Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza niweke kumbukumbu sawa kuhusu hili ambalo limezungumzwa na ndugu yangu Mheshimiwa Vedasto kwamba vita vya Majimaji vilianzia Rufiji katika Kata ya Mbwala, Kata ambayo inapakana na Vijiji vya Kilwa na eneo hili la Nandete ambalo amelisema ni Vijiji vilivyopo Rufiji, Nandete pamoja na Tawi. Lakini pia ikumbukwe hata huyo mpiganaji Kinjekitile Ngwale alinyongwa katika mti uliopo pale Muholo ambao umeng’oka hivi karibuni tu, kwa hiyo, vita hii ilianzia Rufiji haikuanzia Kilwa naomba niweke kumbukumbu sawa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, kuna mwangwi inanipa tabu kujua taarifa hii inatoka wapi!

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Kuchauka.

SPIKA: Aaaah! Mheshimwa Kuchauka Mbunge wa Liwale.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumzia vita ya Majimaji. Muasisi wa vita ya Majimaji ni Kinjekitile Ngwale, Mngindo, na wakati ile vita inaanza Kinjekitile Ngwale alikuwa Iringa anaendelea kukusanya majeshi huku nyuma wanakijiji wa Kijiji cha Nandete walikwenda badala ya kupalilia mashamba ya pamba walifyeka pamba zote ndipo Wajerumani wakaja na nguvu wakaanzisha ile vita wakati Kinjekitile Ngwale bado yupo Iringa. Kwa hiyo, nimpe taarifa kwamba ile vita ya Majimaji ilianza Kilwa na chanzo chake ni wakulima walipokwenda kufyeka pamba badala ya kupalilia. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimwa Spika, taarifa hii siipokei kwa sababu vita ya Majimaji ilishaanza mapema na Kinjekitile alitafutwa kwa kuwa alikuwa mganga tu wa kienyeji, lakini yeye hakuwa muasisi wa vita hii.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa, endelea Mheshimiwa Muhagama. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa babu yangu Mheshimiwa Mchengerwa kwamba Kinjekitile Ngwale alikuwa mganga wa kienyeji aliyewadanganya wapiganaji wa vita kwamba maji yanaweza kupunguza makali ya risasi na ndiye aliyesababisha tushindwe ile vita ahsante. (Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa. (Kicheko)

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, taarifa hii naipokea imekaa vizuri. Pamoja na hotuba nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu iliyosheheni matumaini na ujenzi wa Tanzania mpya, nina imani kubwa sana kwamba vipaumbele vya Taifa letu sasa vimeimarisha hali ya ujenzi si wa Taifa peke yake bali ya ujenzi wa wazalendo wapya. Vipaumbele hivi ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu amevitoa visingefanikiwa kama Taifa hili lisingelikuwa na Jemedari Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ambaye yeye kwa uchapa kazi wake, uhodari wake amechangia kwa kiasi kikubwa sana Taifa letu sasa pengine kesho, keshokutwa linaweza likawa ni Taifa ambalo linajitegemea lenyewe.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imejikita katika mambo mengi hususani katika kilimo, afya, miundombinu, maji, umeme, mafuriko pamoja na eneo hili la Corona na mambo mengine mengi. Tuwaombe tu Watanzania kuhusu eneo hili la Corona kwamba ni vyema Watanzania wakafuata ushauri unaotolewa na Wizara ya Afya, lakini pia ushauri unaotolewa na Kamati zilizoundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati za Maafa za Mikoa pamoja na zile za Wilaya. Kwa hiyo Watanzania waaache viburi, Watanzania waache ujuaji namna pekee ya kuwaokoa Watanzania ni kufuata maelekezo yanayotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, hakuna namna nyingine.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba imekuwa nzuri sana kama ambavyo nimesema Mheshimiwa Waziri Mkuu amegusia eneo hili la mafuriko. Ikumbukwe tu kwamba Rufiji hakuna mvua hata moja inayonyesha, mvua zinanyesha Nyanda za Juu Kusini, pia ikumbukwe tu kwamba eneo kubwa la Rufiji liko kwenye bonde, kwa hiyo maji yote ya mvua na maji ya kwenye mabwawa mbalimbali hapa nchini yanakuja Rufiji na hii imepelekea robo tatu ya Rufiji yote sasa iko kwenye maji. Mafuriko haya hayakuanza juzi japokuwa nitambue mchango mkubwa wa Ofisi hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini lazima tukiri kwamba wataalam wetu walichelewa kutufikia Rufiji na hiki kwa kweli ni kilio cha wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji.

