Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, maana nilishakata tamaa, nilijua leo sipati nafasi. Namshukuru Mwenyezi Mungu Subhana-huwataala kwa kutuwezesha kuwepo hapa. Nakishukuru chama changu kwa kunipeleka mbele ya wananchi wa Kinondoni na hatimaye wakanichagua kwa kura nyingi sana. Nawaambia wananchi wa Kinondoni niko imara, nina nguvu, nina akili ya kuwatumikia kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru familia yangu ikiongozwa na mke wangu Latifa Hasnal Faizal na dada yangu kipenzi Zera Abbas Muhammad Ali ambao kwa kipindi chote wamekuwa ni silaha kubwa katika kuniwezesha kusimama nikawa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati akizindua Bunge hili la Kumi na Mbili, yenyewe inatosha kuwa ni dira ya vipaumbele kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu hili kwa kipindi cha miaka mitano inayokuja. Hata wataalam wa mipango wanaweza wakafyonza humo ndani na wakapata vitu ambavyo Watanzania wengine watavipokea kwa mikono miwili. Siyo rahisi kuandika hotuba kama ile, Rais lazima atakuwa ni mtu mwadilifu, ambaye amemweka Mungu mbele kuangalia Watanzania wanahitaji nini, awafanyie nini na nchi yake iko wapi na anataka aione iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu ni mtu ambaye anaongozwa na hofu ya Mungu. Hii inanifanya niseme kwamba viongozi wa Serikali wawe ni wateuliwa Mikoani au Wilayani, Serikali Kuu wawe na hofu ya Mwenyezi Mungu katika kufanya kazi zao. Hapo tutafanikiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nisome maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo ameyasema. Aliwauliza binadamu lakini akajibu mwenyewe; iko katika Surat Azuma aya ya 9, nitaisoma kama ilivyo, anasema: “Hal astawi? (Anauliza, wanafanana?) Aladhina yaalamuna waladhina laayaalamuna. (Yule anayeijua na yule ambaye hajui, hawa watu wamoja wanafanana hawa?) Akajibu, Mwenyezi Mungu hakusubiri watu wamjibu, akasema, balaa (hapana).” Maana yake imekusudiwa mtu mwenye hofu ya Mwenyezi Mungu ni mtu ambaye amepata daraja kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Tushukuru kwamba tuna Rais ambaye ana hofu ya Mwenyezi Mungu na ndiyo maana mipangoyake inakubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, sisi Wabunge wote humu tumekuja hapa kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, tunapozungumza humu ndani hatuzungumzi kwa utashi wetu, ni utashi wa wananchi waliotutuma. Wananchi wakitueleza kwamba nendeni Bungeni kazungumzieni suala fulani, kaiambieni Serikali yetu suala fulani, Serikali ni ya wananchi na Bunge ni la wananchi, wapi tunakinzana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii kila Mbunge akisimama anaongelea kuhusu TARURA; Spika anazungumzia TARURA, kila mtu anazungumzia TARURA, jamani sasa ifike wakati Serikali msikie hili. Huo ndiyo uadilifu ninaouzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengi humu ndani tukizungumza, maana yake ni kauli ya Mungu, ni kauli ya wananchi na hapo ndipo tutapata mafanikio. Kuna options nyingi tu ambazo zimewahi kujadiliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama TANROADS hatuwezi tukapunguza fedha zake, iunganisheni na TARURA iwe ni kama division ya TARURA, wawe na mfuko mmoja mkubwa, wafanye kazi pamoja. Siyo lazima tuwe na utitiri wa vyombo, hapana, vyombo vinaweza vikawa vichache, kazi zikawa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli is alone, anasaidiwa na watu wachache lakini anafanya kazi kubwa, it is possible! Kwa nini hatumuigi Mheshimiwa Rais? Mbona kaitembelea Tanzania nzima? Wote humu ndani tumepata fadhila zake, tumetumia jina la Mheshimiwa Magufuli katika kupita. Aljazaul-ihisani ilal-ihisani (Anayekufanyia wema, mrudishie wema). Mheshimiwa Dkt. Magufuli katufanyia wema mkubwa katika Taifa hili. Tumrudishieni basi wema kwa kuwatumikia wananchi wake. (Makofi)

(Hapa kengele iligonga kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nisije siku nyingine nikaomba habari za Kinondoni Waheshimiwa mkanikatalia, lakini nataka…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imeshagonga. Ahsante sana.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Basi nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)