Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha leo hii kuweza kuijadili bajeti ya nne kwa Awamu hii ya Tano – 2019, chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Mpango; Naibu wake, Mheshimiwa Ashatu Kijaji pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa umakini wao kwenye kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka huu imegusa kila sekta katika nchi yetu na kuelekea kwamba hali ya uchumi itazidi kuwa nzuri kwa wananchi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umeme wa Maji, Bonde la Rufiji (Stiegler’s Gorge), ni mradi ambao umeleta sura mpya kwa Taifa letu na uhakika na wepesi wa maisha kwani bei ya umeme itashuka, viwanda vingi vitajengwa, wananchi watapata ajira, kutakuwa na utunzaji na uboreshaji wa mazingira na kilimo cha umwagiliaji kitaongezeka. Haya yote ni matarajio makubwa sana kwa Taifa na pia kwa mikoa inayozunguka eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya SGR lazima kuwe na umeme wa bei nafuu ili treni ziweze kufanya safari zake, hivyo mradi wa Stiegler’s Gorge ni sahihi kabisa. Ni vyema, Serikali ikaanza utaratibu wa ujenzi wa skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo kwani maeneo mengi yapo kwenye bonde. Hii itasaidia uzalishaji wa chakula na ajira pia kuwa na viwanda vya kukoboa na kusaga nafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara toka Ubena Zomozi hadi eneo la mradi na kutoka eneo la mradi hadi Utete – Nyamwage kwa kiwango cha lami itafungua uchumi wa nchi na matumizi ya Bandari ya Mtwara na nchi jirani. Pia utalii uliopo Kusini mwa Tanzania ikiwemo na Mafia. Pia barabara ya Kibiti – Mkoka itakapokuwa kwa kiwango cha lami itainua uchumi wetu. Ujenzi wa bwawa hilo sio kitu kigeni duniani kwani hata Ethiopia, Egypt na kwingineko wanajenga. Nimalizie hoja hii kwa kusema kelele za mlango hazizuii mtu kulala.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kodi kwenye viwanda vya taulo za kike ni zuri, hii itasaidia wanawake na watoto wa kike (wasichana) kuweza kumudu kupata kununua hizo taulo. Ni vyema Serikali ikaweka utaratibu wa bei maalum pia utaratibu wa kuhakikisha maeneo mengi vijijini, zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizo pembezoni zinapata taulo hizo kwa urahisi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza kodi kwenye mawigi, hii haina faida yoyote kwa jamii uzuri au kupendeza kwa mtu ni vile unavyojiremba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.