Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya uchangiaji katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nilikuwa nataka nijikite kwenye baadhi ya mambo machache lakini jambo moja kubwa la kwanza ni janga la ugonjwa huu wa Corona ambalo limekumba dunia Tanzania ikiwa ni mojawapo. Nilikuwa na ushauri kidogo kwa Serikali kwamba ni lazima tuongeze bidii katika zile hatua ambazo zilishachukuliwa lakini lazima tuongeze bidii ya kusukuma hatua zingine zaidi ili tujitahidi kuzuia janga hili lisije likaingia nchini kwa kiwango ambacho limeshaingia katika mataifa mengine nadhani kwa uwezo wa uchumi wetu hatutakuwa na uwezo wa kukabiliana nalo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nashauri jambo la kwanza ni lazima tuone namna ya kupata fedha kwa namna yoyote kupitia njia zozote zile za kibajeti na zile ambazo sio za kibajeti labda za kutumia wadau mbalimbali tupate fedha kwa ajili ya kuweza kununua vifaa vya upimaji angalu watu wengin kadri iwezekanavyo waweze kufikiwa na vipimo ili tujue kiwango cha watu walivyoathirika katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tunaweza tukaamini kwamba tuna watu wachache sana ambao ni wagonjwa lakini hatuna uhakika kulingana na vipimo bali kutokana na hali ya kuibuka kwa wagonjwa ambako inawezekana bado wagonjwa wengi wamejificha ndani. Kwa hiyo, ni vizuri tukajua kiwango ambacho tuna maambukizi ili tuweze kukabiliana nayo kwa haraka kadri iwezekanavyo kabla ya kuruhusu hii jambo likawa kubwa katika jamii yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuona namna ambavyo hata vifaa hivi vya kunawia mikono vinavyoweza kupatikana katika maeneo mbalimbali mpaka sasa hivi hivi vifaa vinapatikana kwa watu wenye uwezo fulani, kwa kundi fulani. Lakini walio wengi bado hawajaweza kufikiwa na hivi vifaa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watu sasa hivi wanachukua sabuni wanajitahidi kunawa lakini je hizi defectant ambazo zinatakiwa zitumike kwa kiwango gani zimefika kwa jamii yetu ni suala la Serikali kusukuma hili ili tuone namna ambavyo tunatumia Serikali zetu za mitaa, wakurugenzi wetu, watendaji wetu wa kata tuone jinsi ambavyo tunaweza tukasaidiana ku-mobilize watu hata wadau mbalimbali wachangie kuhakikisha kwamba hata watu wa chini wanafikiwa na huduma hii ili tupunguze uwezekano wa haya maambukizi. Pia elimu iende kwa upana zaidi kuliko inavyoenda sasa kuna jitihada zipo lakini tuongeze jitihada zaidi katika elimu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuangalia athari zake kiuchumi, janga hili kwa sura yoyote ya kawaida lazima litakuwa na athari za uchumi katika Taifa. Tunavyozungumza sasa nina hakika kabisa kwamba sekta ya utalii itakuwa imeathirika sana na wafanyabiashara wengi wa utalii kwa vyovyote vile watakuwa tena hawapokei watalii. Shirika kama la ndege litakuwa limeathirika sana na watu wanaopeleka bidhaa nje watakuwa wameathirika, watu wanaoingiza bidhaa kutoka nje watakuwa wameathirika. Kwa maana hiyo hata wafanyabiashara wa ndani ya nchi watakuwa wameathirika kwa kiwango fulani sasa tunapimaje hiyo adha na hiyo hali manake slogan yetu kubwa kama Serikali ni kukusanya kodi lakini tunatakiwa tukusanye kodi kwa watu wenye uwezo wa kulipa kodi, tunasaidiaje hao watu ili angalau wapungukiwe na huo mzigo unaotokana na adhari wanayopata kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ingekuwa inakaa na wataalam wake kupima adhari za