Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Maryam Omar Said

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Pandani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. MARYAM OMAR SAID: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kwanza katika kipindi hiki cha pili cha leo cha kujadili hoja ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili, nichukue fursa hii kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa makundi matatu ambayo yalishiriki katika kuhakikisha leo Maryam nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu, Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee ziende kwa familia yangu kwa jumla. Pia nikishukuru Chama cha Wananchi CUF kupitia Mwenyekiti wake shupavu, Mheshimiwa Prof. Ibrahim Lipumba kwa kuweza kunisimamisha nikawa mgombe katika Jimbo la Pandani kule Pemba. Pia nitoe shukrani zangu za dhati kwa wananchi wangu wa Jimbo la Pandani kwa kunipa ushindi wa asilimia
56.6 ambazo zimenifanya leo hii nasimama kifua mbele ndani ya Jimbo huku nikijidai kuwa ni mwanamke pekee katika majimbo 18 ya Pemba niliyepata nafasi ya jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo, naomba nichangie hoja ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nikisimama zaidi katika miundombinu ya viwanja vya ndege pamoja na bandari kwa upande wa Pemba. Nilifurahi sana pale Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aliposema atashirikiana na Rais wetu wa Zanzibar bega kwa bega katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Naamini tumepata majembe mawili, tunamuamini Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa sababu amelelewa na Rais wetu ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunaamini yale yaliyoko Tanzania Bara basi na Tanzania Visiwani yatafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa kumtaka Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aongeze kasi zaidi katika kushirikiana na Rais wetu wa Zanzibar katika suala la miundombinu hususan viwanja vya ndege pamoja na bandari, Wapemba wanalalamika, wananung’unika. Tufahamu kwamba Pemba imo katika sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini tupo nyuma. Leo hii nikitaka kusafiri nikiwa Pemba basi nianze kuweka booking ya ticket ya ndege siku mbili kabla nikikosa hapo ndege ya asubuhi ama jioni naikosa. Wapemba wanaomba pia ndege ya Air Tanzania kama jina lilivyo Air Tanzania kiwanja cha ndege kiboreshwe na iweze kufika Pemba pia, wana ndoto, wanaota kila siku ndege ya Air Tanzania ipo Pemba lakini bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa upande wa bandari tumechoka wananchi wa Pemba kutumia saa kumi na mbili tukiwa ndani ya Bahari tu tunaitafuta Unguja. Tunahitaji tuboreshewe miundombinu ya bahari kwa kupata boti za kisasa kwa hali yoyote ile kama ambavyo Unguja na Bara ama Unguja na Dar es Salaam inaunganishwa kwa saa kadhaa tu unatoka Unguja unafika Dar es Salaam. Ni ndoto zetu na sisi Wapemba, tunataka tutumie saa chache kutoka Pemba kuja Unguja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais tunakuamini, ni jemedari mzuri, unaweza kuleta maendeleo kwa kiasi fulani lakini tunaomba umshauri vizuri Rais wetu wa Zanzibar hususan atuangalie kwa jicho la hurumu Pemba kwa miundombinu ya usafiri. Wapemba bado tuko nyuma, wananchi wanalalamika na ndiyo maana ukakuta kwamba siasa kali inahamia Pemba, kimaendeleo bado tupo nyuma. Tunahitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu wananchi wa Pemba mbali na mawili, tuangaliwe kwa jicho la tatu, tuko nyuma katika sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, ahsante sana. (Makofi)