Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mpango huu. Kwanza naipongeza Wizara na Mheshimiwa Profesa Mpango kwa kazi kubwa kweli ambayo yeye na wataalam wake wameionyesha kwenye kipindi cha miaka mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nianze kwa kuipongeza sana Serikali hasa sekta ya madini ambayo mimi ni Mjumbe wake, kwa kazi nzuri sana iliyofanya na imetuonesha hata kwenye taarifa kwamba kutokana na kupokea mawazo ya wadau, Serikali imeongeza kipato kikubwa sana kutokana na wadau wa madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Waziri na pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais pale alipotupa nafasi sisi wa darasa la saba tukaishauri Serikali na akatusikiliza. Baada ya kutusikiliza leo Serikali inavuna mabilioni kutokana na mawazo tuliyoyatoa sisi wa darasa la saba ambao ni watendaji wakubwa kwenye Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe tu ushauri kwa upande wa Serikali. Nianze na suala la miradi. Tumeona Serikali katika kipindi kilichopita imekuwa na miradi mikubwa ya mabilioni ya pesa ambayo haina impact yoyote kwenye Taifa na Watanzania wale chapakazi hasa wale wa chini, hatuoni faida ya miradi mikubwa ambayo Serikali imewekeza mabilioni ya pesa. Nimejaribu kuwasikilisha wiki iliyopita, Waheshimiwa Wabunge wengi wanalia kwamba kwenye TARURA hakuna hela; na nikijaribu kuangalia mawazo ya wenzangu huko chini, naona tunafikiria labda kwenda kuongeza kwenye mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mifano miwili mitatu. Mimi nilipoanza Ubunge nilikuwa Kamati ya Ardhi na tulienda kukagua mradi mmoja Morocco kwenye nyumba za watu wenye hali ya chini; nyumba za maskini; yale majengo mazuri yaliyoko Morocco. Tuligombana sana, sijui ndiyo kilisababisha Mheshimiwa Spika, ukanihamisha kunipeleka Kamati ya Madini! Niliwaambia, ikitokea uchumi ukiyumba, humu tutalaza popo. Wapo Wajumbe tuliokuwa nao hawakunisikia. Leo sasa unaona jengo lile limeisha na hakuna chochote kinachoendelea pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya, nataka kutoa mfano tu kwamba siyo mradi mmoja wa Morocco, tunayo miradi kwa mfano Soko la Morogoro, Machinga Complex na sasa tuna Soko la Ndugai. Wote ni mashahidi, yamefeli, ni mabilioni mangapi yametumika? Ni kwa sababu pengine wasomi wanashindwa kutafakari kwamba wanapojenga masoko, stendi kubwa za mabilioni, ile ni huduma. Sasa wanaviweka kama vitega uchumi; na watu wanaowawekea vitega uchumi ni masikini, hawa Mama Ntilie, hawawezi kwenda mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sisi kuingia humu ukumbini kwa sababu hili jengo nalo lilitumia hela nyingi za Watanzania, pengine na sisi tungekuwa tunachajiwa getini, tungeona uchungu kwa yale tunayoyapanga kwa wale wananchi kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba fedha hizi za mabilioni ambazo tunawekeza kwenye vitu ambavyo havizalishi, tungewekeza zaidi kwa watu wa chini. Kwa mfano, tungechukua haya mabilioni, kila Halmashauri ikaandika miradi kama pesa mnazo, tukaenda kuboresha barabara zetu kule vijijini, wakulima watalima vizuri na mazao yao yatasafirishwa kwa bei nafuu. Itakuwa na impact kwenu walaji, mtapata kwa bei ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka kushauri kuhusiana na suala la biashara mitaani. Tusioneane aibu wala tusifichane, kweli hali ni mbaya. Watu wanafunga maduka, watu wamekata mitaji, lakini sioni namna ambayo Serikali yetu na viongozi wetu na Mawaziri labla wanakuja na mawazo mbadala ya kuweza kuona namna gani ya kuwabeba hawa wafanyabiashara wanaofilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimetokea kwenye tasnia ya biashara huko mtaani, nina uzoefu mkubwa. Ni kweli maduka yanafungwa, wala tusifichane. Kwa nini yanafungwa? Tuone namna ya kuzibadilisha sheria. Wafanyabiashara wale waliomo humu enzi za nyuma kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano, ilikuwa inawezekana kukamatwa ukapigwa faini ukalipa. Ilikuwa inawezekana kujadili. Serikali ya Awamu ya Tano hakuna mahali mtu anaweza aka-temper kulipa kodi. Ila sheria zinazotumika kulipisha kodi sasa hivi ni zile zile wakati bado unaruhusiwa kulipa viwili, vinane vinapita bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tuone namna Serikali kama tunaweza; na namshauri sana Mheshimiwa Rais, kwenye hiki kipengele naona kama Mawaziri wanamwogopa Mheshimiwa Rais. Sasa kwa sababu sisi Wabunge ni Wawakilishi wa wananchi wote kwenye maeneo yetu tunayotoka, namwomba Mheshimiwa Rais awaite wafanyabiashara, awaite waagizaji, awaite wenye viwanda na wauzaji. Tukiendelea kufumbiana macho, watu wanafilisika. Ni lazima tuwaite, tuwasikilize, tuone namna na tujifunze kutoka hata kwenye Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipomfuata Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kukamata, nyang’anya, kamata, nyang’anya, tukamwambia Mheshimiwa Rais, utatumalizia hela. Tuite