Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi kwenye bajeti hii ya mwisho kwa kipindi hiki cha Bunge la Kumi na Moja la Awamu hii ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli. Pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake katika kuongoza Taifa letu kwa kushirikiana na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba nzuri ya bajeti ya 2020/2021 ambayo imegusa kila eneo na kuelekea mafanikio yalipatika nchi.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa juhudi ambazo inazifanya katika kutoa elimu na kupambana na virusi vya Corona ambavyo ni tishio kwa nchi yetu na dunia kwa ujumla. Pamoja na juhudi hizo je, ni kwa kiwango gani nchi yetu tumeweka mpango wa elimu, vifaa tiba kwa maeneo ya pembezoni na maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi?

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na mafuriko maeneo mbalimbali ambapo kumepelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara, nyumbani na maeneo mbalimbali ya majengo ya huduma kwa jamii, mifugo pamoja na mazao na mashamba. Kwa kuwa jambo hili la mafuriko limekuja kidharura na mvua bado zinaendelea kunyesha, je, Serikali imejipangaje kurudisha hali ya miundombinu ya barabara kwa haraka ili kuleta urahisi wa mawasiliano kwa jamii?

Mheshimiwa Spika, miradi mingi imekumbwa na kadhia hiyo hivyo kuna uwezekano wa miradi mingi kuchelewa kukamilika kwa wakati mfano mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere ambao uko Rufiji ambako barabara imeharibika na safari ya kupeleka vifaa kuchelewa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa fedha kwa TANROADS na TARURA ili kuboresha miundombinu ya barabara?

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Waziri Mkuu katika suala la mafuriko alilisimamia vyema kwa kufika maeneo mbalimbali yaliyopata kadhia hiyo na kuwafariji na kutoa misaada. Pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera kwa usimamizi wa Ilani na utekelzaji wake kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako kwa “mmeahidi na mmetekeleza.” Miradi mbalimbali iliyoanzishwa imeweza kuongeza kipato cha uendeshaji maisha kwani tumetoa ajira hasa kwa vijana na kuweza kukuza uchumi wetu. Pia kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana ambayo yanawasaidia kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, kuna kundi la vijana ambao waliathirika kwa kutumia madawa ya kulevya na Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuhakikisha wanaacha na wengi wanaingia kwenye mfumo wa kutumia dawa ambazo zimewawezesha kurudi kwenye hali yao ya kawaida. Ni vyema Serikali ikawawekea utaratibu wa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali. Mfano mzuri wa vijana kama hao ni Kituo cha Kutolea Dawa kilichopo Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nalipongeza Bunge Mtandao limeanza kwa wakati muafaka kwani kutokana na tatizo hili la Corona sijui Bunge letu lingeendeshwaje. Pongezi kwako na Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuwasilisha.