Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu muweza wa yote aliyenipa fursa hii ya kuweza kusimama na kuweza kuzungumza jioni hii katika Bunge lako Tukufu. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja hii iliyo mbele yetu hoja ambayo ni muhimu kwa ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono na sababu ninazo. Sababu ya kwanza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wote na timu yake yote ya Wizara ya Fedha na Watendaji wote na Mawaziri na Serikali chini ya uongozi wa mpendwa wetu Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wamefanya kazi nzuri katika bajeti iliyopita. Nimejaribu kupitia vitabu vyote hivi, nimeanzia na kitabu cha hotuba ya Waziri, nimepitia Taarifa ya Hali ya Uchumi katika Taifa, nimepitia kitabu cha Mpango wa Utekelezaji wa Bajeti, wanyonge wanyongeni haki yao wapewe kazi wamefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono bajeti hii kwa sababu hata bajeti iliyopita kwa kiwango kikubwa ilijielekeza katika miradi ya kufufua uchumi wa Taifa letu. Huwezi kusema unataka kufikia uchumi wa kati bila kuwa na reli yenye viwango vya kimataifa, huwezi kusema unafikia uchumi wa kimataifa bila kuwa na ndege za kutosha kwa ajili ya utalii na kwa ajili ya uchumi. Huwezi kufikia viwango vya kimataifa bila kuwa na umeme wa uhakika, bila kuwa na kilimo chenye tija, hizo ndizo sababu zangu za kuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono kwa sababu Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2019/2020, umelenga kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na umelenga kwenda kutekeleza malengo endelevu. Katika yale malengo endelevu yote Serikali ya Tanzania imeweka vipaumbele tisa na vyote vipo katika mpango, sina kila sababu ya kuunga mkono bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono kwa sababu kero zote zilizokuwa ni kero kwa ajili ya uchumi wa Taifa letu zimeondolewa, Mungu atupe nini, ninaunga mkono. Ninaunga mkono bajeti hii kwa sababu vipaumbele vyote vilivyowekwa vinalenga utashi wa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania. Ukienda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa 16 umejieleza vema, Mheshimiwa Rais alipoingia alituonesha kabisa anataka kuingia kwenye uchumi wa kati na bajeti hii imezingatia matakwa ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze katika mambo machache na leo nimechagua kwa sababu Wabunge wengi wameshaongea kabisa wiki nzima hii mengi wameshayagusia. Leo nimeona nijielekeze katika maeneo yanayogusa wananchi walinichagua na si wengine ni wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa kweli katika kuchangia pato la Taifa wao ndiyo wanaoongoza katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo taarifa zinaonesha uchumi wa Taifa letu kwa kiwango kikubwa pia unategemea kilimo. Wazalishaji kati ya asilimia 65 wanawake ni zaidi ya asilimia 80 wanalima na kwa bahati mbaya wanalima kwa kilimo cha mkono. Wanawake wa Tanzania ndiyo tunaotegemea katika kilimo hata akina baba watanisapoti, ukipita huko vijijini watu unaowakuta kwenye mashamba ni wanawake na watoto wao wa kike. Akina baba walio wengi wanalima lakini si kwa kiwango cha wanawake. Nikitolea Mkoa wetu wa Mara na hasa walaya ninayotoka wanawake ndiyo wanaolisha hata familia, wanawake ndiyo wanaolea familia, wanawake ndiyo wanaoleta uchumi wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo nimeona nijielekeze kuwasemea katika kilimo na hapa ndipo waliponituma. Kilimo chao bado kinategemea jembe la mkono, kilimo chao bado kinategemea kilimo kisichokuwa na utaalam, kilimo chao bado kinategemea kutokuwa na pembejeo za kutosha, kilimo chao bado hata kupata fursa zenyewe za kupata mikopo kwa ajili ya kununua pembejeo bado, kilimo chao hata mazao wanayolima bado kuwa na uhakika wa masoko bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona leo nije niishauri Serikali, kama kweli tunataka kufika uchumi wa viwanda na kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati ninaishauri Serikali yangu tukufu hebu tuwekeze kwenye