Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi nipate kuchangia. nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Watendaji wengine wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ya kutengeneza na kuandaa bajeti hii ambayo tumepewa na tumeisoma, tumeisoma, tumeipitia, ni bajeti nzuri ambayo Wananchi wetu wengi walioko huko kwenye maeneo yetu wanaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niungane na Waziri wa Fedha kuipongeza Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya ya kumsaidia Waziri, kumshauri, kuhakikisha kwamba, anaandaa kitabu hiki ambacho cha bajeti ambacho kimekuwa na maneno mazuri na maandalizi mazuri ambayo yanaeleweka. Nilikuwa naomba tu labda ninukuu maneno ambayo aliyasema Mheshimiwa Waziri, ili kusudi Spika nae aweze kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema kwamba, Kamati hii ya Bajeti imetoa mchango mkubwa sana katika kuboresha sera za uchumi na bajeti kuliko Watanzania wengi wanavyofahamu. Amesema, kusema kweli wanastahili kutambulika kipekee, kama kuna nishani na au tunzo ya Spika kwa kamati hii ya Bunge inayojitanabahisha kwa utumishi uliotukuka basi, kama itakupendeza Mheshimiwa Spika napendekeza iwe kamati ya kwanza kutunukiwa heshima hiyo. Haijapata kutokea katika bajeti zote tulipoanza toka 2015 huyu Mheshimiwa Waziri kuzungumza maneno haya maana yake kamati hii imefanya kazi kubwa mno ya kumsaidia kwa hiyo, ni vizuri Spika nae sasa akaliona hili basi akalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Waziri amezungumzia hapa katika ukurasa wa 16 mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2015. Amezungumza pale, ukiangalia na nimewasikia wenzangu wanasema kwamba, habari ya kwamba, bajeti hii ni ya vitu sio watu, lakini ukiangalia alivyoiandika katika utekelezaji huu ambao amefanya katika kipindi kilichopita anasema ujenzi wa reli ya kati kiwango cha Standard Gauge maana yake unafanyika; hii maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, si ya vitu tu ni pamoja na ya watu kwa sababu watapanda watu. Amezungumzia suala la ufufuaji wa shirika la ndege ambapo sasa tuna ndege Bombadier, wanapanda watu. Amezungumzia ujenzi wa jengo la tatu, terminal three, miundombinu yake katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Julius Nyerere kimekamilika, kinatumiwa na watu. Amezungumzia barabara kuu za mikoa kiwango cha lami, kwenye barabara anapita nani? Si wanapita watu kwa hiyo, ni vitu vya ajabu watu wanapozungumzia kwamba, hii ni bajeti ya vitu sio watu. Ni bajeti ya vitu na watu, nilikuwa naomba sana tafsiri yake basi wenzetu wawe wanaielewa kwamba, bajeti hii ni ya vitu pamoja na watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali yangu kwa umeme wa REA. Kwamba, nchi nzima sasa hivi namsikia Waziri anakimbizana huku na huku anazungumzia masuala ya umeme wa REA. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa kwa kuwa, tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda kwa maana pale Korogwe nina wawekezaji wa viwanda kama wawili wanapata tatizo la kupata umeme. Gharama za umeme wanazotajiwa ni kubwa kiasi kwamba, inawakatisha tamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kiwanda cha matunda ambacho kinatakiwa kuanzishwa pale wameandika kuomba umeme, gharama waliyopelekewa yaani yule mzungu amebaki sasa anashangaa. Ni vizuri viwango vya umeme kama wanaomba wawekezaji wawekewe kiwango ambacho akishaweka maana yake si atakuwa ananunua huo umeme, tusiwakatishe tamaa. Kwa hiyo, tunahitaji kuwa na viwanda, lakini vilevile tunahitaji kuwa na umeme ambao wananchi wetu hawa wawekezaji wakiwekewa unafuu wanaweza wakawekeza na sisi tunahitaji hivyo viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Serikali yangu kwamba, bajeti hii, mpango huu wa bajeti ambao umeweka maeneo ya vipaumbele wa 2019/20 niombe basi Serikali yangu sasa angalau kwa mwaka huu mnaonaje kama fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya hivi vipaumbele tulivyoviweka tukahakikisha kwamba, fedha yote inapatikana itakapokuwa imekusanywa ikapelekwa kwenye hivi vipaumbele, ili tuweze kujipima katika mwaka mzima kwamba, tumeweka vipaumbele hivi je, tumefikia wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuliko tunavyofanya kipindi hiki cha miaka mitatu huku nyuma tumetenga bajeti haifikii kile kiwango ambacho tumejiwekea. Nilikuwa naomba ili tuweze kujipima basi bajeti ambayo tumetenga kwenye hivi vipaumbele itolewe yote ili sasa tuweze kujipima kwamba, sasa tumefikia wapi katika mpango mzima wa vipaumbele ambavyo tutakuwa tumejiwekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru tena kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja. Asante sana. (Makofi)