Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameleta mafuriko ameleta Ugonjwa wa Corona; Mwenyezi Mungu ambaye amewapenda Watanzania kwa kuuchelewesha Ugonjwa wa Corona kuja Tanzania kwanza na ugonjwa huo kuanzia China. Huu ni mpango maalum wa Mwenyezi Mungu.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naona mlimshangaa Mheshimiwa Bungara, hajakosea, imeandikwa tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila jambo. Endelea Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, hivi walikuwa na matatizo hapo? Kheri shari minallahi taalah. Kwa hiyo, tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kama lingekuwa jambo hili limeanzia Kariakoo na hali hii tuliyokuwa nayo sisi hii, aah saa hizi Tanzania ilishateketea! Kwa kuwa imeanzia China ili sisi huku tujipange. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika watu ambao wamenufaika katika Awamu ya Tano, ah, basi Jimbo langu mimi Alhamdulillah. Katika Vituo vya Afya, nina vituo vya afya vitatu, aah, vizuri vyote! Nanjilinji mambo safi, Pande mambo safi, Masoko mambo safi. Barabara ya kwa Mkocho imekwisha, barabara za lami pale Masoko zimejengwa; aah, mambo Alhamdulillah! Mahakama nzuri kabisa, Chuo cha Maedeleo, aah, utasema watoto wako Chuo Kikuu cha nanii, kizuri kabisa! Hakika katika sifa ambazo Chama cha Mapinduzi kinasifiwa, basi Kilwa Alhamdulillah, hasa Kilwa Kusini! Mambo mazuri kabisa. Ninaamini kabisa kwa juhudi za Serikali ikisimamiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haya mambo ndiyo yametimia.

Mheshimiwa Spika, maana yake kuna wengine wanasema sijui Serikali Chama cha Mapinduzi; hapana, kazi ya Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali. Kwa hiyo, haya yote yanayofanyika ni kwa sababu Bunge lako liko strong. Wala siyo CCM, CCM ilikuwa zamani tu, haya hata hayakufanyika. Hayakufanyika haya! Hii inatudhihirishia sasa, kumbe CCM hii ikitesa kwa makusudi, lakini miaka minne tu mambo mazuri eti. Miaka 50 ya CCM imeshindwa. Ingelikuwa speed hii mnayoifanya ya miaka hii minne kama mngelianza miaka 50, sasa hivi tusingeongea habari hizi. Yangekuwa mengine kabisa, lakini mmetuchelewesha. CCM imetuchelewesha! (Kicheko/Makofi)

MBUNGE FULANI: Sana tu!

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kama mngelifanya haya, kwa speed hii kwa mpangilio huu, aah, sasa hivi Tanzania kama Ulaya.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Kwa hiyo, mimi nashukuru sana.

SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Muda wangu, muda wangu jamani.

SPIKA: Aah, tunauchunga. Maana ulianza vizuri, halafu unataka kuharibu tena! (Kicheko)

Mheshimiwa Waziri tafadhali. (Kicheko)

T A A R I F A

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Bungara ambaye anaendelea kuongea sasa hivi kwamba Chama cha Mapinduzi wananchi walikikubali kikamchagua Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ndio Rais wa Tanzania, hakuna Rais mwingine. Rais alichaguliwa na wananchi wote mpaka hao wa Kilwa. Ndiyo maana Rais wetu hana upendeleo na katika kauli zake thabiti amesema maendeleo hayana chama, ndiyo maana katika uongozi wake ametekeleza maendeleo maeneo yote, ilimradi ni Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niliona nimpe ndugu yangu, Mheshimiwa Bungara, hayo ili aweze kujua anachokiongea, ni kwamba imetekelezwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Rais wa Watanzania wote.

SPIKA: Anachosema Mheshimiwa Bungara ni kwamba Serikali hii imetekeleza miradi yote hii bila upendeleo pamoja na kwamba wapinzani mlipiga kura mfululizo kwa miaka yote ya hapana kwa bajeti hiyo. Ndicho anachosema tu.

