Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa kibali sisi Wabunge wote na viongozi wote wa Bunge pamoja na Watumishi wa Bunge kuweza kufikisha Bunge hili la Kumi na Tisa, Mkutano huu wa mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa viongozi wote wa Bunge, viongozi wa Serikali, viongozi wa taasisi mbalimbali, viongozi wa vyama vya siasa, wanachama wote nchi nzima pamoja na wananchi wote walioungana nasi kipindi cha msiba wa Katibu wetu Mkuu aliyetutoka tarehe 30 Aprili, 2020 Mheshimiwa Khalifa Suleiman Khalifa. Mungu awabariki sana kwa moyo wa upendo na Mungu aendelee kumweka mahali pema Peponi kiongozi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye Wilaya ya Kaliuwa. Hospitali yetu ya Wilaya ambayo kwa asilimia 80 imejengwa kwa fedha za wananchi wa Kaliuwa, kwa maana ya mapato ya ndani kwa asilimia 80, mwaka 2019 tulipata usajili wa muda kwa maelekezo kwamba tukamilishe baadhi ya majengo muhimu kama theater majengo ya wazazi ili tupate usajili wa kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 tulitengewa shilingi bilioni 1.5. Ninashukuru kwamba tumepata shilingi milioni 500 tu, mpaka sasa hivi shilingi bilioni moja hatujapata. Kwa kweli ninaiomba Serikali, kwa jicho la pekee waweze kukamilisha ile shilingi bilioni moja iliyobaki kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha ili hospitali ile ya Kaliuwa iweze kukamilika na kupata usajili wa kudumu, wananchi waache kuhangaika kwenda Hospitali za Kigoma, Urambo, Tabora na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba suala la watumishi wa afya kwa Wilaya ya Kaliuwa, tatizo sugu kubwa sana; mwaka 2018 nililia hapa Bungeni, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi akaniambia nilete maombi rasmi kwa Sekta ya Afya nikaleta maombi rasmi tuliokuwa na tatizo, lakini tulipewa watumishi sita tu tangu mwaka 2018 na bado wengine wanahama. Kwa hiyo, bado kilio chetu kiko pale pale. Tunaomba Kaliuwa tuangaliwe kwa jicho la pekee kwa suala la watumishi wa Sekta ya Afya. Tumejenga Zahanati na Vituo vya Afya; Zahanati ina watumishi wawili na Kituo cha Afya kina watumishi watatu. Ni tatizo! Kwa hiyo, naomba suala la watumishi lipewe kipaumbele cha kutosha katika Wilaya ya Kaliuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Walimu wa Sayansi kwa Wilaya ya Kaliuwa ni tatizo. Tumehamasisha watoto wetu, wameanza kupenda kusoma sayansi, lakini pia tunaenda kwenye uchumi wa viwanda. Hatuwezi kwenda kwenye uchumi wa viwanda hatuna Walimu wa Sayansi. Walimu hawa ni wachache; shule inakuwa na Walimu wa Sayansi wawili, anachukuliwa mmoja anahamishiwa shule nyingine. Kwa hiyo, shule nzima inakuwa na Mwalimu wa Sayansi mmoja, ni tatizo. Tunaomba Serikali iangalie namna gani ya kuondoa changamoto kubwa ya Walimu wa Sayansi katika Wilaya yetu ya Kaliuwa na ninadhani pia ni suala la nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alitoa waraka kwa Halmashauri zote kuhakikisha kwamba walimu na watumishi wanapandishwa madaraja. Bado kupandisha watumishi madaraja ni tatizo. Wilaya ya Kaliuwa inaweza kuwa na tatizo kubwa zaidi, kwa sababu kuna walimu wamekaa tangu mwaka 2013 mpaka leo hajawahi kupanda daraja hata moja. Mwalimu huyu tunampa moyo gani wa kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2018 kuna waliopewa barua za kupandishwa vyeo. Wameenda kusoma, tena wamejisomesha au wamesomeshwa na Serikali, lakini wamerudi hawajapandishwa cheo chochote; siyo mishahara wala siyo cheo. Bahati mbaya mwaka 2018 wamepewa barua mwaka 2019 wamenyang’anywa zile barua za kupandishwa vyeo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mwalimu kama huyu, mpaka wengine wameamua kuacha kazi kwa sababu hatuwatendei haki. Kwa nini Mtumishi wa Serikali apandishwe cheo kwa barua, halafu uje mnyang’anye ile barua ya kumpandisha cheo, ni Wilaya ya Kaliuwa tu au na wilaya nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ifuatilie, ni kwa nini Wilaya ya Kaliuwa walimu hawapandishwi vyeo, hawapandishwi madaraja na kwa nini wale wengine