Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuzungumza jioni hii ya leo. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwenye wingi wa rehema kwa kunijalia afya na kunipa kibali cha kuweza kusimama ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niunge mkono hoja ya hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Ili kukuza uchumi pamoja na sekta ya uzalishaji ni lazima tuimarishe miundombinu ya barabara pamoja na nishati ya umeme. Tunamshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli tumeshuhudia ndani ya utawala wake barabara zimejengwa na zinaendelea kujengwa, reli ya SGR inajengwa, bwawa la Nyerere katika Mto Rufiji linajengwa, hizi zote ni juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna imani miradi hii yote ikikamilika nchi yetu itaendelea kupaa, wananchi wataweza kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo hivyo wataweza kusafirisha mazao yao katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa sababu usafiri utakuwa ni wa uhakika, lakini pia tutakuwa tumeweza kupata umeme wa uhakika. Kwa maana hiyo wataweza kukuza kipato chao na kuchangia pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie kuhusu kilimo, kilimo kimeajiri watu wengi sana takribani zaidi ya watu asilimia 58 ni wakulima wakiwemo wanawake. Hivyo basi, naomba niishauri Serikali, bajeti ya kilimo iongezwe kusudi iweze kufanya vizuri katika kilimo. Ninyi wote ni mashahidi, mchana tulienda nyumbani kupumzika lakini tulirudi tukiwa tumepata chakula, chakula kinachotokana na kilimo. Kwa hiyo, naomba niwashawishi Waheshimiwa Wabunge, tuhakikishe bajeti ya kilimo inaongezwa ili wananchi wetu ambao wengi wamejiajiri kwenye kilimo waweze kunufaika kupitia kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ikiongezeka tutaweza kupata pembejeo na dhana bora za kilimo, lakini kilimo cha umwagiliaji kitaweza kufanyika vizuri kwa sababu miundombinu itakuwepo. Kwa mfano katika Mkoa wetu wa Kigoma, tunalo bonde la Mto Lwiche, bonde nzuri sana, ambalo tunaweza kulima kilimo cha umwagiliaji tukalima kilimo cha mpunga, kikaweza kuwanufaisha wananchi kwa chakula, lakini pia wakizalisha mchele wanaweza kuuza hata nje ya nchi wakaweza kuongeza kipato chao na kuweza kuchangia pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusu zao la mchikichi; tunaishukuru sana Serikali kwa kulifanya zao la mchikichi kuwa zao la kimkakati, Serikali imeweza kutoa miche ya mbegu lakini bado haitoshelezi kwa sababu wananchi wameitikia kilimo hicho. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee kutusaidia kuongeza miche ili wananchi waweze kuzalisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu zao la mchikichi pamoja na alizeti vikiweza kulimwa na kutoa matunda, tutaepukana kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi kwa sababu pesa nyingi tumekuwa tukizutumia kwenda kununua mafuta nje ya nchi, lakini tukizalisha sisi wenyewe tutaweza kunufaika kupitia kilimo chetu cha ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba kuchangia kuhusu ushirika, katika ushirika bado hatujafanya vizuri kwa sababu wananchi kwanza hawana elimu, lakini hata Maafisa Ushirika wenyewe bado ni wachache. Kwa hiyo, elimu inayotolewa kwa Vyama vya Ushirika, SACCOS na SACCAS bado haitoshelezi, kwa hiyo, naomba niishauri Serikali iweze kuongeza juhudi za kutoa elimu katika Vyama vya Ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nimalizie kwa kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Kigoma, walionichagua kwa kura nyingi, walifanya ya kwao lakini wakanichagua nikaweza kurudi ndani ya Bunge lako Tukufu, kwangu mimi Wajumbe wale ni wema kwangu sana. Nawashukuru sana lakini nakishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuweza kuniteua na kugombea hatimaye nikaibuka mshindi. Ahsante. (Makofi)