Endelea Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, mimi naona hatugombani sana kwa sababu kasema; nami nilisema zamani kwamba hii Serikali siyo ya CCM, ni ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Kwa hiyo ananiunga mkono tu. Kwa hiyo, wala sina matatizo na hilo. Mimi nilichosema, Serikali ya CCM miaka 50 imeshindwa, lakini ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli si ndiyo imefanya! Sasa tunapishana wapi? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitunzie muda wangu.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mazuri haya na safari hii mimi nitapiga kura ya neutral, inaitwaje ile?

MBUNGE FULANI: Abstain,

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Abstain; sisemi hapana wala ndiyo, kwa sababu kuna mazuri halafu kuna mabaya. Kwa hiyo, nitakaa kati kwa kati.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na maendeleo haya yaliyokuwepo lakini sisi Waheshimiwa tunaishi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunaapa hapa kuwa tutailinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunachukua misaafu na nini, tunalinda, tunaapa! Ukiapa hapa ina maana kuilinda Katiba ni pamoja na kukaa katika Ubunge miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuna watu wameapa hapa, nitailinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; katikati ya miaka mitatu wameshuka, wametoka Bungeni amekwenda CCM.tatizo lililokuwepo, walipokwenda kule wakaahidiwa watapata Ubunge. Kwa hiyo, wakaacha Ubunge. Waliapa kwamba sisi tutakuwa katika Bunge miaka mitano, halafu wakatoka wakaingia CCM, halafu kufika CCM kule, wakaomba Ubunge. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kitendo kile cha kuomba Ubunge; na kwa kuwa waliahidiwa kwamba watapata Ubunge, wakasimamia, ndipo tunaposema Tume sio huru sasa. Tume sio huru hapo. Wakahakikisha lazima Mheshimiwa Maulid Mtulia awe Mbunge tena. Kwa kuwa wapinzani tulikuwa tuna nguvu, wakafanya figisufigisu kwa sababu wamevunja Katiba ya Jamhuri, akapigwa mtu risasi; alivyopigwa mtu risasi ni kwa sababu ya huyu Mtulia aliyevunja Katiba…

SPIKA: Samahani kidogo Mheshimiwa Bungara. Nilikuwa nawatafuta baadhi ya watu humu ndani; hivi Mheshimiwa Lusinde yupo! Ndio mchangiaji atakayefuata baada ya hako wewe. Nilitaka kumpa taarifa tu.

Endelea Mheshimiwa Bungara. (Kicheko)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anapokuja leo Mheshimiwa Mtulia akasema Chama cha CHADEMA kifutwe kwa sababu ya kuua, lakini sababu ilikuwa Mtulia. Aliacha Ubunge ndani humu Mheshimiwa Mtulia wa Kinondoni huyu. Tunaposema tume siyo sawasawa, huyu Mtulia akapita bila kupingwa kwa tume kusema kwamba watu wa CHADEMA na CUF hawakupeleka fomu, akapita bila kupingwa.

Mheshimiwa Spika, tunaposema tume siyo huru wala halali, kwetu Kilwa sisi Madiwani wetu wamerudisha fomu kabisa, Mkurugenzi akasema fomu hazikurudishwa, wamepita bila kupingwa. Tunaposema tume siyo halali, siyo kwa sababu tu tume siyo huru; pale Maalim Seif anaposhinda na anaposema kwamba mimi naongoza ukafutwa uchaguzi. Tunaposema tume siyo halali ni hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, tume huru ipo lakini watu sio huru. Sijui mnanielewa! Tume huru katika Katiba ipo, imeandikwa tume huru, lakini watu sio huru na wasimamizi sio huru. (Makofi)

SPIKA: Samahani kidogo. Tume hiyo hiyo inapomtangaza Selemani Bungara zaidi ya mara moja kwamba ameshinda uchaguzi, ni huru siyo huru?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, inakuwa hivi, lazima utoe kongoro kwenye mchuzi. Inaitwa kongoro mumchuzi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunavyoongea hapa tumesema mengi katika Bunge hili kuiambia Serikali, lakini miaka mitano imepita sasa hivi hali si nzuri. Nilisema hapa kuna watu wamepigwa risasi katika msikiti, Mheshimiwa Ismail Bweta kapigwa risasi msikitini; tumesema kwa Waziri Mkuu, kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, hamna chochote kinachofanyika, hali mbaya.

