Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo alitoa Bunge la Kumi na Moja na Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, kwanza naunga mkono hoja na niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano katika vipindi vyake vyote viwili kwa kazi kubwa na nzuri na jinsi hotuba zake Mheshimiwa Rais alizokuwa akizitoa hapa Bungeni na kwenda kujibu mahitaji ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo nataka kushauri Serikali yetu ya Awamu ya Tano, katika kupitia hotuba ya Mheshimiwa Rais alipokuwa akihutubia Bunge hili tukufu alisema anao mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba anajenga uwezo kwa Watanzania kuwa mabilionea lakini kuhakikisha kuwa wakulima wanaweza kupata mbegu zilizo na tija. Mambo haya yanaenda sambamba pamoja na kuwa na elimu bora lakini na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tumekuwa jinsi Serikali inavyofanya kazi zake vizuri lakini nataka kutoa ushauri wangu sehemu ya uwekezaji. Wazungumzaji wenzangu wamegusia suala zima la umeme, kuna changamoto ya umeme katika maeneo mbalimbali. Namwomba sana Waziri mwenye dhamana ya nishati kuhakikisha maeneo yaliyo na changamoto ya umeme hususan kwa Mkoa wetu wa Simiyu na Mkoa wa Katavi, tumeona jitihada zinazofanywa na Wakuu wa Mikoa kwenye maeneo husika lakini changamoto ni kutokuwa na nishati ya kutosha kwenye maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni Serikali kuhakikisha inapeleka pembejeo kwa wakulima kwa muda muafaka. Tunapozungumzia utajiri kwa Watanzania tunategemea kilimo, yaani kilimo cha pamba, kahawa, tumbaku, mahindi na kadhalika. Yote haya yakitekelezwa, naamini tutaendelea kutengeneza mabilionea wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asubuhi Mbunge wa Hai kauliza swali la msingi sana na Mheshimiwa Naibu Waziri alizungumzia kwamba ushirika ni hiari kwa wananchi lakini jambo hili limekuwa na sintofahamu. Serikali inasema haiingilii ushirika, ni hiari lakini kuna maeneo mfano ni hivi sasa tunavyoendelea na Bunge hili, baadhi ya maeneo choroko zimeiva ambapo mama anapeleka choroko kilo mbili au tatu lakini kunakuwa na mpango wa stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia stakabadhi ghalani tuelewe kwamba sisi kama Watanzania hatuna uwezo wa kuhifadhi hicho chakula au kukitumia kwa pamoja, tunategemea nchi za nje kuichukua malighafi hiyo. Hivi sasa bei za choroko ni nzuri sana zinakwenda mpaka 1,500 lakini inaporudi kwenda kwenye stakabadhi ghalani, tunarudisha umaskini kwa vijana wetu ambao wanafanya kazi nzuri ya kusaidia jitihada za maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba jambo hilo liwekwe vizuri kwa sababu kumekuwa na mwingiliano mkubwa sana. Kuna watu wanaitwa AMCOS, kwanza hawana maghala lakini wanasema wewe mfanyabiashara nunua sisi tunaomba utuchangie shilingi 50 kwa ajili ya maendeleo ya ushirika wetu. Ni jambo ambalo kwa kweli lisipoangaliwa linaweza likatuletea changamoto kubwa katika utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo naliona, katika mitaala yetu kwenye elimu zetu za juu, tumekuwa na vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu lakini hawana mahali pa kwenda. Jambo hili ni muhimu sana likatazamwa kuanzia shuleni kuanza kuwajengea uwezo wa kujitegemea vijana wetu. Maana yake ni kwamba, vijana wetu wanapomaliza elimu ya vyuo vikuu changamoto kubwa wakitegemea wataenda kuajiriwa na ajira inapokosekana inabaki ni manung’uniko ndani ya mioyo ya vijana wetu hawa na ile elimu inakuwa haina maana kwa kuipata yule kijana, lakini ina maana akianza kujengewa uwezo akiwa darasani na hususan mwaka wa mwisho, akipewa elimu ya ujasiriamali inaweza ikatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine niendelee tu kuipongeza Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea kuifanya, lakini niiombe Serikali, imewekeza kwenye hospitali zetu za wilaya, hususan Wilaya yangu ya Itilima, jimbo jipya. Ningeomba sana sasa kupeleka vifaa tiba, vitendea kazi na wataalam kwenye maeneo hayo, ili kusudi sasa haya yote tunayoyazungumza yaendane sambamba na utekelezaji wa hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala zima la barabara zetu hususan kwenye maeneo ya TARURA. Yako maeneo ambayo ni ya kiuchumi katika vijiji vyetu, lakini barabara hizo hazipitiki, lakini na bajeti ya TARURA tunaipitisha pamoja ni kidogo, lakini maamuzi yale yanachukua muda mrefu sana kufanya utekelezaji wa hayo majukumu.

Mheshimiwa Spika, ningeomba sana kwa haya niliyoyazungumza basi Serikali iyachukue na kuyafanyia kazi. Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)