Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa mahali hapa na kupata nafsi hii muhimu kabisa ya kuchangia Hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020. Hotuba hii inakwenda kuhitimisha bajeti kuu ya Serikali katika mipango mbalimbali na mikakati, aidha, bajeti hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kama ilivyoelekeza. Halikadhalika nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kuipongeza Serikali kwa kuandaa hotuba nzuri, inayokwenda kutupatia mwelekeo wenye tija kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa pongezi nyingi kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi kubwa ya kusimamia wanyonge kupinga ufisadi kuhakikisha maliasili zote zinainufaisha nchi na watu wake ili kuleta maendeleo kwa Taifa, katika bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali imetuambia ilitarajia kupata jumla ya shilingi trilioni 32.48 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Aidha, mchanganuo wa mapato yaliyopatikana hadi Aprili, 2019 ikilinganishwa na lengo la kipindi hicho ni kama Serikali ilivyoainisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapato yasiyo ya kodi yalifikia shilingi trilioni 2.04 sawa na asilimia 122 ya lengo. Mapato yasiyo ya kodi yalivuka lengo kutokana na kuimarika kwa matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa maduhuli kwenye taasisi za Serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa Serikali wa ukusanyaji wa mapato (Government electronic payment Gateway –GEPG); mapato ya Halmashauri yalifikia shilingi bilioni 529.25, sawa na asilimia 72 ya lengo; misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ilifikia shilingi trilioni 1.70 sawa na asilimia 86 ya lengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ilifikia shilingi trilioni 3.3, sawa na asilimia 57.4 ya lengo; na mikopo ya masharti ya kibiashara ya nje ilifikia shilingi bilioni 692.3, hizi ni hatua nzuri zilizofikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhakikisha kila lengo lililopangwa linatimia kwa wakati na kulifanya Taifa lisonge mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika Serikali imetueleza namna ilivyoshindwa kwa baadhi ya maeneo kutofikiwa kwa malengo ya mapato ya kodi kulitokana na sababu mbalimbali zikiwemo ugumu wa kutoza kodi sekta isiyo rasmi, kuendelea kuwepo kwa upotevu wa mapato kunakosababishwa na tatizo la magendo hususani kupitia bandari bubu kwenye mwambao mrefu wa Bahari ya Hindi na mwamko mdogo wa wananchi kudai risiti za kieletroniki wanapofanya manunuzi au baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutotoa risiti wanapofanya mauzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali katika changamoto hii, kutotoa risiti ama kwa wananchi kutokudai risiti ni jambo ambalo linahitaji muda kuweza kulitatua. Kwanza elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi ili wajue ni wajibu wao kudai risiti, wasipodai risiti wanapoteza mapato ya Serikali na hivyo kupelekea kwa baadhi ya miradi ya maendeleo kutokukamilika hasa katika huduma za kijamii ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja. Vilevile Serikali ianzishe sasa kutoka elimu ya wajibu wa kulipa kodi tangu shule za msingi ili kutengeneza kizazi kijacho chenye kutambua umuhimu wa ulipaji kodi, msingi huu utasaidia sana kwa mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Watumishi wa TRA wana wajibu wa kutoa elimu kwa walipa kodi na kutokutumia vitisho pale wanapokusanya kodi. Imejengeka hali ya uoga na vitisho kati ya mlipakodi na mkusanya kodi kwa baadhi ya watumishi hawa kujenga mianya ya rushwa na kupelekea kwa baadhi ya wafanyabiashara kufunga hata biashara zao kwa kuona kodi wanazodaiwa ni kubwa kuzidi mitaji ya biashara zao. Vilevile naishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuzirasimisha bandari bubu ili sasa zitambulike na kukomesha uhalifu unaofanyika huko, kuzirasimisha bandari hizo kutasaidia Serikali kupata kodi ambayo sasa wanaikosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto ya muda mrefu ya malimbikizo ya madai mbalimbali ya Wazabuni, Watumishi wa Serikali na kadhalika kuidai Serikali. Changamoto hiyo pia imewakumba baadhi ya watumishi wa Serikali Jimboni Kibaha Vijijini hasa katika Sekta ya Elimu kuwa na madai ya muda mrefu, lakini Mheshimiwa Waziri ametuambia Serikali imeendelea kuhakiki na kulipa madeni ya wazabuni, makandarasi na watumishi ambapo hadi Mei, 2019 kiasi cha shilingi bilioni 598.4 kimelipwa kati ya bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 600.0 kwa mwaka 2018/2019. Kati ya kiasi kilicholipwa shilingi bilioni 300.5 ni kwa ajili ya Wakandarasi, shilingi bilioni 232.9 ni kwa ajili ya watoa huduma na shilingi bilioni 65.0 ni kwa ajili ya Watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha tumeelezwa kuwa, Serikali imelipa malimbikizo ya kimshahara ya Watumishi 790 waliostaafu kabla hawajalipwa, ambapo hadi Aprili, 2019, jumla ya shilingi bilioni 3.10 zililipwa, ni hatua nzuri sana, lakini bado changamoto ipo ukilinganisha na hali halisi, malimbikizo haya yanapolipwa ama kwa wazabuni, watumishi basi yanakwenda kusaidia sana katika kukuza uchumi wa watu kwani fedha hizo zinakwenda kuingia kwenye mzunguko na hivyo kusaidia hali