Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote ningependa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu ya kila siku katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni; fedha zinazopitishwa na Bunge katika kila Wizara kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hazifiki kwa wakati na pia fedha zitolewazo hazipelekwi zote na hazitoshelezi kuweza kuendeleza miradi hiyo. Naishauri Serikali katika kila Wizara fedha zinazopitishwa na Bunge ziwe zinaakisi hali halisi ya kuweza kuitekeleza miradi ya maendeleo katika Wizara husika na pia fedha hizo zitolewe kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa malimbikizo ya madai; katika hotuba ya Waziri, ulipaji wa madai umeelezewa katika ukurasa wa 15-16 kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri. Kuna madai ambayo ndani ya hotuba hii hayajatolewa maelezo kabisa. Wamiliki wa Viwanda ambao wanatumia sukari ya viwandani, takriban miaka minne wanaidai Serikali bilioni 45 na ni kiasi kidogo sana ambacho Serikali imewalipa shilingi bilioni sita tu ndizo zilizotolewa. Hii hudhoofisha mustakabali mzima wa kuelekea Tanzania ya viwanda, maana wafanyabiashara hawa wanaidai Serikali na kukwamishiwa mitaji yao na kupunguza uzalishaji katika viwanda vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuchelewa kurejesha kwa ushuru wa forodha 15% (Refundable Import Duty 15%) katika sukari ya viwandani. Serikali imeleta changamoto kwa wahusika jambo lililopelekea kiasi cha mitaji ya wazalishaji wetu kushikiliwa na Serikali na kuwapunguzia mitaji yao. Nashauri fedha hizo zilipwe ili wamiliki wa viwanda hivyo waweze kufanya kazi ya kuzalisha bidhaa zao bila kusuasua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya vipaumbele kwa mwaka 2019/2020, ambapo katika kitabu cha hotuba ya Waziri, kuhusu kipaumbele cha viwanda na kilimo, kwa upande wangu sijaona sehemu yoyote katika hotuba hii inayozungumzia kuhusu jitihada za Serikali katika kuchukua hatua za kisheria kwa vile viwanda vilivyobinafsishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iunde Tume Maalum ya kufuatilia viwanda vyote vilivyobinafsishwa ili kujionea hali halisi ya utendaji wake maana kuna baadhi vimekiuka kabisa ili dhana na masharti waliyopewa wakati wa zoezi hilo la ubinafsishaji matumizi ya eneo lililobinafsishwa. Hivyo kipitia Tume, hiyo Serikali ivibainishe na kuvichukua viwanda vyote ambavyo havijaendelezwa na kuwapa wawekezaji wengine ili kufikia lengo la Serikali kuelekea Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, kuondoa tozo za kuhifadhi Maiti katika Hospitali zetu za Serikali maana imekuwa kero kwa wafiwa na wakati mwingine hushindwa kulipa na kupelekea Serikali kuchukua jukumu la kuzika. Hivyo naishauri Serikali huduma ya kuhifadhi maiti katika hospitali zetu za Serikali iwe bila gharama (bure).

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, igawe taulo za kike bure katika shule za msingi na sekondari na pia kurudisha Corporate Income Tax kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato na kubakia 30%, ile ile na kusimamia muuzaji wa mwisho kupunguza bei ya taulo hizo ili kila mwanamke kuanzia mijini na vijijini wawe na uwezo wa kununua na kutumia, kuepusha kutumia bidhaa zisizofaa katika kujisitiri wakati wa hedhi na hii njia huleta maambukizi ya magonjwa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, namwomba Mwenyezi Mungu ampe afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake ili waweze kuyatekeleza majukumu yao ya kila siku.