Mheshimiwa Spika, juzi wamekamatwa watu, wamechukuliwa watu na watu wasiojulikana, watu sita njia nne hapo; mtu wa kwanza Juma Selemani Farahan, Omary Kassim Mkwachu, Rashid Abdallah Mwinyigoha, Nurdin Ally Mnyiwiwa, Selemani Sefu, Yussuf Ramadhan, tarehe 15 Januari, wamechukuliwa hatujui wapi walipopelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaposema kwamba, Serikali ya CCM hamuwezi kushinda Masheikh wetu mpaka sasa hivi wako gerezani miaka sita, hamuwezi kushinda! Tunaposema Serikali ya CCM haiwezi kushinda sio kwa sababu ya kujenga barabara, barabara hata Afrika Kusini zipo, Marekani huko zipo na watu wanatolewa vilevile, barabara nini? Sisi Kilwa Kivinje barabara tulikuwanayo tukaikataa CCM, barabara sisi hatuchagui barabara tunataka utawala bora, utawala wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo watu wanatekwa wanapotea, wanapigwa risasi, Serikali ya CCM imekaa kimya tu. Katiba inasema kabisa kila mtu ana haki ya kuishi, nataka Serikali ya CCM Masheikh watoke Mahakamani; hatuna matatizo kukamatwa kwa watu, tuna matatizo mkiwakamata! Muwapeleke Mahakamani. Watu wetu wamekamatwa hawa sita Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 15 wamekamatwa watu sita hatujui waliko na wamechukuliwa na watu, nini jamani? Halafu ninyi mchukue nchi ninyi? Mchukue nchi kwa kitu gani? Kwa barabara? Kwani Afrika Kusini barabara zilikuwa hakuna? Umeme ulikuwa hakuna? Walienda watu wakaenda wakamtoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana Waziri Mkuu tunakuomba sana. Tena Waziri Mkuu hata Kilwa hujaja kila siku unatuongopa tu nakuja leo, nakuja leo; njoo Kilwa tuje kukuambia mambo…

SPIKA: Mheshimiwa Bungara nchi hii kubwa anazunguka kila mahali atakuja tu.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, na Kilwa si katika nchi? Au Kilwa sio nchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sana vijana hawa sita hawa wamechukuliwa eti Serikali ya CCM miaka mitano mnashindwa watu kuwajua watu wasiojulikana, mnashindwa kuwajua ninyi? Kweli mnashindwa kuwajua ninyi? Intelijensia ninyi, mkutano wa Bwege mnauzuwia, intelijensia, watu wanachukuliwa vijana wetu…

MBUNGE FULANI: Wamechukuliwa na nani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA:…Hamuwawezi, hamuwezi kuwakamata?

MBUNGE FULANI: Wamechukuliwa na nani?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA:…kuna nini Mheshimiwa, sikiliza, kuna kitu gani? Kuna siri gani?

Mheshimiwa Spika, tuliambiwa na Mkurugenzi wa Upelelezi hapa wa Usalama wa Taifa hakuna jambo linalofanyika Tanzania Usalama wa Taifa hawalijui, hapa kuna nini hapa? (Makofi)

SPIKA: Labda kulisaidia Bunge japo muda wako umeisha, wamechukuliwa na nani hawa watu?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, na watu wasiojulikana.

SPIKA: Hawa vijana sita?

MHE. SELAMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, watu wasiojulikana, lakini CCM mnawajua, mnawajua. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Bungara muda wako umeisha. Ahsante sana Mheshimiwa Selemani Bungara. (Makofi)