ya uchumi wa chini, kati kuwa katika hali nafuu. Naishauri Serikali kuongeza kiwango cha kulipa malimbikizo hayo ili kuleta nafuu kwa wadai na wategemezi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wanaouza kwa rejereja bidhaa mbalimbali baada ya kufanikisha kuzinunua kwa wazalishaji wakubwa kwa maana ya viwanda wamekuwa wakitozwa kodi, ni jambo jema sana kwani kodi ndio msingi wa maendeleo katika Taifa lolote lile duniani, lakini sasa naomba kuishauri Serikali kuanza kutumia aina tofauti ya ukusanyaji wa mapato ambayo kwa kiasi kikubwa itawaondolea wenzetu wa TRA usumbufu wanaoupata katika kukusanya kodi kwa wafanyabiashara wa mwisho, kwa maana wale wanaouza kwa rejareja, Serikali iweke mfumo maalum wa TRA wa kukusanya mapato kwa pamoja hasa katika vyanzo vya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, mfano Viwanda vya Mabati, Nondo, Saruji, Vinywaji mbalimbali, Viwanda vya Sukari na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huo uwe unakata kodi zote mpaka ya mfanyabiashara wa mwisho kwa maana ya wale wanaofanya kwa rejareja, kwa maana hiyo mfanyabiashara huyu wa rejareja anapokwenda kuchukua bidhaa kwa mzalishaji mkubwa (Kiwanda) anauziwa bidhaa anazohitaji kwa bei ambayo itakuwa imejumuisha kodi zote pamoja na kodi ambayo kwa sasa wafanyabiashara wa mwisho wanakatwa. Hatua hii itakwenda kusaidia zaidi watu wa TRA kwa kupata kodi yao kwa uhakika bila kusumbuana kama ilivyo sasa, tunaona namna ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara wa mwisho (rejareja) unavyosuasua kwa namna ya elimu ama wengine kutokutoa risiti kwa kila bidhaa wanayoiuza. Vilevile hatua hii itapunguza nguvu kubwa inayotumia Serikali katika kukusanya kodi kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu mwingine kwa Serikali, ni kuanzisha mikoa ya kikodi kwa Sekta nzima ya Maliasili na Utalii, mikoa hiyo ya kikodi kazi yake ni kukusanya kodi zote husika zinazotokana na maliasili na utalii, mfano katika sekta nzima ya utalii, kuna mahoteli, vivutio vya utalii na mambo mengine mbalimbali yanayohusiana na sekta nzima ya utalii, Serikali ikifanya hivyo itakwenda kusaidia sana ukusanyaji wa kodi katika sekta nzima ya utalii na kuepusha ukwepaji wowote ambao kwa namna moja au nyingine kwa baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakikwepa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wetu wa kukusanya kodi ni mzuri sana, napenda kuipongeza tena Serikali kwa jitihada inazofanya katika kukusanya kodi, lakini tuna changamoto moja na muda mrefu ambayo imekuwa ikilalamikiwa na Watanzania walio wengi, ni tozo kubwa za kodi zinazotozwa bandari kwa vifaa mbalimbali, mfano, vyombo kama magari, bei ya kununulia nje ya nchi kama Dubai, Japan na kwingineko ni kiasi cha wastani, lakini ukileta hapa nchini, tozo ya kodi ya kutolea gari hiyo inakuwa mara tatu na bei ya chombo halisi, haileti maana hasa ukizingatia bei ya chombo husika iko wazi na inajulikana, najiuliza kwa nini tozo inakuwa kubwa kuliko bei halisi ya manunuzi? Naishauri Serikali kuanza utozaji mkubwa wa tozo za kodi kwa bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini kwa maana viwanda vyake vipo hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kuagiza nje ya nchi bidhaa zinazozalishwa nchini ni kuua viwanda vya ndani, kufanya hivyo kutasaidia sana kuviinua viwanda vyetu vya ndani, aidha kwa bidhaa zozote ambazo hazizalishwi hapa nchini, basi Serikali naiomba ichukue ushauri wangu wa kupunguza kodi ili sasa Watanzania waweze kumudu kuagiza vitu mbalimbali, hasa magari kwani ndio tozo zake zimekuwa zikilalamikiwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na kukua kwa miji mbalimbali hapa nchini kwetu, hali hiyo imetupata pia watu wa Kibaha Vijijini, kwani sasa mji unazidi kukua kwa kasi sana na huduma mbalimbali muhimu zinapatikana, idara mbalimbali nazo zinapatikana, mfano Idara ya Maji, tuna ofisi ya Halmashauri pamoja na Jeshi letu la Polisi kwa kituo chetu kupandishwa hadhi, naiomba Serikali sasa kutokana na hayo yote niliyoyataja na mengine mengi yenye kutupa hadhi wana Kibaha Vijijini kuwa na sifa zote, Serikali sasa ni wakati wa kuja kufungua Ofisi za TRA, Kibaha Vijijini, kufunguliwa kwa Ofisi ya TRA kutasaidia kwa kiasi kikubwa kusogea kwa huduma hiyo karibu na wananchi, na pia kutasaidia kwa Serikali kukusanya kodi zake kwa urahisi na kugundua changamoto mbalimbali na kuzifanyia kazi kwa uboreshaji zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua ya kufuta ada hiyo, ilikuwa kero kubwa kwa wananchi ililinganishwa na hali halisi ya uhaba wa maji na changamoto mbalimbali katika sekta ya maji ambazo ni za muda mrefu. Changamoto hizo zimepelekea wananchi kwa gharama zao wenyewe kuamua kujichimbia visima vyao ili kupata maji kwa matumizi ya nyumbani, lakini wakakumbana na kikwazo cha kulipia kodi, kikwazo hicho sasa kimeondolewa, pongezi tena kwa Serikali, hivyo nawasihi wananchi mbalimbali wenye uwezo kuendelea kuchimba visima kwa kufuata taratibu zilizopo kisheria na kujipatia maji. Hata hivyo, nazishauri Bodi za Maji za Mabonde kuendelea kufuatilia visima vyote ili kuwa na idadi kamili na kuepuka uchimbaji holela unaoweza kujitokeza kwa namna yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.