walipewa barua za kupandishwa madaraja halafu wakaja wakanyang’anywa leo wana miaka mitano, wana miaka sita, wana miaka nane hawajapanda madaraja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la shule za Kata. Tunatambua shule za kata kiukweli zimesaida Taifa hili sana, kila mmoja ata-acknowledge hicho kitu. Watoto wetu hata wa maeneo ya vijijini wamepata elimu kwa mazingira hayo hayo, lakini angalau wamepata elimu. Tukumbuke waliosaidia shule hizi za kata 2007 ni walimu waliolelewa kwa mpango wa crash program; Walimu ambao walitolewa, wakaambiwa njooni mkafundishe watoto hawa. Wengine walikuwa na fani nyingine mbalimbali, wakaambiwa yeyote mwenye kutaka kuja kufundisha, aje akafundishwe kwenye crash program, wakafundishwa, wakaja kufundisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, 2007 wamefanya kazi miaka 10, mwaka 2017 wakaondolewa kama wezi, bila chochote. Kwa kweli Serikali hatukutenda haki. Hata kama kulikuwa na makosa, waliambiwa wajiendeleze, wengine walikuwa vyuoni wanasoma, wengine washajiendeleza, wengine walikuwa hawajachukua hatua yoyote; walioko mashuleni wametoka, wameshaondolewa kazini; waliokuwa wanajiendeleza wamefika degree, wengine wamefika mwaka wa pili ameondolewa kazini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Serikali iangalie namna ya kuona juhudi walizofanya kuendeleza Shule za Kata kwa 10 years wanaondolewa kama vile wameiba, hawakutendewa haki. Wana familia, wamehudumu katika Taifa hili kwa moyo wao wote, wengine walitaka kuwa wafanyabiashara, wakaamua kuwa walimu. Tuwaangalie kwa namna ya pekee. Ninaiomba Serikali iangalie namna gani kuwatia moyo angalau wamalizie masomo yao waone jinsi ya kuweza kuwarudisha kazini waendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni la TARURA. Napongeza kazi nzuri ya TARURA wanayoifanya, lakini barabara zetu zimebomoka sana, sana na fedha wanayopewa TARURA haitoshi. Kwa hiyo, bado tatizo ni kubwa. Wilaya ya Kaliuwa peke yake tuna mzunguko wa ndani barabara za udongo, barabara za TARURA 1,370.5, tunapata kwa mwaka mzima shilingi milioni 600.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 tulipata shilingi milioni 675, mwaka huu tumepata shilingi milioni 625, inazidi kupungua, lakini mvua ni nyingi na barabara zimekatika. Kwa hiyo, bado wananchi wanashindwa kupitisha mazao yao kwenye barabara mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaomba mara nyingi Bungeni namna gani TARURA iongezewe fedha, kiukweli wanafanya kazi bila kupewa fedha. Shida ni kwamba fedha hawapewi, ni kidogo sana na mzunguko wa barabara ni mkubwa. Kwa hiyo, wanashindwa kutekeleza wajibu sawa sawa na ile kazi ambayo wamepewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala lingine. Mheshimiwa Rais alitoa ahadi Wilaya ya Kaliuwa ya kilometa saba za lami katikati ya mji. Natambua ahadi za Mheshimiwa Rais zinatekelezwa na TAMISEMI. Kaliuwa huu ni mwaka wa tano, Mheshimiwa Rais anaenda kumaliza muda wake, hata robo kilometa hatujawahi kupata. Ninaiomba Serikali iangalie, kilometa saba, hata moja kweli! Hivi Rais anavyokuja wakati mwingine kuja kuomba ridhaa ya wananchi wale, atawaambia hata kilometa moja ameshindwa kuwapa kweli jamani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iangalie ahadi za Mheshimiwa Rais ambazo wengine wamepata angalau kilometa mbili, kilometa moja; Kaliuwa na wananchi wake nao wana haki ya kupatiwa japo kilometa chache ili angalau anapokuja Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuomba kura kwa wakati mwingine awe na cha kusema kwa wale wananchi ambao aliahidi hadharani na nina imani kabisa kwamba watakuwa wanamhoji maswali mengi kuhusiana na suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa muda nilioupata Naendelea kuwashukuru wananchi wa Kaliuwa kwa kunitia moyo na kuendelea kuniamini na kuwatumikia. Nami nina imani kwa kipindi hiki tukimaliza na Serikali isaidie kutekeleza ahadi ambazo ilikuwa imeahidi ili angalau tunapokwenda kwenye kampeni tuwe na ya kusema. Ahsante sana. (Makofi)