Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon Salim Mussa Omar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gando

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu Azzawajal kwa kutujalia siku ya leo sote tukiwa wazima na akili timamu. Pili, nikishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kunichagua miongoni mwa vijana ambao wameaminika kupeperusha bendera katika nafasi hii ya Ubunge katika Jimbo ambalo kwa mara ya kwanza linaongozwa na Chama cha Mapinduzi toka 1995. Nawaahidi wananchi wa Jimbo langu la Gando Pemba Kaskazini kwamba sitowaangusha. Naamini huko wanakonisikia sasa hivi au watakaponisikia wataamini kwa yale ambayo yameshaanza kutendwa na Mbunge huyu ndani ya miezi hii miwili mitatu ambayo tumeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika mchango wangu kidogo kwa kutumia dakika chache kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Magufuli kwa yafuatayo. Kwanza, namshukuru sana katika hotuba yake aliposema kwamba ataleta meli nane Tanzania, nne zitaelekezwa upande wa Zanzibar na nne zitabaki upande wa Tanzania Bara. Hii imeonesha wazi kwamba Mheshimiwa Rais wetu kumbe anafahamu kwamba sisi Wazanzibar hatuna madini, madini yetu yako katika bahari. Ndiyo maana licha ya utofauti wa ukubwa uliopo baina ya Tanzania Bara na Zanzibar aliweka uwiano sawa wa mgawanyo wa meli zile, ahsante sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, papo hapo niiombe Serikali yangu ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Bunge hili Tukufu kwa kupitia Waziri wetu wa Muungano mama yetu Mheshimiwa Ummy Mwalimu afanye juhudi za kuweza kushauri na kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanza sasa mchakato mzima wa kutoa mafunzo katika suala zima la bahari kuu. Kwa sababu licha ya kwamba meli hizo zitakuja, tunahitaji utaalam kutoka kwenye kidau au viboti vidogo tulivyovizoea mpaka kwenda kuyazoea mameli haya yanayokuja kunahitaji taaluma kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali iweze kujikita katika suala la utoaji wa elimu kwenye hilo. Naamini ushirikiano ambao Mheshimiwa Rais aliaahidi katika hotuba yake yataenda kuifanya Zanzibar kuwa kama Brunei In shaa Allah. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake hakusita kuzungumzia suala la ushirikiano wa dhati kabisa na Rais wa Zanzibar kwenye suala la amani na utulivu sambamba na kuulinda Muungano na Mapinduzi Matukufu. Nimwombe kaka yangu Mheshimiwa Mkuchika na Waziri wa Mambo ya Ndani wasitoe fursa na mwanya hata kidogo kwa wale watu wachache wa Zanzibar ambao wanatumia platform za kidini lakini pia na za kisiasa kutaka kuchokonoa amani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, nimwombe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu aliahidi kwamba atatoa ushirikiano kwa Rais wa Zanzibar basi afanye hivyo. Nakumbuka alipomtuma Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja Pemba katika kampeni yake kumwakilisha alipopiga simu pale alisema atakuja Pemba. Tunamuomba basi Mheshimiwa Rais aje Pemba tupitie katika yale maeneo ambayo ni kero ili aweze kutoa msukumo wa hali ya juu na kumshawishi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar. Kwa nguvu yake mimi naamini mambo yataenda kwa kasi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, namwomba Mheshimiwa Rais pia katika suala la business dispute ambalo alilizungumzia kwenye hotuba yake lipewe kipaumbele kwa sababu yapo makampuni yana shida nyingi sana. Sisi vijana ambao tulimaliza vyuo tukaamua kujiajiri mwanzo tumekumbana na mambo mengi ambayo mwisho wa siku hujui uende ukalalamike wapi. Unakuta muda mwingine unafanya kazi na taasisi ya Serikali wana-freeze pesa, wanashindwa kuzirejesha Serikalini, wanazibakisha ndani ya akaunti ya kampuni yako, kushtakiwa hushtakiwi, pesa ukiangalia ipo lakini kukopesheka hukopesheki na mwisho wa siku unaua mpaka ile taaluma ndani ya kampuni yako. Kwa hiyo, naiomba hii business dispute hii ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo ili sisi tulioelekea kujiajiri na wenzetu ambao wanamaliza shule sasa hivi wanaofikiria kujiajiri waweze kujua wapi wanaelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)