Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Ardhi na Mbingu hashindwi na walimwengu apangalo yeye huwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nampongeza Rais wetu na wasaidizi wake. Hapo walipotufikisha wametufikisha mbali, Watanzania tunajionea wenyewe maendeleo yaliyofikiwa katika kuwasaidia wananchi kwenye huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Fedha na wasaidizi wake wote kwa hotuba nzuri walizotuletea za mipango na makadirio. Naunga mkono hoja zote zilizowasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na sekta ya kilimo. Kilimo kimeelezwa kwenye Mpango wa Mwaka Mmoja na wa Miaka Mitano. Naunga mkono hatua mbalimbali zilizoelezwa kwenye hotuba zote za kuimarisha kilimo kama uti wa mgongo wa kumuinua mwananchi mmoja mmoja na kuinua nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kina sekta nyingi lakini nitagusia kilimo ambacho kitahifadhi mazingira yetu. Ardhi yetu tunaihitaji sisi kama tulivyoikuta lakini pia na kuvirithisha na vizazi vijavyo. Nahamasisha kilimo kilimo hai na kilimo hifadhi. Kilimo hai na kilimo hifadhi kinalinda ardhi yetu ili iweze kutumika kwa miaka mingi lakini pia kinatoa mazao ambayo hayana kemikali ambapo kwa sasa ni mazao yenye bei sana katika soko la dunia na wananchi duniani wanayahitaji mazao ya aina hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha bustani ni kilimo ambacho sasa hivi kinaleta hamasa sana kwa vijana na wanawake kwa sababu kina soko kubwa nje ya nchi. Hata hivyo, lazima sasa tupange ardhi yetu, ardhi ya kilimo, ufugaji, viwanda, majengo na mengineyo. Kilimo hiki ukataji wa miti ni mkubwa, tunakata miti mikubwa ya kudumu tunalima bustani. Kwa hivyo, kilimo hiki kina fedha nyingi lakini pia kizingatie hali ya mazingira na hali ya nchi yetu kulingana na mabadiliko ya tabia nchi yanayotukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na waliosema kuhusu mbegu bora. Mbegu bora zinahitajika ili kwendana na mazingira ya nchi yetu, udongo wa nchi yetu na hali ya hewa. Kwa maana hiyo sasa ni vizuri kuwekeza kwenye utafiti. Utafiti unahitaji wataalam na elimu hii ni ya muda mrefu, nashauri Serikali, kuna wataalam wetu wa utafiti ambao wamestaafu lakini sasa wanatumikia nchi za jirani, watafutwe waungane na hawa waliopo ili waje kuendeleza soko hili la kuzalisha mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji ndiyo muarobaini kutokana na hali ya hewa na mazingira ya tabianchi. Kilimo cha umwagiliaji kinatupa usalama wa chakula lakini kitatoa mazao bora kwa ajili ya malighafi za viwandani. Nashauri Sekta ya Maji iimarishwe ili yapatikane maji ya kuhudumia mifugo, viwanda, ukulima na sisi wananchi tupate maji safi na salama. Juzi nilisema Mfuko wa Maji umefanya kazi nzuri sasa unahitaji kujengewa uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzalishaji wa malighafi za viwandani, lakini pia wakulima wana changamoto kubwa baada ya kuzalisha mazao yao, hakuna usafiri wa kutoka kwenye maeneo yanayozalisha hivyo vyakula kuyafikia masoko ya mijini. Mfano maziwa ni bidhaa ambayo inaharibika kwa muda mfupi sana kwa hivyo barabara za vijijini zikiwa mbaya, wakulima wa maziwa wanapata hasara na Taifa letu pia linapata hasara ya kukosa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ujenzi wa maghala na vihenge, naipongeza Serikali imefika hatua kubwa na mipango inaonesha kuna maendeleo makubwa katika ujenzi wa vihenge. Pia katika kuhifadhi chakula na usalama wa chakula, naishauri Serikali mwananchi mmoja mmoja naye aweze kuhifadhi chakula chake kwa mwaka mmoja au miwili. Kwa maana hiyo, kuna viwanda vya wawekezaji hapa nchini tayari wanazalisha mifuko ya kilo 100 na 200 kwa maana ya mwananchi aweze kuhifadhi mazao yake. Ni vyema viwanda vile vikapunguziwa kodi na tozo mbalimbali ili mwananchi aweze kumudu gharama za kununua ile mifuko aweze kujihifadhia mwenyewe chakula chake na watu wake huko nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nagusia kidogo Sekta ya Uvuvi. Uvuvi wa Bahari Kuu tunaipongeza Serikali kwa ununuzi wa meli za uvuvi, bandari za uvuvi na maghala ya kuhifadhia samaki. Kwa vile chombo hiki ni cha Muungano, nashauri Shirika la Uvuvi la TAFICO, kuna mpango wa kuliimarisha, naomba sana na Shirika la Uvuvi la Zanzibar (ZAFICO) mambo haya yaende sambamba ili kuwekeza zaidi katika uchumi wa bahari kuu. Katika Mipango ya Miaka Mitano, nashauri na bandari moja ya uvuvi kule Zanzibar nayo ijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta hiyo ya uvuvi, napenda kuchangia kwenye ukuzaji wa viumbe kwenye maji. Sekta hii ni sekta ambayo haitumii nguvu kubwa. Ni vyema sasa na wala haihitaji elimu kubwa, wale vijana wetu waliomaliza darasa la saba, waliomaliza masomo darasa la tano na la nne, wanaweza kufanya hii sekta ya viumbe kwenye maji. Nina ushahidi mtoto wa darasa la tatu anafuga mwenyewe samaki wa gold fish, anawalisha biscuit tu na anawauza kwa watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana sekta hii inawezekana kwa vijana wetu wa darasa la saba na la tano kufanya sekta ya ukuzaji wa viumbe kwenye maji, kwa sababu ni sekta ambayo haihitaji elimu kubwa, haihitaji utaalam mkubwa. Tukiwekeza hapa tutapunguza wale vijana ombaomba wanaozunguka mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ile Mifuko yetu ya ujasiriamali ya vikundi vya vijana ni vyema sana zikaandaliwa program maalum za vijana hawa, baada ya kumaliza masomo ndio wakapewa ile mitaji sasa kwa sababu tayari wameshapata ujuzi, wameshapata uelewa na kazi watakuwa wanaipenda, kwa hivyo, watakuwa wanafanya kitu ambacho wanakipenda, kwa hivyo, kutakuwa na ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nakuombea dua wewe uendelee kutuongoza vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na timu yake aendelee kutuhudumia sisi wananchi tunamhitaji, tunampenda na tunampongeza sana kwa juhudi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)