Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge letu Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, napenda kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai, afya njema na leo tuko hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi Taifa na Mkoa wangu wa Katavi kwa kuniamini na kunituma tena kuja hapa Bungeni. Napenda kuwashukuru sana akina mama wa Mkoa wa Katavi kwa kuniamini tena kunipa nafasi kwa kipindi cha pili, leo hii tena nimekuja Bungeni kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kuwatumikia Watanzania na kwa kuwapa moyo wa kufanya kazi mpaka nchi yetu imetoka kwenye lile group la nchi maskini na imeingia kwenye group la nchi ambazo zina uchumi wa kati. Ni wajibu wetu sote sisi Watanzania kushirikiana na Mheshimiwa Rais lakini na kumpongeza kwa bidii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Waziri Mkuu na Mawaziri wote. Nawapongeza Wabunge wote mliorudi kwenye Bunge la Kumi na Mbili; hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, nimeisoma hotuba yake aliyokuja kutufungulia Bunge letu la Kumi na Mbili, lakini pia aliyofunga kwenye Bunge la Kumi na Moja. Mimi nakwenda kwenye page ya 16 pale mahali ambapo Mheshimiwa Rais ameongelea jinsi ya kuleta nidhamu ya kazi maofisini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema wazi, katika umri wangu huu ina maana nilisoma katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, nikafanya kazi kwenye Serikali ya Awamu ya Pili, ya Tatu na ya Nne na hii ya Tano nikaingia Bungeni. Niliona mmomonyoko wa maadili katika maofisi kwa awamu zote hizo tano. Kwa hiyo, bila kuuma maneno napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kurudisha nidhamu kazini. Awamu ya Tano oyee, nidhamu kazini ilikuwa imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano kwenye sekta ya afya. Mama anakwenda kujifungua unakuta wale manesi wanashona vitambaa. Mtu anaweza akawa anaumwa uchungu anaita nesi njoo nisaidie anaambiwa mtapike mtoto. Hizo zilikuwa ni lugha za zamani, siku hizi hazipo, sasa hivi nidhamu imerudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho napenda kukizungumzia hapa ni suala la amani. Suala la amani katika nchi yetu hii tunatakiwa sisi Wabunge tuliomo humu ndani tulihubiri, tuilinde hii amani ili watoto wetu wanaokuja waje waikute amani hii. Ni wajibu wetu kuitunza, kuilinda na kuiendeleza amani kwa faida yetu na kwa faida ya wajukuu zetu. Sisi tumekuta nchi hii ikiwa na amani, lugha zetu ziwe za kuendeleza na kudumisha amani, zisiwe za kubomoa, ziwe za kujenga kwa sababu sisi sote ni Watanzania, Tanzania ni moja lakini ina Tanzania Visiwani na Tanzania Bara.

Naomba Wizara ya Muungano itoe elimu ya Utanzania kwenye redio. Mtu ukiwa Zanzibar jisikie kwamba wewe ni Mtanzania, ukiwa Tanzania Bara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TASKA R. MBOGO: Ukiwa Tanzania Bara jisikie kwamba wewe ni Mtanzania. Tanzania ni moja, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)