Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya iliyo bora, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii leo ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako Tukufu nianze kwa kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Msalala kwa kunipatia imani kubwa hii ya kuweza kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, niseme sisi kama Wanajimbo la Msalala, hotuba hii imeleta mapinduzi makubwa sana katika Jimbo langu la Msalala. Niliarifu Bunge lako Tukufu hili kwenye ukurasa wa 37, lakini pia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ya 2020, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika Jimbo la Msalala ameweza kutupatia miradi mikubwa kabisa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ametupatia mradi mkubwa wenye zaidi ya bilioni 13 ambao ni mradi wa maji unaotoka Magu kuja Ilogi. Hata hivyo, hajaishia hapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ametupatia mradi mkubwa kabisa wa maji unaotoka Kagongwa kwenda Isaka unaogharimu kiasi cha bilioni 23. Pia hajaishia hapo, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kutupatia mradi mwingine wa maji ambao unatoka Nduku Mtobo kwenda Busangi, ambao unagharimu kiasi cha shilingi bilioni nne nani kama Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumeona azma yake ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, wilaya kwa wilaya. Katika Jimbo langu la Msalala, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameweza kutupatia barabara mbili zenye kiwango cha Lami, barabara hizi ni barabara inayotoka Solwa kuja kupita Kata ya Ngaya na Kata ya Bulinge kuja Kahama lakini pia ametupatia barabara nyingine inayotoka Bulyanhulu kuja Segese mpaka Kahama. Naiomba Wizara ya Ujenzi iweze kuona namna gani inaweza kuanza utekelezaji wa barabara hizi mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala nzima la afya, niseme tu mbele yako Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sisi Wanabulyanhulu alianza kupambana juu ya kupitia mikataba upya ya madini na mikataba hiyo sisi kama Wanamsalala tumeweza kunufaika pakubwa sana na mikataba hii. Leo hii ninapozungumza tunapokea fedha za CSR. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Doto Biteko, Waziri wa Madini aweze kufanya ziara na kuona namna gani sasa Wanamsalala tunaweza kunufaika na fedha hizi za CSR.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ucheleweshwaji wa miradi mbalimbali inayopangwa kwa ajili ya kutekelezwa na watu hawa wa mgodi zinazotolewa na fedha za CSR. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Doto aweze kufika katika Jimbo langu la Msalala ili tuweze kufanya kikao na watu hawa tuone namna gani wanaweza kutekeleza miradi hii ya CSR ili iweze kuleta tija kwa wananchi wa Jimbo la Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imeweza kutufanya Jimbo la Msalala kuhama kutoka uchumi wa chini na kuhamia uchumi wa kati. Ninavyozungumza hapa tuna vituo vinne vya afya katika Jimbo langu la Msalala, lakini pia tunaenda kujenga kituo kingine kwa fedha zetu za ndani za jimbo, tunaenda kujenga kituo cha afya katika Kata ya Isaka. Niiombe TAMISEMI na Waziri Mheshimiwa Jafo, kaka yangu aweze kutusaidia kutupatia vifaa tiba ili kituo cha afya kinachokamilika kiweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu sio hilo tu, lakini tumekuwa na uhaba wa watumishi katika sekta ya afya katika Jimbo la Msalala; nimwombe Mheshimiwa Jafo aweze kutuangalia kwa jicho la huruma Wanamsalala, tuna uhaba wa Walimu pia, naomba ndugu yangu atusaidie katika suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu juu ya kauli yake ya kuhakikisha kwamba tunaenda kuongeza madarasa katika nchi nzima. Katika Jimbo langu la Msalala napenda nimhakikishie Mheshimiwa Waziri Mkuu tulilipokea wazo lake hilo na maagizo yake hayo kwa kutekeleza ujenzi wa madarasa na tumeweza kuongeza madarasa katika kila kata mawili. nami kama Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie Mheshimiwa Waziri Mkuu nilitoa lori la cement kuhakikisha kwamba naunga juhudi za ujenzi wa madarasa hayo. Kwa sasa tunavyozungumza tuko katika hatua nzuri na baadhi ya shule tayari madarasa hayo yameanza kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la ajira..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeisha Mheshimiwa.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)