Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili nipate kutoa mchango wangu. Kabla ya hapa naomba tumshukuru Mwenyenzi Mungu aliyetujalia uhai mpaka tunakuwa na mazingira ya kukusanyika hapa pamoja na majanga mbalimbali tunawatumikia wananchi.

Mheshimiwa Spika, niungane mkono na wenzangu walioanza na nakumbuka mwezi Novemba, 2015 Mheshimiwa Rais alikuja humu na wengine waliondoka. Hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa so impressive, ilikuwa na matumani makubwa sana na tunaona kwa miaka mitano yametekelezwa. Kwa hili tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kundi lake la Baraza la Mawaziri kwa kweli wametutendea haki, sina haja kutamka wametekelezaje ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo sisi tulienda kuahidi Watanzania tutawafanyia nini kwa miaka mitano, kwa kweli kwa kiasi kukubwa yamefanyika, pongezi sana kwa Serikali waetutendea haki. Sasa sisi wengine wa CCM tunatembea kifua mbele, maana yake sisi wa Morogoro tunasema manta hofu maana yake tunatembea bila wasiwasi, tunaenda Oktoba hii tuna hakika tunawafyeka tena.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu utajikita zaidi kwenye hotuba hii ibara ya 43 mpaka 45, ni kwamba tumeendelezwa kupitia Dira ya Taifa kwamba ifikapo 2015 tutaingia uchumi wa kati, uchumi unaowezeshwa na viwanda. Hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu imeleeza, imenyooka moja kwa moja na hata ukiangalia Mpango wa Maendeleo wa 2020/2021 na hata bajeti imesisitiza na imetengeza vile vipaumbele vinne mojawapo ni kuwezesha uchumi wa viwanda ili twende huko katika Dira ya 2025.

Mheshimiwa Spika, hivi viwanda tunavyovizungumzia vikubwa vingi vinatokana na mazao ya kilimo na mifugo. Hali ilivyo kama tunataka twende huko kuwezesha hivyo viwanda ni lazima tuwe kilimo cha biashara na mojawapo ya sifa za kilimo cha biashara ni lazima muwe na miundombinu ya uhakika na usafiri na usafirishaji. Ni lazima muwe na maji, maji haya kilimo kinahitaji maji, tusitegemee ya mvua za Mwenyenzi Mungu, maji ya skimu za umwagiliaji. Tatu, tunahitaji nishati ili kuchakata mazao yetu, kuongeza thamani, na la nne ni soko la uhakika. Serikali naona wanatupeleka huko, lakini balaa la mwaka huu, maana mwaka huu ni changamoto kidogo, maradhi upande wa pili tuna mvua nyingi sana ambayo imeharibu miundombinu ya barabara na madaraja.

Mheshimiwa Spika, mfano tu ni barabara ambayo inapita katika ukanda mkubwa wa uzalishaji ambapo Serikali wamepeleka Mradi wa SAGCOT ambayo inaanzia Mikum – Ifakara – Lupilo – Malinyi - Kilosa Mpepo – Londo – Lumecha - Kitanga - Songea. Barabara hii ikiwezeshwa itatufikisha tunakokwenda kwenye uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja na ameona barabara hiyo, naipongeza Serikali wameanza hatua ya kuifanyia kazi kwa vitendo maana CCM inafanya kazi kwa vitendo. Mmeweka mkandarasi kile kipande cha kilometa 70 kuanzia Mkamba - Ifakara, sasa ni mwaka wa pili, wa tatu mkandarasi yule anasuasua. Kila tukijiuliza hatupati majibu, Serikali tuambieni tatizo liko wapi, anatuchelewesha huyu na ndiyo maana upande wa pili wanapata ajenda. Tunakwenda kwenye uchaguzi, Mheshimiwa Waziri Mkuu hebu mwangalieni huyu mkandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkimaliza kipande cha kuanzia Ifakara mmeahidi mnakwenda kipande cha Ifakara – Lupilo - Malinyi - Songea, barabara hii ni muhimu sana. Kama tunataka kilimo cha biashara barabara hii ndiyo itawezesha kupeleka mazao haya kwenye soko na vilevile ndiyo itakuwa kivutio. Kilimo cha biashara tusitegemee hawa wakulima wetu wa kawaida wadogo wadogo, tunahitaji wawekezaji na mwekezaji hawezi kuja kwenye maeneo ambayo hakuna usafiri wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeahidi mara nyingi sasa ni wakati muafaka muanze kujenga barabara hiyo nayoizungumzia ambayo ina tija kwenye mwelekeo wa kumfanya Mtanzania aingie kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025 na wala siyo mbali. Habari njema bado tunaye Jemedari, mtu anayethubutu, Dkt. John Pombe Magufuli ndani ya miaka mitano atatufikisha huko kwenye uchumi wa kati 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, sipendi kuzungumzia huu ugonjwa mpya ulioingia ambao unasababishwa na Virusi vya Corona. Mimi ni mjumbe wa Kamati ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya. Tunaipongeza Serikali wamepokea ushauri wetu, wameufanyia kazi lakini kuna mambo mawili, haya naendelea kusisitiza kama wajumbe wenzangu walivyosisitiza tusije tukachanganywa na huu ugonjwa mpya, bado UKIMWI ni tishio.

Mheshimiwa Spika, kwa miaka iliyopita bajeti ya kudhibiti ugonjwa wa UKIMWI tunategemea fedha kubwa kutoka kwa wafadhili, karibu mpaka asilimia 98. Sasa ifike wakati pamoja na changamoto hizo, tena habari ambayo siyo njema tayari baadhi ya wafadhili wamepunguza msaada huo wao kwa asilimia 23.

Mheshimiwa Spika, niombe kwenye bajeti hii tuanze kuwekeza kwenye vita dhidi ya UKIMWI kwa fedha zetu za ndani angaliu asilimia 75. Tumelizungumza sana suala hili sasa tumefikia mwisho na Kamati inavunjwa lakini mtakuja mtukumbuke. Kama tusipowekeza kwenye vita dhidi ya UKIMWI kwa pato la ndani na huyu adui mwingine wa Corona aliyeingia ndiyo tutazidi kuchanganyikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine kwenye UKIMWI ni Mfuko wa UKIMWI (ATF). Mfuko huu tunauzungumzia lakini bado una changamoto na sisi tumependekeza ikiwezekana wekeni tozo au kwa sababu ninyi mna wataalam tafuteni vyanzo vingine, vinginevyo huu Mfuko utabaki kuitwa Mfuko lakini hauna fedha, Mfuko maana yake ni fedha.

Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)