Mheshimiwa Spika, tatizo ambalo naliona si lingine isipokuwa sababu kubwa ni Fungu 37 hatukutenga fedha kwenye hichi Kitengo cha Maafa hakuna fedha na badala yake tunategemea zile Ofisi za Maafa za Mikoa na Wilaya. Niiombe pengine Bunge kwa kuwa sasa eneo hili Mbunge wa Jimbo ndio anawajibika kuwahudumia wananchi na ikumbukwe nchi hii ni ya wananchi na mfariji namba moja kwa wananchi ni Serikali, hii ni kwa mujibu wa Ibara ya Nane ya Katiba ambayo inasema nchi ni ya wananchi. Basi, tuwaombe Wizara kuangalia uwezekano sasa wa kutenga fungu kwenye hili Fungu la maafa ili wataalaam wetu pale ambapo wanasikia taarifa za maafa iwe rahisi wato kutufikia.

Mheshimiwa Spika, japokuwa zaidi ya familia 20,000 zimekosa makazi, zimekosa vyakula, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ilituletea baadhi ya vitu ambavyo kwa kweli ni vichache hususan kwenye eneo hili ambalo lilikuwa eneo la maafa. Walituletea ndoo ambazo zilikuwa tupu nadhani unaweza kuona wananchi wa Rufiji wanachohitaji ni faraja hawahitaji ile huruma ambayo pengine wanapaswa wasifanye kazi hapana wanachohitaji ni faraja kidogo ambayo pengine Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inasema tunacho chakula cha kutosha kwa zaidi ya asilimia 110, hii haijapata kutokea toka nchi yetu imepata uhuru. Vyakula vilivyopo leo hii ni zaidi ya asilimia 110, naamini ofisi hii haishindwi kuja kutuletea hata kama vyakula vikikosekana, hata mbegu za msaada ili tuweze kupanda pale maji yanapokuwa yametulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba mafuriko yameleta maafa makubwa katika kila sekta kwa mfano vipo vituo vya afya ambavyo vimezingirwa na maji na vingine havifai kabisa. Eneo la maporomoko ya mto yamekikumba Kituo cha Afya cha Muhoro, tayari ofisi yetu ya Wilaya Ofisi ya Mkoa tumekwishaandika barua TAMISEMI kuweza kuomba fedha za dharura ili wananchi wetu waweze kujengewa kituo cha dharura kwa sababu eneo hili la Muhoro lina wakazi zaidi ya 25,000.

Kwa hiyo niombe Ofisi ya Rais TAMISEMI, watakapokuja kufunga hapa watuambie iwapo kama kuna fedha hizi za dharura ambazo tunatambua kwamba zipo waangalie uwezekano wa kuwasaidia wananchi hawa.

Mheshimiwa Spika, leo hii wananchi wa Muhoro wanakosa matibabu, japokuwa tunatambua kwamba maji yameanza kuondoka taratibu, japokuwa yapo mabwawa mengine ambayo yemefunguliwa hivi karibuni, maji haya yanaweza kuchukua muda mrefu kwa kuwa mafuriko ndio kwanza yataanza mwezi huu mwezi wa nne kule kwetu Rufiji. Kwa hiyo tuwaombe Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa fedha za dharura kuweza kuona uwezekano wa kuwaangalia wananchi wetu wa Kata ya Muhoro kwa kutoa fedha hizo ili tuweze kujenga kituo kuwahudumia wananchi zaidi ya 25,000 ambao kwa leo hawana hawapati huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, mafuriko yameathiri ikiwa ni pamoja na mradi wetu wa kuzalisha umeme mradi ule wa Mwalimu Nyerere. Tunapata kigugumizi wakati mwingine pale ambapo tunamtafuta Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi kumweleza maafa ya mafuriko kwenye mradi huu Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hajawahi kufika Rufiji kupitia barabara ambayo mradi huu unaelekea. Barabara kubwa inayotumika ni barabara ya Kibiti kuelekea Mroka lakini Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi hajawahi kufika Rufiji kupitia barabara hii, pengine anasubiri Mheshimiwa Rais akiwa anakwenda yeye ndio aje Rufiji kupitia barabara hii. Hata nilipozungumza naye alisema amewaagiza wataalam wake kupeleka vifaa kupitia Morogoro. Vifaa hivi vinatoka Mtwara Dangote, inawezekana vipi vitoke Dangote vipite Pwani, vipite Dar es Salaam viende kwenye mradi wa umeme.

