Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Zainabu Mussa Bakar

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ZAINAB MUSSA BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia napenda kuzungumzia miradi mitatu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni Mradi wa Barabara ya Wete hadi Chakechake, takribani kilomita 40; Bandari ya Mpiga Duro Malindi Zanzibar na Mradi wa Ujenzi wa Airport ya Pemba na hitimisho la Uwanja wa Ndege wa Unguja Terminal 3. Serikali ya Muungano ikishirikiana na Wizara ya Fedha wamekataa miradi hii isiendelee na Wazanzibar wasifaidike na miradi hii; uchumi wa Wazanzibar uendelee kudidimia. Nasema hivi kwa sababu Serikali ya Muungano imekataa kuweka saini kwenye miradi yote hii maana yake hawapendi kuona maendeleo katika upande wa pili wa Muungano yakitokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni unyanyasaji na ni hasadi ya hali ya juu kabisa. Serikali ya Muungano inashindwa kujenga kilomita 40 Zanzibar lakini Tanzania Bara wanajenga zaidi ya kilomita 1,500 za barabara; hii kama si hasadi ni nini? Kila siku tunaambiwa tu wachochezi tukizungumzia suala la Muungano, kwamba halina umuhimu wowote kwa maslahi ya Zanzibar. Leo hii limedhihirika kwa kukataa kuweka saini; halafu tunaambiwa ni ndugu zetu wa damu. Damu gani hii ya kudhulumiwa? Huu si ndio udugu wa makopa wa kukutania kwenye sufuria, ambao hauna faida yoyote ile? Bora ukatike, udugu huu hauna tija yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali ya Muungano iweke saini ili tujenge barabara, bandari ambayo inaweza kufunga gati kwa meli zisizozidi 5 ingawa ya Bagamoyo mlikata wenyewe ambayo ingeweza kufunga nanga meli takribani 35. Mliikataa wenyewe ila sisi tunahitaji hiyo bandari na viwanja vijengwe ili kuinua uchumi wa nchi yetu. Serikali hii ya Awamu ya Tano haijui kipaumbele chake. Iliingia madarakani kwa kujigamba, kujinata na mbwembwe tele kuwa ni Serikali ya viwanda mpaka, sasa hatuoni viwanda hivyo na vichocheo vya viwanda havipewi pesa za kutosha. Tukiangalia sekta ya kilimo imetupwa mbali wala haithaminiwi. Ni wazi kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Kilimo inachangia ajira kwa asilimia 70, Pato la Taifa kwa asilimia 28.2, lakini ukuaji wake ni mdogo sana na wa kusuasua, sawa na asilimia 5.2. Hali hii inapelekea kutofikia ndoto ya Tanzania ya Viwanda. Napenda kuishauri Serikali kuondoa kodi zifuatazo ili kufikia kwenye ndoto ya Tanzania ya Viwanda.

(a) Kodi kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

(b) Hali kadhalika kuondoa kodi kwenye viwanda vinavyotengeneza na kukarabati mashine, zana na pembejeo za kilimo, uvuvi na mifugo.

(c) Pia uwepo wa umeme wa uhakika.

(d) Kushirikisha sekta binafsi kwa kupitia mpango wa PPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri Mpango ayachukuwe haya na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imewasusa watumishi wa umma ambao ni walipa kodi wa uhakika. Serikali hii imekuwa ikisuasua kuwapa watumishi nyongeza ya mshahara ya kila mwaka (annual increment) pamoja na madai yao mengi kama fedha zao za likizo, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya mishahara; jambo ambalo ni la kisheria na kikanuni. Hata wanaopandishwa madaraja halafu unastahiki pindi wakipandishwa madaraja hulipwa mshahara uleule wa mwanzo; jambo ambalo si halali. Hata hivyo katika mwaka huu wa fedha nimeona takribani trilioni saba. Hizi ni za mishahara tu hizo nyingine sijaziona.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali ya Awamu ya Tano wataacha kuwakandamiza watumishi hawa? Huku ni kuwafanya maisha yao yaendelee kuwa magumu; na pia Serikali hii haina nia njema kwa watumishi hawa. Hali kadhalika kuna dalili ya kuwadhulumu mafao watumishi hawa ambao ni walipa kodi wa uhakika wa nchi hii. Tunaitaka Serikali iache mara moja tabia hii ya kuwadharau watumishi hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusu taulo za kike. Tunaitaka Serikali iache kigeugeu itoe hiyo kodi kama ilivyofanya awali ili watoto wetu wasitirike na kutowatoza kodi kutokana na maumbile yao na jinsi yao. Huu ni unyanyapaa na ubaguzi wa hali ya juu, kuwatoza kodi kila mwezi na wengine mwezi mara mbili kwa ajili ya maumbile yao. Jambo hili halikubaliki na hata dini zetu hazikubali. Naomba kuwasilisha na naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani na yale yenye manufaa ya Waheshimiwa Wabunge wengine. Ahsante.