Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao ni wa kuanzia mwaka 2021/2022 na 2025/2026. Nianze tu kwa kusema kupanga ni kuchagua, unavyopanga mpango matarajio ni kwamba, mpango ule angalau utatekelezeka kwa asilimia kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepanga katika maelezo ya Mheshimiwa Waziri, wanasema wametenga karibu trilioni 118 za miradi, lakini nikisema niseme jinsi fedha zinavyotolewa katika mipango ambayo imekuwepo toka Mpango wa Kwanza, Mpango wa Pili na sasa tunakwenda Mpango wa Tatu; nichukulie tu mfano sekta ya viwanda, kwa fedha za maendeleo ambazo zilitolewa kwa mwaka 2016/2017 ilikuwa ni asilimia 44; mwaka 2017/2018 ilikuwa asilimia 9.5; na mwaka 2018/2019 ilikuwa asilimia 6.5 tu. Sasa hivi ukijumlisha kwa miaka hiyo unakuta kwamba, utekelezaji wake ulikuwa ni asilimia 20 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunavyokuwa tunapanga hii mipango wananchi wanakuwa na mategemeo makubwa sana ya kuhakikisha kwamba, mipango tuliyopanga itatupeleka katika uchumi ambao tumesema tunataka kufikia, uchumi wa kati, lakini nashukuru Mheshimiwa Muhongo ameielezea vizuri jinsi ambavyo tunaweza tukafikia katika uchumi huo wa kati kama tukifuata mikakati na jinsi ambavyo tutaishauri Serikali iweze kufikia katika huo uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya viwanda ambayo kwa miaka minne, Awamu ya Nne mwaka 2015 tulifikia kiasi cha dola 1.3 bilioni, lakini kwa Awamu ya Tano tulishuka, mwaka 2018/2019 ilikuwa ni dola milioni 894, mwaka 2019/ 2020 dola 805.2 milioni. Sasa unaangalia thamani ya mauzo ya nje ya viwanda, hii value of exports tumeshuka, sasa kama tumeshuka, je, nini ambacho kinakwamisha tusifike kule? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotukwamisha ukiangalia masuala mengi hatuna mazingira muafaka ya uwekezaji. Mazingira ya uwekezaji yamekuwa ni ya kusumbua wawekezaji, watu wanafilisiwa, watu wamehamisha biashara Mheshimiwa Musukuma amezungumza, utitiri wa kodi, sasa hivi vyote vinaikosesha Serikali mapato. Kwa hiyo, Serikali lazima iangalie namna ambavyo inaweza ikarekebisha tozo mbalimbali zikawasaidie wawekezaji na uchumi uweze kupanda na tuweze kunyanyua kipato hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hakuna mkakati mahususi kwa vijana wetu. Nasema kwa vijana kwa sababu, unapowekeza kuanzia kwa vijana mpaka watafika mbele watatengeneza uwanda mpana sana wa maendeleo. Sasa private sector haijapewa mkakati mkubwa, tumeiweka pembeni hatuitilii mkazo, vijana hawaandaliwi kuja kuwa wawekezaji. Kwa hiyo, lazima Serikali iwe na mkakati wa kuhakikisha vijana wanaandaliwa kuja kuwa wawekezaji katika nchi hii. Tunasema vijana ni Taifa la leo, wawekewe mikakati mahususi ya kuhakikisha kwamba, watakuwa wawekezaji wazuri katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine lazima tuwezeshe uchumi wa wananchi kuwa na mtaji. Waziri wa Viwanda aliyetangulia, Mheshimiwa Mwijage, alikuwa anatuambia hata ukiwa na vyerehani vitatu au vinne ni kiwanda, hata ukiwa na blender ni kiwanda, lakini lazima tutengeneze uwezo wa kuwawezesha watu kuwa na mitaji. Hii itafanya watu kuwa wanawekeza kwenye viwanda, Watanzania hata watu wa nje wanaweza wakawa na mitaji ya kuweza kuwekeza katika nchi yetu. Sasa Serikali iangalie hawa Mawaziri ambao wanakuja wakitamka maneno ya namna hiyo na kuwafanya Watanzania washangae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, enzi za Mwalimu ilikuwa ukitamka kiwanda unajua kuna kiwanda cha TANCUT Almasi, kuna MWATEX, kuna Kiwanda cha Magurudumu, vilikuwa vinaeleweka, lakini leo tunatajiwa kwamba, kuna viwanda elfu nane na kitu ambacho Mheshimiwa Waziri ametamka hapa, lakini ukiangalia vingi viko kwenye makaratasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kKivitendo kwenda ukaviona hivyo viwanda ni changamoto. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri anaporudi kujibu hapa atueleze kinagaubaga uwekezaji huo umewekezwa wapi? Pamoja na kwamba, wametaja baadhi ya viwanda vinne, vitano, ambavyo viko pale kwamba 201 hivyo ni viwanda vikubwa, lakini sijui kuna viwanda elfu nane na kitu ambavyo hivyo havieleweki viko wapi? Naomba ufafanuzi uwepo wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie jinsi ambavyo tutaoanisha kilimo na viwanda. Kilimo tumekitupa kabisa katika, hatujawekeza. Mwaka, kama sikosei 2018/2019, ni asilimia mbili tu ya fedha za maendeleo ndio ilitolewa kwenye kilimo. Kwa hiyo, nashauri tuwekeze katika kilimo kwa sababu, kilimo ni ajira na vijana wengi na asilimia zaidi ya 67 wanaweza wakapata ajira kupitia kilimo, akinababa, wanawake, vijana, wanaweza wakapata ajira kupitia kilimo. Kwa hiyo, Serikali lazima iangalie katika utoaji wa fedha katika bajeti ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tunafanya mipango, tunaisoma kwenye maandishi, utekelezaji Wizara ya Fedha toeni fedha katika utekelezaji katika sekta hii kwa sababu, fedha hazitoki. Tutaona, tutakwenda tutaangalia katika bajeti, fedha ambayo ilitengwa 2020/2021 utakuja kukuta kwamba, asilimia kubwa kabisa haijatolewa. Kwa hiyo, tuombe Serikali itoe fedha kwenye sekta ya kilimo ili hawa watu waweze kufanya kilimo chenye tija na waweze kutumikia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi katika miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kitasaidia sana katika kuongeza pato na mpango ukaweza kufanikiwa, lakini sisi hatuna miundombinu inayoridhisha katika kilimo cha umwagiliaji, sisi tunategemea mvua ambayo Mwenyezi Mungu anatupa. Kwa hiyo, tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji kwa nafasi kubwa, ili tuweze kukidhi hayo yanayotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la ukuaji wa pato la Taifa. Pato la Taifa wanasema linakua, lakini hali- reflect hali halisi. Wanasema pato limekuwa, lakini hali halisi tunaiona, wamezungumza Waheshimiwa Wabunge wenzangu hapa, ukiangalia Maisha ya Mtanzania, hali ni ngumu, watu wanaweza wakasema kwamba, ooh, sijui kuna kubana matumizi, kuna hiki, kuna kile, lakini hili pato la Taifa ambalo tunasema limekua kiuchumi, tunaomba wachumi wenzetu watueleweshe vizuri, wale wakulima wa kule kijijini wanavyosikia pato limekua hawaelewi kwamba, limekuaje? Maisha yanazidi kuwa magumu, vitu bei zinapanda na masuala mengine kama hayo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo…

MWENYEKITI: Sentensi ya mwisho, malizia.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)