Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa wachangiaji. Katika kuchangia kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba zote mbili; wakati wa kufunga Bunge na wakati wa Ufunguzi wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Bunge linaahirishwa au likihitimishwa, ndiyo kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, jemadari na ndiyo iliyofanya Wabunge wengi turudi hapa ndani, kazi hii! (Makofi)

Katika ufunguzi, mwelekeo huu wa miaka mitano, naomba nichangie na nianze na elimu. Tunapozungumzia elimu bila malipo na ndiyo imefanya watoto wetu wengi wapatikane katika maeneo yetu, ambapo wazazi wao walikuwa hawawezi kuwapeleka shule. Elimu bila malipo kwenye sekondari tunasema, msingi na sekondari, ombi langu kwa bajeti inayokuja na Rais wetu mpendwa, isiwe elimu bila malipo kidato cha kwanza mpaka cha Nne. Inatupa taabu hata sisi Wabunge kule Majimboni wakati fulani kusema. Tunaomba iwe mpaka kidato cha sita yaani kuanzia kiadto cha kwanza mpaka cha sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunadhani hili linaweza kuwa ni zuri. Tunamwomba Waziri mwenye dhamana katika bajeti ambayo inakuja, hebu tujipange vizuri, tuishauri Serikali kupitia Rais wetu kwamba elimu bila malipo iendelee mpaka mpaka kidato cha Sita, yaani cha Kwanza mpaka cha Sita.Tutakuwa tumekwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamechangia hapa juu ya mikopo, nilikuwa nafuatilia jana. Kwenye mikopo hii kuna baadhi ya watu ambao watoto wetu hawa wanafadhiliwa na taasisi mbalimbali na baadhi ya watu. Inapofika mahali yule mtu aidha ameshindwa kuendelea kumfadhili na kadhalika; unakuta mtoto amefaulu vizuri Kidato cha Sita na kuendelea anashindwa mkopo na baadaye anakuwa hana mahali pa kwenda kwa sababu wafadhili wake wameshindwa na kadhalika. Nami nina mifano hai mingi, watu mbalimbali na wananchi wanavyokuja kwangu, najua hii iko pia kwa Wabunge wenzangu.Ombi langu, jamani wapewe bila masharti, bila kujua amesoma wapi na kadhalika. Maadamu ana vigezo vya kupata mkopo, apewe bila masharti ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la umeme, ndugu zangu Waziri mhusika yuko hapa, Mheshimiwa Kalemani. Unajua penye kazi nzuri ambayo mtu amefanya lazima tumpongeze. Amefanya kazi nzuri sana. Ombi langu sasa kwenye jimbo langu, najua na kwa wenzangu, asubuhi tumetoka kuongea, Kijiji cha Mutanga kule, walianza kupeleka nguzo, lakini wamesimama. Ombi kwa Mheshimiwa Waziri, wananchi hawa wapewe umeme wa kule Mtanga na Ingangidung, utakuwa umetusaidia na baadhi ya maeneo, nitawasiliana na Waheshimiwa Madiwani, baadhi ya vitongoji ambavyo leo amezungumzia kwamba ni lazima na vyenyewe sasa tulete ili waweze kupata umeme. Kwa hiyo, nitawasiliana na Madiwani, mwishoni mwa wiki hii nitamkukabidhi maeneo ambayo bado hayajapata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye afya, kazi iliyofanyika ni nzuri sana ya kujenga vituo, zahanati na kadhalika. Ombi langu, kwenye Jimbo langu la Makambako wananchi wanaonipenda sana, nami nawapenda sana kwa dhati kabisa kabisa; na Rais wao wanampenda sana; ombi langu tumekuwa tukizungumzia habari ya X-Ray na Ultrasound. Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana yuko hapa, hivi kweli Mji wa Makambako ambako ndiyo corridor ya kwenda Songea, Mbeya na wapi, ndiyo Jiji kubwa, hivi hatuna X-Ray. Chumba cha X-Ray tulishakijenga, kipo tayari. Tunaomba katika bajeti tunayokwenda nayo tupate X-Ray, Mheshimiwa Waziri atakuwa ametutendea haki katika Mji wetu wa Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji; Mheshimiwa Aweso yuko hapa, ambaye ni Waziri wa Maji. Naomba ndugu yangu Waziri; Mawaziri wote wanafanya kazi nzuri, wanaendana na kasi ya mwenyewe, wote! Sasa Mji wa Makambako ndiyo mji mkubwa katika miji yote kwa ukanda. Ndiyo corridor pale jamani; kwenda wapi na wapi kama nilivyosema. Ule mradi mkubwa ambao tunapata mkopo nafuu kutoka Serikali ya India, ni vizuri sasa katika Miji 26 ile na Mji wa Makambako upo, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa amesimama hapa atuambie ni lini mradi huo wa maji Makambako utaanza ili nikawaambie wananchi wangu wa Makambako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba leo asubuhi Mheshimiwa Waziri amenijibu kuhusu maji, sasa aseme hapa kwamba maji hayo ni ya mwakani au ni ya mwaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara, naishukuru Serikali kwa Mji wangu wa Makambako, tumepata fedha za lami kilometa 3.5 Mjini pale, tunaishukuru sana Serikali. Hata hivyo, wenzangu wameongelea chombo cha TARURA. Naomba kwenye bajeti hii tutakayoanza, naomba tuongezewe fedha ili barabara zetu ziweze kupitika msimu wote. Kwa hiyo, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu hapa kuna maboma mbalimbali ambayo yamejengwa; madarasa, zahanati na kadhalika. Ombi langu, Wizara hasa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, ahakikishe maboma haya ambayo wananchi wamejenga pamoja na Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wabunge tuliomo humu ndani, yanaisha kwa kipindi hiki.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, siyo kwa umuhimu…

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wameongelea hapa juu ya Rais wetu kumwongezea aidha muda. Kuna watu wengine ni kama dhambi hivi kumwongezea. Ndugu zangu, mtu huyu amefanya kazi kubwa kwa miaka mitano iliyoisha na mipango ya miaka hii mitano, ombi langu hapa ndani, atake asitake tumwongezee muda ili aweze kufanya kazi na kukamilisha mipango yake vizuri katika nchi hii. Kabisa! Ili aweze kufanya kazi yake vizuri ili mipango aliyoipanga iweze kukamilika. Atake asitake, tumlazimishe! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, nilisema hapa kama mnakumbuka kipindi fulani kwamba China wamefanya hivyo na mahali pengine wamefanya hivyo, siyo dhambi kwa mtu anayefanya vizuri. Hata ninyi Wabunge mliorudi maana yake mlifanya vizuri, ndiyo maana watu walisema tena mrudi, kwa hiyo, siyo dhambi tena kumwongezea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)