utusikilize. Akatuita, tukamweleza, akapangua kutoka kodi ya asilimia 50 kurudi asilimia saba peke yake. Kwa hiyo, nadhani hata kwa hawa wafanyabiashara wa viwanda, maduka na watu wengine, tukiwaita, tukawasikiliza tutaondoa lawama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukipita huko mtaani, watu wengi tu wanasema, Magufuli amebana. Serikali imebana hela. Imebana wapi? Ni kwa sababu hatujarekebisha kodi rafiki ambazo mtu atalipa bila kuumia na Serikali itakusanya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2016, Mheshimiwa Dkt. Mpango alivyokuja hapa alikisia kukusanya milioni 81 peke yake kwa wachimbaji wadogo, tulibishana sana hapa kama Hansard inaweza ikakumbusha. Nikamwambia hiyo ni kodi ya mtu mmoja, baada ya kutusikiliza hebu leo ona kutoka 4.6 pato la madini mpaka kwenda kwenye five point. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Rais awaite wafanyabiashara awasikilize, haya maneno ya kusema hali ni nzuri, tusione aibu watu wanafilisika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilikuwa namuangalia Mheshimiwa Rais kwenye siku ya sheria alitaja orodha ya benki ambazo zinawadai wafanyabiashara kwamba zimechukua hela na hawajarudisha na benki wameenda mahakamani. Ni kweli, watu wameenda Mahakamani kwa sababu? Sababu ni nyepesi. Kwa mfano, mimi nina mtaji wangu wa shilingi milioni 50, nimeaminiwa na benki shilingi milioni 500, nafanya biashara vizuri nalipa rejesho langu vizuri inafika mahali anaingia TRA anasema tunakudai shilingi milioni 500, zinaenda zile hela za benki. Kesho yake mimi nakuja kuuziwa nyumba, nitakubalije? Ni bora nikimbilie benki na mimi nikapaki tu huko tuelewane. Kwa hiyo, ni vizuri haya mambo Serikali yetu iweze tukayapitia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza juzi wajumbe wanazungumza sana kuhusu Bodi ya Mikopo, mimi nadhani Bodi ya Mikopo inafanya vizuri sana na Serikali inatoa hela nyingi ila nina ushauri mdogo tu. Serikali inaamini ubongo bila mkataba, mtu anakuwa tu na elimu yake amefaulu anaenda kuaminiwa mkopo mpaka anapata degree, karatasi. Kwa nini Serikali isije na wazo mbadala kwamba baada ya kumpa ile degree, kwa sababu sisi tunaohudumia watoto mpaka kupata degree kwa kweli kule vijijini tunakuwa tumeshamaliza na ng’ombe tumezeeka, Serikali ije na dirisha lingine kwamba mtu anapopata degree karatasi kuwe na dirisha la mikopo ya hela wakaanze biashara aweke dhamana ile degree kwenye lile dirisha. Akiweka kile cheti chake cha degree at least hata milioni 10 au 20 tupunguze hizi kelele za watu kukaa wanatembea na ma-degree. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifungua simu za Wabunge wako kila mtu ana CV za watu kutoka Jimboni kwake 10, 20 au 30. Sasa kama mkifungua hili dirisha mkopeshe na mitaji kwa kutumia vyeti tutaweza kuondoa ule usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni la kumuongeza Mheshimiwa Rais muda, mimi naliona tofauti kidogo. Nimejifunza kwenye awamu ya kwanza, ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano ukijenga hoja hapa, nazidi tu kumuomba Rais afikirie hili kwamba kwa nini watu wanasema Rais aendelee? Nikiangalia kutoka huko tulikuwa tumeshapaki anzia treni, ndege tumekata skrepa, treni tulikuwa tumeshaanza kununua skrepa leo hivi vitu vyote vinaendelea. Tunaanzisha miradi mikubwa kwa ujasiri wa mtu mmoja na hakuna ubishi kwamba bila Magufuli mawazo yake yale tusingefika hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tujifunze kwa wenzetu wa Zimbabwe. Mimi siyo msomi lakini kwa sababu ya biashara nimezunguka kidogo. Wazimbabwe walipoamua kuwafukuza Wazungu na kujitegemea Wazungu waliwapimia tu wakasema itafika mahali hawa watakuja kutupigia magoti, wakawawekea vikwazo. Wakafanya miradi yao ilivyokamilika kuwafukuza Wazungu wakajenga mpaka na kiwanda cha fedha. Ilipofika muda zilipoisha karatasi za ku-print pesa wazungu wakawaambia hatuwezi kuwapa hizi material za karatasi kwa sababu mko kwenye vikwazo. Ndiyo Serikali ya Zimbabwe ikaanza kuwa inabadilisha tu Rais anatangaza noti ya milioni moja inakuwa ya milioni 10. Baadaye watu wakaanza kulipwa mshahara kwenye kiroba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe haya mambo ambayo Rais ameyafanya na tumeona mengine yanaangukia 2024, 2025, kwa ujasiri ule ule tunaweza kuona namna kama alivyosema Mzee Butiku juzi tukamuongeza muda kwani kitu gani? Mbona wenzetu wamefanya? Ina maana sisi Watanzania tunaijua demokrasia zaidi ya Wachina ambao ni matrilionea na kila mtu ana teknolojia yake? Wamefika mahali wakasema tumuone kwa mawazo haya, tumuongeze muda hata miaka 20 mbele ili aweze kukamilisha yale ambayo alikuwa ameyapanga. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Musukuma.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho tu…

MWENYEKITI: Muda hauko upande wako. Nakushukuru sana kwa mchango wako.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja asilimia 100. (Makofi)