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa umeme kama kweli Taifa letu limedhamiria ukamilike wakati Mheshimiwa Rais wetu Magufuli akiwa madarakani, basi ni vyema wataalam hawa wakafika maeneo haya, barabara hii…

SPIKA: Ni barabara unayoongelea Mheshimiwa?

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, ni barabara ya Kibiti - Mroka. Barabara ya Kibiti - Mroka imeharibika na magari makubwa yameharibu barabara hii hata mafuriko ya mwaka 62 barabara hii iliendelea kupitika lakini leo hii barabara hii haipitiki, inachukua masaa 10, barabara hii inahitaji tu utatuzi…

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa unapata taarifa toka kwa Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mbunge anayeongea Mheshimiwa Mchengerwa mjukuu wangu kwamba mvua zilizonyesha ni mvua za return period ya miaka 100. Wakati tunaanza mradi wa kujenga Bwawa la Nyerere mkandarasi alipewa barabara tatu; barabara ya kwanza ni hiyo Kibiti - Mroka, njia ya pili ilikuwa ni kwenda na TAZARA, anakwenda mpaka eneo la Fuga na tuliimarisha na ile barabara ya kutoka Fuga kwenda kule, nayo imeimarishwa vizuri, lakini barabara ya tatu ilikuwa ni ya upande wa Morogoro na yeye amekuwa anatumia zaidi ile barabara ya kule kwa Mheshimiwa Mchengerwa kwa sababu ni kweli ni fupi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mvua zilizonyesha kuna kipande cha mita 200 ambacho kuna bwawa lipo eneo lile, limeungana na mafuriko ya Mto Rufiji na kile kipande kina maji ya kina cha mita mbili, kwa hiyo hakuna namna yoyote gari linaweza likapita. Kwa hiyo, mkandarasi sasa hivi atapita Fuga au atapita njia iliyoko kule upande wa Morogoro. Kwa hiyo nilitaka kumpa taarifa kwamba hii ni nature ambayo hatuwezi kufanya chochote kwa akili ya kawaida ya mwanadamu. Naomba avumilie tu Mheshimiwa Mchengerwa baada ya mafuriko kupita na barabara ile kukauka basi hatua nyingine zitafanyika.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, tunachoomba Mheshimiwa Waziri apite kwenye hii barabara ajionee. Hii barabara miaka yote toka mafuriko ya 1962 mafuriko ya 1974, mafuriko ya 1998, 1988, 2018 barabara hii iliendelea kupitika, leo hii wananchi wangu wanatumia masaa 10 kupita barabara hii, mimi mwenyewe nimepita, yako matrekta yanapita pale kinachohitajika ni kifusi tu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la aibu kwenye mradi huu, mradi unatekelezwa Rufiji, waathirika wa kwanza watakuwa ni Warufiji, lakini cha kushangaza Mkurugenzi wa Kinondoni anaomba service levy ya utekelezaji wa mradi. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aeleze hapa, mradi huu uko Rufiji, unatengenezwa Rufiji, Warufiji ndio watu wa kwanza kuupokea kupitia Mbunge wao, lakini mpaka leo service levy haijalipwa Rufiji, watu wa Kinondoni wanaitaka service levy,. Angalia ajira 3,300 Warufiji waliajiriwa ni 200 kati ya ajira 3,300, tukiuliza ni upande wa nishati, hatupati majibu; tukimuuliza mkandarasi yeye ameweka watu tu, kwa hiyo athari zakwanza za mradi huu zitawakuta wananchi wa Rufiji na sisi ndio watu wa kwanza kuupokea mradi huu hatuna tatizo hata kidogo.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye Hansard hotuba yangu ya mwaka mwezi Novemba, 2016, nilipambana na Mheshimiwa Waziri Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati wakati ule kuomba utekelezaji wa mradi huu tunachoomba Warufiji wapate haki hata kama kidogo; hatuna nishati, hatuna madini, hatuna Tanzanite, tuna mradi huu, hiki ndio kitu pekee tulichonacho. Tunachoomba Wizara hizi mbili ziwaangalie Warufiji kwa sababu ndio watu wa kwanza utekelezaji wa mradi huu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)