Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Azza Hilal Hamad

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia afya na uzima na hatimaye nimeweza kusimama ndani ya ukumbi huu kuweza kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na anaendelea kuifanya katika kuwatumikia Watanzania. Niwapongeze pia wasaidizi wake wa karibu; Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, wamekuwa karibu sana na Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba masuala yote ambayo wanakuwa wamekusudia kuyafanya yanafanyika kikamilifu na yanaonekana mbele za Watanzania, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, Manaibu wako na watendaji wote wa TAMISEMI, hakika mmeitendea haki Wizara hii; hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kushukuru kwa yale makubwa ambayo yamefanyika ndani ya Mkoa wa Shinyanga. Ninaanza kwa kushukuru kwa sababu kuna mambo ambayo niliyasema sana ndani ya Bunge hili, lakini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali sikivu inayoongozwa na Jemedari, Dkt. John Pombe Magufuli, wamekwenda kuyafanya kikamilifu na wananchi wa Shinyanga wanayaona, naomba nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali na kumshukuru sana Rais wetu kipenzi, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga unaendelea na uko katika hatua nzuri; ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga umekwishakamilika, hospitali ambayo nimeipigia kelele toka nimeingia mwaka 2010 ndani ya ukumbi huu, sasa hivi imekwishakamilika. Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu umekwishakamilika, ujenzi wa mabweni katika shule zetu za sekondani, nizitaje baadhi ya shule hizo; Shule ya Sekondari Saba Sabini, Ulowa, Kinamapula, Nyashimbi, Bukamba, Busoka Sekondari. Hiyo yote ni kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano ndani ya kipindi cha miaka minne; hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza sana Serikali kwa ujenzi wa vituo vya afya sita katika Mkoa wa Shinyanga. Vituo hivyo vimekamilika na vinafanya kazi na wananchi wetu wanapata huduma kwa ukaribu zaidi, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niingie katika sekta ya elimu, nilikuwa najaribu kusikiliza hotuba ya Kambi ya Upinzani; wanasema miundombinu haitoshi hawajaona chochote, miundombinu haitoshi; lakini niwapitishe tu kwa harakahara. Kwenye suala la miundombinu katika shule za msingi Mheshimiwa Waziri Jafo hapa amesema vyumba vya madarasa 19,808 vimejengwa ndani ya miaka mine; vyumba vya maabara 227 vimejengwa ndani ya miaka mine; vifaa vya maabara shule 1,258 vimesambazwa katika shule zetu; matundu ya vyoo 7,922 yamejengwa katika shule zetu; na ukarabari wa shule kongwe 73 umefanyika kwa kiasi kikubwa kwa kiwango cha juu katika shule zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda tu Mkoa wa Shinyanga vyumba vya madarasa 276 vimejengwa; matundu ya vyoo 155; nyumba za Walimu 23; maabara 10; na mabweni 16. Kwa nini nisiseme hongera Daktari John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo umeifanya ya kuwatumikia Watanzania na kutekeleza ahadi ambazo umekuwa ukizitoa?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwenye…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Azza kuna Taarifa.

MHE. FRANK G, MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa Taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Azza kwamba, kwa mujibu wa taarifa ya tafiti ya Haki Elimu baada ya tangazo la elimu bure ongezeko la watoto kujiandikisha ni 17%, lakini ongezeko la miundombinu katika nchi hii ni 1% peke yake.

Kwa hiyo, ni kweli anazungumza kwamba, yamefanyika na Mheshimiwa Waziri ameonesha kwenye bajeti, lakini ukweli ni kwamba, bado tuna upungufu mkubwa na ndio maana bado hawakuweka mahitaji na upungufu uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri Mbunge ajue kabisa kwamba, bado tuna upungufu mkubwa na tumshauri tu Mheshimiwa Jafo aendelee kuhakikisha kwamba, wanaongeza vyumba kwa kasi na wapange fedha nyingi kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Kuhusu ushauri kwenye hiyo taarifa utatoa wakati wako wa kuchangia, lakini pale ulipoishia kwenye Taarifa, ndio nitakapomuuliza Mhesimiwa Azza kama anaikubali hiyo Taarifa au anaikataa?

MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa yake siipokei na wala siikubali. Namwambia kwamba, maendeleo ni hatua kwa hatua, huwezi ukafanya mambo yako yote ukayakamilisha kwa wakati mmoja. Hata sisi humu ndani leo hii ukipewa pesa begi zima hutamaliza yale yote ambayo umeyakusudia katika nafsi yako. Kwa hiyo, Serikali inafanya awamu kwa awamu, infanya hatua kwa hatua, hongera Daktari John Joseph Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ambayo ameisoma Mheshimiwa Jafo leo nimeangalia na nimesikiliza kwa makini kwa mwaka huu wa fedha Mkoa wetu wa Shinyanga tumetengewa shilingi milioni 840 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa. Taarifa hiyo iko ukurasa wa 339, kwa nini nisiseme maendeleo ni hatua kwa hatua? Hatua moja huanzisha hatua nyingine. Hongereni sana. Ukamilishaji wa maabara. Mkoa wa Shinyanga peke yake tumetengewa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara 44 ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi upande wa afya katika kazi ambazo zimefanyika ndani ya miaka hii minne. Ujenzi na ukarabati wa hospitali za Halmashauri zetu umefanyika kwa Halmashauri 98. Vituo vya afya 433, zahanati 368 ambazo zimejengwa na kufanyiwa ukarabati, lakini kwa Mkoa wa Shinyanga pekee vituo vya afya sita vimejengwa vyenye thamani ya shilingi bilioni 7.4, tunashukuru sana wananchi wa Shinyanga kwa kazi kubwa ambayo imefanywa. Hospitali za Halmashauri katika Mkoa wetu zimejengwa hospitali tatu ambazo ni Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Hospitali ya Wilaya ya Ushetu na Hospitali ya Halmashauri ya Msalala ambayo bado haijakamilika na mwaka huu nimeona imetengewa tena bilioni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa afya ukamilishaji wa zahanati nimeona Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa katika bajeti ya mwaka huu kila Halmashauri itapata zahnati tatu. Kwa Mkoa wa Shinyanga peke yake tuna bilioni 3.9 kwa ajili ya zahanati, sina sababu ya kukaa hapa kuanza kutaja kwamba, naomba zahanati fulani, naomba zahanati fulani, naamini hizi bilioni 3.9 zitakwenda kukamilisha zile zahanati zetu ambazo zimeanzishwa na wananchi na wananchi sasa kwenda kupata huduma ambayo inastahili, tunawashukuru sana; lakini pia nitumie fursa hii kuishukuru Serikali kwa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala tumetengewa bilioni moja kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali ya Halmashauri ya Msalala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika bajeti ya mwaka huu katika ujenzi wa nyumba za watumishi na majengo ya utawala. Nitumie fursa hii tena kusema kwa Mkoa wa Shinyanga tuna bilioni 2.5 ambazo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala na majengo haya yanakwenda kujengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu. Naishukuru Serikali kwa kuona kwamba, watumishi wetu wanatakiwa sasa kuwa na sehemu nzuri ya kufanyia kazi ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Shinyanga na Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwani kwa muda wote wameniamini na kuweza kufanya nao kazi ndani ya miaka minne.

Nawashukuru sana kwa ushirikiano mkubwa ambao wamenipa, lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambayo ndio Halmashauri Mama ninayoishi kwa kuweza kunilea na kunifikisha hapa nilipofika. Niko pamoja na ninyi na nitaendelea kuwa pamoja na ninyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona unanitazama kengele imegonga, naunga mkono hoja. (Makofi)