Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili basi nami niweze kuchangia katika hotuba ya mtani wangu Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa wasilisho zuri la jana, ameonesha umahiri mkubwa, Watanzania wameelewa vizuri na wameelewa utendaji wa shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Spika, nianze na wazo la kuzitaka Halmashauri kwamba mapato yake ya ndani, zile asilimia kumi zigawanywe kwa akina mama, vijana na watu wenye ulemavu na likapitishwa kuwa sheria. Ni jambo jema sana na Halmashauri nyingi sasa zimeanza kutekeleza vizuri ingawa zipo ambazo zimeanza kukwama, zinaanza kuzalisha madeni. Ukiwauliza kwa nini mnafanya hivyo? Kati ya sababu wanazozisema ni pamoja na kwamba wanakosa vikundi sahihi vya kuvipelekea fedha hasa katika asilimia mbili.

Mheshimiwa Spika, ziko Halmashauri nyingine mapato yake ya ndani ni makubwa sana. Asilimia mbili kwenda kwa walemavu inafikia wakati kwamba wanakosa sasa walemavu waliopo kwenye vikundi ili waweze kupata zile fedha matokeo yake wanashindwa kupeleka zile fedha. Sasa naomba hili Serikali waliangalie kwa makini, kwa sababu vinginevyo upo uwezekano walemavu uwezo wa kuwaweka kwenye vikundi ni mgumu na wanashindwa kupata hizo fedha.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kwamba kama hivyo ndivyo, basi walemavu wana yale mahitaji yao maalum kulingana na aina ya ulemavu waliokuwa nao; na mpaka sasa hatujawa na utaratibu maalum wa kuhakikisha mahitaji hayo yanapatikana.

Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Mheshimiwa Amina Mollel, nilitegemea unasikiliza, hoja muhimu hii. Endelea Mheshimiwa Vedasto.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika maeneo ya vijijini walemavu wa ngozi hawana uelewa wa kwamba kuna mafuta maalum kwa ajili ya kuboresha ngozi zao. Hawajkui lolote, hawajui kabisa na Serikali haijatenga na hatujawa na fungu maalum la kuhakikisha hawa walemavu wanapata elimu, lakini ikiwezekana wanapata hayo mafuta.

Mheshimiwa Spika, viungo bandia vinauzwa kwa bei ya ghali sana. Ikitokea mlemavu anataka kupata kiungo bandia cha mguu, ni bei ghali sana na Serikali haijawa na mpango maalum. Ila shime sikio, fimbo nyeupe, kama hivyo ndivyo, naishauri Serikali ije na waraka maalum kwamba kama wanashindwa kupeleka zile asilimia mbili kwa vikundi vyote, basi hizo fedha zitumike ili wawanunulie walemavu mahitaji maalum kulingana na aina ya ulemavu waliokuwa nao. Hii itakuwa ni msaada sana kwa walemavu. Naomba hilo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nizungumzie vitambulisho vya wajasiriamali. Serikali ilikuja na utaratibu huu wa vitambulisho vya wajasiliamali na vikagawiwa kwa wajasiriamali kwa mchango wa shilingi 20,000/=. Hivi karibuni kumekuwa na utaratibu ama kusitisha au Serikali kama haijaeleza nini sasa kinafuata, lakini katika baadhi ya maeneo kwa mfano kwangu mimi pale Kilwa Kaskazini maeneo ya Somanga maeneo mengine, watendaji wamewanyang’anya wajasiriamali vitambulisho ambavyo tayari wameshanunua.

Mheshimiwa Spika, ni mbaya sana Wajasariamali wamenunua vitambulisho Watendaji wanakwenda kuwanyanganya vitambulisho bila hata kuwarejeshea na hawatoi maelezo ya kina kwa nini wanaamua kuchukua vile vitambulisho. Naomba Serikali ifuatilie hilo kwa sababu vinginevyo kunakuwa na mkanganyiko miongoni mwa wananchi, na wananchi wanaiona kama Serikali imewahadaa jambo ambalo nafikiri hilo liwekwe vizuri ili wananchi inapotokea tena Serikali ikija na program ya aina hiyo waipokee na waone tija ya jambo kama hilo kufanyika.

Mheshimiwa Spika, tuzungumzie suala la maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu ndio inashughulikia mambo ya maafa na majanga. Nichukue nafasi hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mwaka huu umekuwa ni mwaka wa Majanga na maafa na kutokana na mvua zilizokithiri, tuna mafuriko kule kwangu maeneo ya Njinjo, kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na sasa hivi Mto Rufiji umefurika kwa hiyo tuna matatizo, tuna matatizo makubwa ambayo Ofisi ya Waziri Mkuu inatakiwa iangalie kwa kina.

