Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nami namshukuru Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais, Chama changu cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Kilombero kwa kunipa imani ya mimi mtoto wa fundi charahani mwenye nywele za kipilipili leo kusimama hapa kuwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni imani yangu ya dhati kaka yangu Mheshimiwa Polepole atanisaidia kufikisha shukrani zangu zote kwa chama kwamba sisi vijana tunawashukuru sana. Sisi vijana wadogo ambao tumepata nafasi ya kuingia katika Bunge hili tuna imani kubwa na ma- senior mliokuwepo humu mtatusaidia sana kutufundisha na kutuelekeza bila kutuacha tuharibikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Wabunge wenzangu wengine wamechangia, nami nitumie fursa hii kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kwanza, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwa vijana na katika maendeleo ya nchi yetu. Nitachangia katika sekta mbili au tatu, ya kwanza miundombinu ambayo ameizungumzia katika ukurasa wa 26.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 mimi nilikuwa mgombea wa Ubunge wa Chama cha Mapinduzi japokuwa sikutangazwa, Mheshimiwa Rais alifika jimboni kwetu, tulimuomba ujenzi wa barabara ya lami ya Ifakara – Kidatu kwa kiwango cha lami. Barabara hii haikuwapo kwenye Ilani lakini kwa mapenzi yake Mheshimiwa Rais aliahidi ataijenga na akaleta mkandarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wasaidizi wa Mheshimiwa Rais kuifuatilia barabara hii kwa ukaribu. Namshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Eng. Chamuriho alifika ameona changamoto za Mhandisi Mshauri (consultant) ambaye amekuwa aki-delay katika mambo ya GN na designing ili ahadi hii ya Mheshimiwa Rais iweze kutimilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo hilohilo kwa kuongezea kidogo ni kwamba katika swali langu la msingi Mheshimiwa Waziri amejibu hapa kwamba barabara hii itakamilika Oktoba 2021. Sisi ambao tuko site kule ukitazama unaona muda huu ni mfupi sana. Kwa hiyo, naomba Wizara ifuatilie kwa makini barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni katika elimu. Mheshimiwa Rais akituhutubia hapa Bungeni aliahidi jambo la msingi kwa dada zetu, wasichana wa nchi hii kwamba atajenga sekondari za watoto wa kike kila mkoa. Naomba Wizara husika iliharakishe jambo hili lifanyike kwa wakati. Mkoa wetu wa Morogoro, Jimbo la Kilombero liko katikati ya Mkoa mzima. Pendekezo langu Wizara itakapojenga shule hizi ijenge katikati ya Mkoa ili kutoa nafasi kwa majimbo na wilaya zote kupeleka watoto pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili katika elimu, mjadala umekuwa mwingi sana hapa kuhusu suala la elimu ya chuo kikuu. Mheshimiwa Rais amesema katika hotuba yake ukurasa wa 33 mabilioni ambayo Serikali inatoa kwa mikopo ya elimu ya chuo kikuu. Pendekezo langu ni kwamba vile vyuo vya umma, mathalani University of Dar-Es-Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Serikali inalipa mfagizi, dereva mpaka anaepeleka karatasi pale, kwa nini tusifikie hatua ya kusema kwamba vyuo vya umma wanafunzi wasilipe ada kwa sababu Serikali inapeleka pale kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mjadala huu wa mikopo, Bodi ya Mikopo, asilimia za kukatwa kuja kulipa ni kubwa, anapata huyu huyu hapati, lakini kwa sababu Serikali inapeleka huduma zote katika vyuo vya umma kwa kuanzia nilikuwa nashauri tuanze kulifikiria hilo. Mheshimiwa Rais amefanya vizuri sana katika elimu bure lakini tunakokwenda tufikirie vyuo vya umma ambavyo Serikali inahudumia kila kitu kwa nini mtoto wa Kitanzania asiende kusikiliza lecture akapata ufahamu? Kuwe na mjadala baadaye ama anatokea nyumbani ama anatokea wapi lakini afike apate nafasi ya kusoma chuo kikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mjadala hapa kuhusu kazi nzuri ambazo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya. Mimi kubwa kuliko yote ni suala la kunifanya nijiamini kama Mtanzania. Mimi kama kijana wa Chama cha Mapinduzi nimezunguka katika nchi za Afrika na tulikuwa na mafunzo ya vijana wa Afrika, hasa Afrika ya Mashariki, kuna nchi hapa walikuwa wanajisifia na Marais wao, leo sisi tukienda tunaheshimika kwa Rais wetu, ndiyo salamu yetu ya kwanza. Kubwa kuliko yote ni hilo Rais amenifanya mimi najiamini kila sehemu na kila wakati amekuwa akirudia kusema Watanzania tuwe makini tunaweza, Tanzania ni tajiri, ile imani inatufanya tunashinda vita. Hilo ni kubwa kuliko yote na ndiyo maana linakuza mjadala hapa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)