Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Juma Othman Hija

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri mkuu.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na watendaji wake wote kwa kuweza kutayarisha na hatimaye kuiwasilisha kwa makini na kwa ufasaha mkubwa hotuba hii iliyojaa matumaini makubwa kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika kuchangia hotuba hii napenda kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza ni kuhusu huduma za jamii; napenda kuchukua fursa hii kuipongeza kwa dhati Serikali yetu ya awamu tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Joseph Magufuli kwa kusimamia vizuri pamoja na mambo mengine kuwa na uendelezaji wa huduma za jamii nchini. Kitendo cha kuweka elimu bila ya ada ni kitendo chema na kinapaswa kupongezwa na jamii yote ya Tanzania. Elimu ndio ufunguo wa maisha, mtu kukosa elimu sio jambo sahihi. Tunaipongeza Serikali yetu kwa jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu katika jambo hili ni kwamba Serikali ifuatilie na ielimishe wananchi hasa wa kijijini juu ya kuweka fursa hii. Inawezekana fursa hii ikatumika kwa watu wanaoishi mijini tu na kukosekana kuwafaidisha wananchi wa vijijini kutokana na kutokuwa na fursa hii.

Pili ni TASAF, miongoni mwa mipango bora ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kupunguza umaskini ambazo Serikali yetu imeendelea kufanya ni kupitia mpango huu wa TASAF. Mpango huu ni miongoni mwa mikakati inayopaswa kuendelezwa kwa nguvu zote. Mpango huu umesaidia sana wananchi hasa wale wa kaya maskini, umewainua kiuchumi, kufikra na umewaendeleza katika juhudi zao za kujitafutia kipato.

Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuipongeza Serikali yetu inayoongozwa kwa umakini kwa hali ya juu na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa. Ushauri wangu katika jambo hili kwa watendaji kama alivyoagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu kuwa waaminifu katika kutekeleza jambo hili. Bado kuna manung’uniko katika upembuzi usiokuwa sahihi wa kaya husika. Bado kuna kaya ambazo hazina sifa ya kupata fursa hii na zinaachwa zile ambazo zinastaahiki kupata fursa hii.

Mheshimiwa Spika, tatu ni kilimo; kilimo ni uti wa maisha na maendeleo ya nchi. Serikali yetu inaendelea na juhudi za kusimamia kwa ukamilifu kilimo ili kuona tumefikia katika malengo tuliyojiwekea. Miongoni mwa mambo ambayo Serikali inayasimamia ni pembejeo na zana za kilimo. Bila ya pembejeo na zana za kilimo hakuna uwezekano wa kupata mafanikio ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, nashauri sana Serikali kwa kuiwezesha, kuisimamia na kujielekeza Benki ya Kilimo ya TADB kuhusu kuwakopesha wakulima wetu wa chini, lakini bado gharama za matrekta ni kubwa sana. Kikundi cha wakulima ambao nimejipanga kuendeleza kilimo kuwapa mkopo wa shilingi milioni 78, ni kitendo ambacho kinatakiwa kuangaliwa, si rahisi kuweza kumudu kurejesha mkopo wa aina hii kwa wakati. Ushauri wangu katika hili TADB iendelee kutafuta namna nzuri zaidi ya kuweza kuwapunguzia wakulima bei ya trekta ili waweze kumudu kwa wingi kukopa matrekta hayo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.