Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa mimi, nanyi kuturudisha salama na kutuingiza katika Bunge hili. Hakika Mungu ametufanyia mambo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais kunipa dhamana tena kwa mara nyingine ya kuendelea kuhudumu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Pia niwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Kisarawe na familia yangu kwa ujumla kwa mapenzi makubwa ya kunirudisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge. Mchango wangu ambao nimepewa katika Wizara hii ya wananchi nitaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza yale mambo yote mahususi yanayohusu katika maeneo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 20 Novemba, 2015, Mheshiiwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa speech yake hapa Bungeni. Katika speech aliyotoa ukienda katika eneo la pili, maana baada ya kusema rushwa aliizungumza Ofisi moja inaitwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Katika speech yake alisema hafurahishwi na haridhishwi na mwenendo wa ofisi hii katika suala zima la usimamizi wa miradi isiyotekelezwa ndani ya muda, ukusanyaji wa mapato na mambo mengine ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yanamnyong’onyesha Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na niwashukuru Wabunge wote katika kutekeleza speech ya Bunge ile ya kuzindua Bunge la Kumi na Moja kipindi kile nikiwa nimepewa dhamana kuhakikisha kwamba, TAMISEMI inahusika na ujenzi wa zahanati, hospitali za wilaya na halikadhalika vituo vya afya. Kutekeleza hotuba ile tulitoka katika vituo 115 vyenye uwezo wa kufanya huduma ya upasuaji mpaka tumefika vituo 487, ni rekodi ya kwanza tumeiweka. tumetoka hospitali za wilaya 77, leo hii tunakamilisha hospitali 102 mpya ndani ya miaka mitano, lakini tumejenga zahanati zetu 1,198. Katika upande wa afya tunasema eneo tulilopewa Mamlaka ya Serikali za Mitaa tumejitahidi kutimiza wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya pili hii sasa ya ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili Mheshimiwa Rais alikazania tena katika suala zima la huduma ya afya, afya iweze kuimarika na hususan afya zetu za msingi. Katika eneo hili tumejipanga ndugu zangu. Kama tumeweka rekodi miaka mitano iliyopita Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumeazimia kwenda kuvunja rekodi ya kwetu sisi wenyewe na Waheshimiwa Wabunge naomba niwahakikishie tutapambana kila liwezekanalo kuhakikisha tunamaliza changamoto za wananchi wetu katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii nimewaita Wakurugenzi wote wa Halmashauri ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upande wa Tanzania Bara na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya. Katika mwaka wa fedha unaokuja na niwaombe sana Wabunge ninyi mkiwa Wajumbe wa Baraza la Madiwani na Kamati za Fedha, tunaenda kuweka rekodi ya kwanza ya ujenzi wa vituo vya afya visivyopungua 185 ambavyo vituo hivi ni matumizi ya own source kabla hatujapata top up kutoka Serikali Kuu, hii inakuwa ni rekodi ya kwanza tunaenda kuifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaambie Wabunge tumeshaazimia kikao cha leo na Wakurugenzi wote, kuna halmashauri zitajenga kituo cha afya kimoja, zenye bajeti ya kuanzia bilioni moja mpaka bilioni tano. Kuna halmashauri zitajenga vituo viwili kwa own source zenye bajeti kuanzia bilioni tano mpaka 12, lakini kuna halmashauri zitakazojenga zaidi ya vituo vitatu zenye bajeti kuanzia bilioni 12 na kuendelea. Tutapata zaidi ya vituo 185 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ambayo hizi ni fedha za mapato ya ndani kabla hatujaingia katika fedha za Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyozungumziwa ni kuhusu suala zima la TARURA hapa, tumelisikia sana. Mnafahamu tumefanya kazi kubwa miaka mitano japo resource zilikuwa chache, lakini Serikali tunaendelea kulifanyia kazi hili na nishukuru sana Bodi ya Mfuko wa Barabara, hivi sasa wanapitia ile formula kuangalia jinsi gani formula ikae vizuri kwa lengo la kuisaidia TARURA ifanye kazi vizuri. Ndugu zangu Wabunge, naomba tuwe na Subira timu inafanya kazi tutapata majawabu kabla mpango wa bajeti haujafika tutakuwa katika sura nzuri ya kuhakikisha jinsi gani TARURA inafanya kazi yake vizuri, lakini hiyo ikienda sambamba na kufanya resource mobilization, kutafuta vyanzo vingine vya kuisaidia TARURA ifanye kazi vizuri, hii ondoeni shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa elimu ambayo tumepewa mamlaka ya kuhakikisha kwamba, elimu ya msingi tunaisimamia, tunaanza shule za awali mpaka kidato cha sita. Miaka mitano hii tulifanya kazi kubwa, ukiangalia shule kongwe kati ya shule 89 tumekamilisha shule 86 mpaka hivi sasa. Ninyi Wabunge ndio mashahidi, maeneo mlikotoka shule kongwe zilikuwa zimechakaa sana zimechoka, leo hii kazitazame tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 89 katika shule kongwe peke yake, lakini tunaenda kufanya kazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu katika mpango wetu wa ujenzi wa shule za kata 1,000 ambao tunatumia zaidi ya shilingi trilioni 1.2 ndani ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kujenga zile shule 26 za wasichana, lakini tutahakikisha kata zote 718 ambazo hazina sekondari za kata, Wabunge naomba niambieni, tunajenga sekondari kata zote ndani ya Tanzania. Tunaenda kusimamia program ya elimu bila malipo ambayo kila mwezi sasa inatumika hivi sasa shilingi bilioni 24. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda katika mradi mwingine unaitwa TACTIC katika suala zima la kuboresha miji yetu. umefanya vizuri ndani ya miaka mitano. Halmashauri zenu zote zenye manispaa na halmashauri za miji leo hii mkienda mnashangaa, tumejenga barabara nzuri, kuweka taa za barabarani, kujenga na madampo sehemu nyingine, miaka mitano inayokuja ni miaka ya funga kazi ndugu zangu Wabunge. Tunaenda kushughulika na mradi wa TACTICS katika miji 45, tunataka Watanzania walioondoka Tanzania 2010 wakirudi 2025 wapotee miji yao wasiweze kuifahamu.

Hii ndio kazi kubwa tunayoenda kuifanya. Katika eneo hilo ndugu zangu Wabunge naomba niwahakikishie hatutanii na hii miaka mitano ni miaka ya mchakamchaka miaka ya kazi. Naomba niwaambie Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Serikali kwa ujumla itatoa ushirikiano wa kutosha mambo yaende sawasawa bila kikwazo cha aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na issue ya suala zima la mikopo ya akinamama, vijana na wenye ulemavu. Tunaenda vizuri, tumenza awamu ya kwanza kutengeneza sheria na juzijuzi nimeshasaini mabadiliko ya kanuni kuhakikisha akinamama na wenye ulemavu waweze kupata fursa nzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeniishia, nilishukuru sana Bunge hili, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)