Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama hapa dakika za mwisho mwisho, dakika za majeruhi.

Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani za dhati na pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri wa Afya, kwa jinsi wanavyochukua juhudi katika kushughulikia janga hili la dunia maana hili siyo janga la Taifa ni janga la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka niseme kitu kimoja. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Waziri Mkuu wa Tanzania na juhudi anazozichukua ni kwa ajili ya Taifa zima la Tanzania. La kusikitisha na jambo ambalo limenifanya leo nimuombe Mheshimiwa Spika kwa bidii zote angalau kunipa hizi dakika tano ili nikupe ujumbe huu ni kwamba kuna mchezo na mzaha mkubwa juu ya maisha ya watu Zanzibar kuhusu ugonjwa huu wa Corona. Upo mchezo, mzaha na dharau.

Mheshimiwa Spika, kuna Waziri mmoja alikuwa safari nje ya nchi aliporudi Zanzibar akiwa katika hali ya kuumwa alikataa kukaa kwenye karantini. Waziri huyu Salama Aboud Talib alienda kukaa nyumbani kwake ugonjwa ulipomzidia alirudi hospitali ya umma ya Mnazi Mmoja. Taarifa na uamuzi wa Serikali ni kwamba wagonjwa wote wanaohisiwa kuwa na ugonjwa wakae karantini, alikataa, ndani ya muda wa siku tatu ameng’ang’ana kukaa Hospitali ya Mnazi Mmoja. Baada ya kuonekana hili jambo limekuwa kubwa na minong’ono na malalamiko kuwa mengi ndiyo alikubali kuwekwa karantini kwa nguvu. Athari yake tayari nyumbani kwake wapo wawili aliowaambukiza na pale hospitali haijulikani ni nini kilichoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, alifanya hivi kwa sababu ya kiburi cha madaraka yake. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Makamu wa Rais wa Zanzibar alipotoka safari alikwenda kukaa kwenye karantini yeye mwenyewe bila kulazimishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu ndiyo utu na uongozi. Leo Waziri huyu aliyekiuka amri ya Serikali, amri yako wewe Waziri Mkuu na hata amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nani yeye na kiburi hiki kakitoa wapi?

Mheshimiwa Spika, jana tumeona kwenye taarifa za habari za Kenya, Naibu Gavana ametoka pale hospitali na pingu anaenda kusulubiwa. Kwa sasa hatuwezi kumchekea mtu kwa sababu ni Waziri au ni nani, lazima Mheshimiwa Waziri Mkuu hili alichukulie hatua haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, isitoshe baada ya kiburi hiki, kuna mpumbavu mwingine anaitwa Hafidh, ni daktari, hadi ninavyoongea ameng’ang’ana hospitali hali ya kuwa ameathiriwa na ugonjwa huu wa Corona. Yuko pale Hospitali ya Mnazi Mmoja. Kwa nini anafanya hivi? Ni kwa sababu ana nasaba au ukoo wa wakubwa. Hii ni hatari inayofanyika Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siwezi kusema wakubwa wa Zanzibar wanawaogopa watu hawa lakini nachosema ni mchezo unaofanywa kwa kuhofia watu na madaraka yao. Leo Uheshimiwa wake ni kwa sababu ana uhai wa Mwenyezi Mungu, anapumua, dakika moja akifumba jicho anageuka anakuwa marehemu, sasa na awe marehemu yeye asiue wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taharuki iliyopo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya matukio hayo ni kubwa. Hivi ninavyoongea nataka Mheshimiwa Waziri Mkuu afuatilie huyu Daktari anayeitwa Hafidh kama bado yupo pale Mnazi Mmoja au amekubali kwenda karantini? Kwa sababu kauli anazotoa kwenye mitandao ya Facebook anasema hakuna yeyote anayeweza kumfanya lolote, anazitoa yeye mwenyewe. Pia matusi anayotukana, hayawezi kusemeka kwenye hadhara ya watu wastaarabu.

Mheshimiwa Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba mambo haya yanafanyika Zanzibar. Sasa tufanye nini? Kuna msemo wa Kiswahili unasema: “Zumari ikipigwa Chopocho Pemba anacheza wa Mtwara”. Haya maradhi yakianza popote ndani ya nchi ujue ni athari kwa Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anaogopewa vipi mtu huyu? Hivi vitu vinasikitisha sana. Tukiangalia juhudi za Serikali, Taifa na dunia imekaa katika tension lakini kuna watu kwa sababu tu eti naitwa Waziri anaamua kuhatarisha maisha ya watu. Huyu mtu wa namna hii anatakiwa akiua mtu na yeye auliwe. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. (Makofi)

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)