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tubadilishe mawazo yetu, NEMC ije na mawazo chanya. Kwa sababu hapa kwetu ukitaka kuweka kiwanda kwenye nyumba yako unaambiwa unaharibu mazingira. Ukienda China unakuta familia moja, chumba kimoja inatengeneza mabegi; familia moja chumba kimoja inatengeneza simu; ndipo sasa utaweza kwenda kwenye viwanda vikubwa. Huwezi kuanzia juu ukaja chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yetu iweke guarantee kwa wale walio tayari, kama sivyo, Serikali tu- sacrifice, shilingi bilioni 230 ni nini, tuipe Jeshi lijenge kiwanda kikubwa, wafungwa waendeshe kiwanda, watoto wa JKT waendeshe kiwanda, tutafikia uchumi ambao tunautarajia. Kama hatutafanya hivyo, tutakuwa tunazungumza pamba ambayo haitusaidii sana, tunaagiza nguo kutoka nje na pamba tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali, lazima iamue, tunajenga madaraja na barabara…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga nilitaka kukukumbusha tu kwamba sasa huo ndiyo uchangiaji wa Mpango. Ile habari ya barabara ya kutoka mahali fulani kwenda kwenye kijiji changu, hiyo subirini wakati wa bajeti. Sasa hivi tueleze Mpango, ili mpango huu ukatuletee hela Serikalini, Serikali iwe na fedha halafu sasa ndiyo tutaongea habari ya barabara yako ya kata moja hadi nyingine. Kama unavyotueleza kwamba tukiwekeza kwenye pamba tunaweza tukatoka. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Kiswaga, endelea. (Makofi)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunajenga barabara, madaraja, stendi na masoko kadhaa, kwa nini Serikali isiamue kutoa shilingi bilioni 230 ikakabidhi hata Jeshi kama sekta binafsi haiaminiki, hapo sisi tutakuwa soko la Afrika kwa vitambaa na tutamaliza matatizo mengi. Wale wakija kununua vitambaa, watalala hoteli, kuna kodi ya Serikali; watakunywa bia, kuna kodi ya Serikali; watatumia taxi, watatumia mafuta, kuna kodi ya Serikali; wenye taxi watanunua tairi, kuna kodi ya Serikali. Kwa hiyo, tusiangalie tu jambo moja tukashindwa kuangalia kwa upana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wowote wa Maendeleo duniani huhitaji kuongeza ajira, kukusanya kodi na kuweka mifumo mizuri ya kuhakikisha mpango ule unatekelezeka. Kuna wakati taasisi zetu wakati mwingine zinaweka mipango ambayo haitekelezeki na kandamizi. Mfano, wenye mabasi; kuna kitu kinaitwa LATRA, wameingizwa kukata tiketi kwa mfumo, ambapo kimsingi wanalazimishwa kuweka fedha kwenye mashine. Kama una magari 40 lazima asubuhi uweke milioni 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wafanyabiashara wetu wa mabasi wana uwezo, kwanza basi wanakopeshwa, halafu unapoweka huo utaratibu, maana yake kuna 2% wanakatwa hawa wafanyabiashara. Hiyo pia, hakuna mkataba wowote ambao unawafanya wafanyabiashara hawa wawe na imani kwamba fedha hizi zikikatwa kwa mtandao zitarudi au zitaenda Benki?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Ni hoja muhimu lakini muda wako umekwisha.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wapewe EFD machine wafanye kama ambavyo wafanyabiashara wengine wanafanya bila kupitia utaratibu huo. Hapa tutaongeza ajira, Mama Ntilie watapika chakula, wapiga debe nao watafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. Tutachangia kwenye Mipango mingine. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga, huja-declare interest, una mabasi mangapi? (Kicheko)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina basi ila kwenye pamba.