Mheshimiwa Spika, na kati ya jambo ambalo limejitokeza ni pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya Serikali ikiwemo Shule, Vituo vya Afya, kitu ambacho au jambo ambalo linapelekea kwa mfano katika Tarafa ya Njinjo shule nne miundombinu yake imeharibiwa kabisa na maji mpaka leo tunavyozungumza kuna zaidi ya wanafunzi elfu tatu hawana sehemu ya kusoma, niombe Serikali iliangalie jambo hili kwa uharaka kuhakikisha watoto wale wanapata sehemu ya kusoma kwa sababu hili ni janga na suala la kupata elimu ni jambo la muhimu nani haki ya watanzania wote. (Makofi)

SPIKA: Ungezitaja ingekuwa vizuri zaidi kama unazikumbuka hizo shule.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, kuna Shule ya Msingi Njinjo, kuna Shule ya Msingi Ndende, kuna Shule ya Msingi Msitu wa Simba na Shule ya Msingi Wenje, hizo shule haziwezi tena kutumika ninaomba sana Serikali iwaangalie wananchi wa Jimbo la Kilwa Kaskazini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jingine nizungumzie Vita ya Majimaji nahii marazote ninavyochangia hotuba ya mtani wangu Waziri Mkuu lazima niseme hili kwa sababu ndio kilio cha watu wa Kilwa. Mheshimiwa Waziri Mkuu watu wa Kilwa wanaomba kwa kuwa Vita ya Majimaji imeanza Kilwa, wanaomba sana Serikali itenge bajeti ya Sherehe ya Vita ya Majimaji kama ambavyo inafanyika Songea na sisi watu wa Kilwa tupate hiyo haki. Wanaomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu nafikiri mtani wangu utakuwa umenisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze suala la Corona, suala la Corona Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wamezungumza Serikali imechukua hatua ni jambo jema…

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Vedastus pokea kutoka kwa Mheshimiwa Mchengerwa.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Naomba nimpe taarifa jirani yangu kwamba vita vya Majimaji vilianzia Rufiji katika Kijiji cha Tawi sio Kilwa. (Makofi)

SPIKA: Namuona Chief Whip nae ameniandikia hapa kwamba vita vya Majimaji vilianzia Songea na sio Rufiji wala Kilwa. (Makofi/Kicheko)

Sasa sijui nani ataamua ugomvi huo, Mheshimiwa Vedasto endelea.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, taarifa ya ndugu yangu Mchengerwa siipokeu kwa sababu yeye anajua kwamba Vita ya Majimaji ilianzia Kilwa katika Kijiji cha Nandete na Majemedali wake anawafahamu kama kina Ngulumbalio, Mandali, Ndimio Machela na wengine wakina Kinjekitile Ngwali na wengine. Kwa hiyo, hiyo inafahamika na tunavyo vitabu na hatuna haja, Mheshimiwa Jenista analifahamu hilo kwa hiyo naomba hilo tuliache, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu alizingatie hilo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia suala la korona kama ambavyo...

SPIKA: Kwa hiyo Kinjekitile alikuwa Mngindo!

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Alikuwa Mngindo na alikuja Kilwa kama mganga wa kienyeji.

SPIKA:Okay (Makofi/Kicheko)

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Yah! (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Corona imezungumzwa na niipongeze Ofisi yako ya Bunge kwa hatua ambazo tulichukua kwa ajili ya kuzuia lakini naomba suala la Corona lipate uhalisia. Kama wewe, Wabunge wako umewaelekeza kuchukua tahadhari kule kwa wananchi bado mambo hayajakaa sawasawa kuna mikusanyiko ya hovyo, ya holela naomba Serikali ikaze uzi kidogo. Hatuna sababu mpaka leo kwamba mabaa tunayo yanaendelea tu kiholela holela, hatuna sababu kwamba ukienda feli kwa mfano hata usafiri wetu na namna tunavyosafiri bado hatujakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali ikaze uzi kidogo kwa sababu vinginevyo tusipoziba ufa tutakuja kujenga ukuta hali itakuwa mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, jingine nizungumzie suala la Bima ya Afya kwa wote. Miaka mitano tunamaliza tuliahidiwa hapa Serikali italeta Muswada wa Sheria wa Bima ya Afya kwa wote lakini mpaka sasa hivi Serikali ni kama inasuasua. Wananchi wa Tanzania wanapata shida sana kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa namna ya kupata huduma ya matibabu. Serikali ije na Muswada wa Sheria kwa ajili ya Bima ya Afya kwa wote sijui kwa nini Serikali inalega lega nafikiri hili lingefanyika basi wananchi wangekuwa na uhakika wa kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kipato cha mwananchi wa kawaida akipata maradhi yoyote uwezo wa kumudu matibabu kwa fedha za mfukoni ni ngumu sana lakini tukumbuke ya pia, CHF imefeli imeshindwa lazima tuwe na mpango mwingine. Mheshimiwa Jenista naomba ujitahidi utuletee huo Muswada wa Sheria ili basi tuhakikishe tunawapatia wananchi wetu huduma ya uhakika ya matibabu.

SPIKA: Mheshimiwa Vedasto asante sana.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, asante sana nashukuru.