kilimo. Hapa ninatoa ushauri kwamba ni lazima Serikali katika bajeti hii na hata katika bajeti zijazo tujielekeze kuimarisha kilimo chetu na katika vipaumbele vyetu kama ambavyo bajeti imesema, tuongeze wigo wa kilimo cha umwagiliaji. Tanzania ina hekta nyingi sana za kilimo, zaidi ya 4,000 lakini zinazofanyiwa kilimo ni chache sana. Mpango wa Wizara ya Maji kwa mwaka uliopita walielekeza wanataka tufikie hekta 1,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba Serikali iharakishe hii mipango ili twende kwenye kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kujikomboa kiuchumi kama bado tunaendelea kutegemea kilimo cha mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya mikoa, kwa mfano hii Kanda ya Kati ya Dodoma hata ufanyeje, kuna Wilaya kama ya Kongwa hata ukilima mazao kama ya mahindi hayaoti. Ukienda Mkoani kwetu Mara sasahivi ardhi imechoka. Sasa tunayo maziwa, mito, maji ya mvua na mpaka hatuna hata mabwawa. Ninaishauri Serikali hebu sasa tutafute fedha kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo ili sasa uchumi wetu huu tunaouzungumza kwamba umekuwa kwa kiwango cha asilimia 7.5 sasa uende hata kumnufaisha mwananchi ili naye aone matokeo ya kukua kwa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee uwezeshaji wa wanawake kiuhumi. Ninaipongeza Seriakli yetu ya Chama cha Mapinduzi, imekuwa mstari wa mbele kuwawezesha wanawake. Kama ambavyo nimetangulia kusema, mwanamke ndiye kila kitu, ukimuwezesha mwanamke ni sawasawa na kuliwezesha taifa. Ni ukweli usiopingika kwamba mapato anayoyapata mwanamke kwa kiwango cha asilimia zaidi ya 90 kinakwenda kwenye familia. Ninaposema hivi ninao ushahidi kwa sababu akina baba matumizi yao ni mengi, lakini hakuna mama anayeweza akaishi vizuri bila kuhakikisha mtoto wake anasoma bila kuhakikisha malezi ya mtoto. Hawa akina baba wakipata hela zinakuwa na matumizi mengi lakini akina mama akikipata vyote vinakwenda kwenye familia. Kwa hiyo ninashauri hapa, hebu tuwawezeshe wanawake kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 tulitengeneza hapa sheria ambayo inaitaka Serikali kila palipo na jambo lolote la manunuzi, kila mahali ambapo wanatengeneza tender, iwe ni kujenga barabara, reli na kufanya kila kitu katika miradi ya maendeleo asilimia 70 wanaopata hiyo kazi au wanaopata hiyo zabuni au wanaopata hiyo tender wawe ni wanawake. Ninafurahia mpango huo na ninaipongeza sana Serikali yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kufanya utafiti, baadi ya taasisi zetu za Serikali hazitekelezi. kKwa hiyo ningependa kujua Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa hebu tuambie, tangu tumepitisha sheria hii mpaka sasa ni wanawake wangapi wananufaika? Na kama hawanufaiki Serikali ina mkakati gani? Kwa sababu baadhi ya miradi ni mikubwa, kwa mfano mradi wa ujenzi wa Stiegler’s Gorge, mradi wa reli na miradi mingine hata ya kununua ndege wanawake wananufaikaje? Tujue! Hata hivyo, hata huko kwenye kilimo hata kwenye miradi mingine ya ujenzi wa madarasa, n.k tujue wanawake wananufaikaje. Tunapoagiza vitu kutoka nje ya nchi wanawake kwenye asilimia 30 wananufaikaje. Hapa nitaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuaj hebu tusaidie kuainisha ili baadaye sisi kama Bunge tupime, isije baadaye sheria hiyo nayo ikaja ikaondolewa kwa sababu tumeshindwa kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naona wenzangu walikuwa wanapiga kelele juu ya mambo ya taulo za kike. Taulo za kike tulijichelewesha wenyewe, tulifanya uzembe, sisi wenyewe Wabunge hatukuwa serious, matokeo yake mpaka imeondoka. Sasa na kwenye hili naomba tusiwe wazembe, hii asilimia 30 tunasemaje katika kuhakikisha inanufaisha wanawake?…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. AMINA S. MAKILAGI: Nitaleta kwa maandishi ikiwemo pamoja na taulo za kike nimetoa ushauri wangu, nimezungumzia juu ya asilimia tano ya wanawake, vijana na walemavu na nimezungumzia pia utaratibu wa utoaji wa uboreshaji wa mapato ya kodi. Nitaleta kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)