kiuchumi za tatizo hili na kuona jinsi ambavyo wanaweza kuchukua hatua za kusaidia watu wetu katika athari hizi za kiuchumi, kwa sababu wenzetu wa Rwanda wameshafanya, wenzetu wa Kenya wameshafanya baadhi ya hatua kiuchumi tumefanana nao kwa kiwango fulani. Kwa hiyo, nadhani tunaweza tukachukua baadhi ya hatua tukiangali wenzetu wanavyofanya na zile ambazo tunaweza tukachukua ndani yetu sisi wenyewe. Kwa hiyo, nilidhani kwamba tunapaswa kulipima hili janga kwa uzito unaostahili ili watu wetu wasiumie, wafanyabiashara wetu wasiumie na wananchi wetu wa kawaida pia wasiumie.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumze suala la uchaguzi mkuu, tunaenda kwenye uchaguzi kulingana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba tunaenda kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu Octoba. Ni vizuri tukajitambua kwamba hapa ndani sote ni watanzania na kujitambua kwamba wote tuna haki ya kufurahia matunda ya uhuru wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo baya sana kama watanzania kutakuwa na kundi linaloamini kwamba lenyewe ni bora zaidi kuliko kundi lingine katika nchi moja. Kwa hiyo, ni vizuri kwanza sense yetu wote mawazo yetu tubaki pale ambapo mwasisi wa Taifa hili alituweka miaka yote kwamba sisi wote ni watanzania. Mifumo hii ya vyama vya siasa isiwe sababu ya kutubagua na kutugawanya, mifumo ya vyama vya kisiasa iwe ni sababu ya kutuunganisha na kuweka mawazo mbadala kusukuma Taifa hili mbele. Sasa kama tutatafsiri vinginevyo mifumo hii ya vyama vya kisiasa ikatubagua ikaonekana kuna watu bora kuliko wengine katika Taifa moja maana yake tunalipeleka Taifa hili mahali ambapo sipo mahali ambapo si salama kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna amani ambayo tumeijenga kwa miaka mingi sana amani hii haikuangauka imejengwa kwa nguvu za watu na kwa jitihada za watu ni lazima amani hii ilindwe kwa nguvu zote. Mara nyingi chaguzi zimekuwa ndio sababu ya kuvunja amani ya Taifa, amani za nchi, kuvunja umoja wa watu. Kwa hiyo, ni lazima tukubaliane kama kuna watu wanaonung’unika wanaoamini kwamba kuna mambo ambayo hayaendi sawasawa ndani ya Taifa letu tusijadili kwamba wanaonung’unika ni akina nani tusiwaangalie kwa itikadi ya vyama vyao vya kisiasa kwa dini zao wala makabila yao tuwaangalie kama watanzania na tuwasikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilio kikubwa cha watanzania hao wanaoonekana wanapenda kulalamika ni Tume huru ya uchaguzi lazima tujiulize tume hii maana yake tukijadili hapo mara nyingi majibu ya Serikali ni kwamba mbona na nyie mlishinda na nyie mko huku ndani. Ni kweli tulishinda lakini tukishinda kwa ngarambe hatukushinda kirahisi. (Makofi)

Pili, angalau hata mazingira yale ya kipindi yalikuwa yana nafuu sio mazingira ya sasa ambapo msimamizi wa uchaguzi anaweza akaondoka kwenye ofisi yake asipokee fomu za mgombea. Anaweza akakataa fomu za mgombea, polisi anaweza akaingia mahala akafanya vurugu yoyote kusumbua mawakala sio hali hiyo ilivyokuwa huko nyuma, kulikuwa kuna shida lakini zilikuwa sio kwa kiwango hiki. Sasa sisi tunachokiomba ni kwamba uchaguzi huu uwe huru na uwe huru kweli, ili kila mmoja aridhike.

Mheshimiwa Spika, tunaamini kuna mambo ambayo yamefanyika ambayo siku zote tunasema ni mazuri yamefanywa na awamu hii sasa kwa maana hiyo twendeni kwenye uchaguzi ulio haki na uhuru. Kwa hiyo nilidhani kwa machache hayo nikushukuru kwa nafasi hii ahsante sana.