Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kushukuru Mungu kupata nafasi hii lakini pili nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu ambaye kimsingi anatenda vizuri sana na Waheshimiwa Mawaziri wake hasa Waziri Mpango na Naibu wake, mtani wangu, Naibu Waziri wa Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, usiposema ukweli hautajulikana. Miradi hii ambayo nimeisoma hapa katika hali hii ya uchumi na imeelezwa vizuri sana na Mheshimiwa Waziri. Naomba tu leo nisome mistari ya Biblia kutoka Yohana 20:27, inasema: “Kisha akamwambia Tomaso, leta hapa kidole chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye”. Haya ni maneno ya Yesu mwenyewe wakati anawaeleza Mitume wake ambao hawakuamini mambo ambayo yalikuwa yanatendeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mpango maneno haya yampe faraja huko anakoelekea maana ni vigumu sana kwa wengine kueleza habari ya Stigler’s, SGR au ndege. Hii ni miradi ya kimkakati ambayo imesemwa na nchi hii ili kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati, hali hii isipokuwepo namna gani tutaendelea? Kwa hiyo, mimi nikupongeze naendelea hivyo hivyo. Najua wengine watakwambia acha hii, watabeza sana lakini maneno haya ya Biblia kutoka Yohana yaendelee kukutia moyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukupa moyo sasa nijielekeze kwenye kilimo. Kwa kweli nipongeze walau kwa namna fulani mwaka huu imeonyeshwa jinsi ambavyo tutaelekea kwenye eneo hili la kilimo. Asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanategemea sana kilimo na ukiangalia imeanza kupanda kutoka asilimia tatu kwenda asilimia nne. Sasa basi ni vyema tukaelekeza mipangilio yetu katika eneo hili la kilimo kwa sababu ukiangalia ipo miradi mingi ambayo inatekelezwa hasa masuala ya mabwawa ambapo mengine yamefanya kazi lakini mengine bado.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kulingana na nchi yetu hatuna mvua za kila mara, mvua zetu zinahesabika ni wakati wa masika, tukiwekeza katika mabwawa kilimo chetu kitakuwa na uhakika kwa sababu tutanyeshea wakati mvua hakuna. Kwa maana hiyo basi, Serikali ikijielekeza katika kujenga mabwawa mengi ni wazi kwamba baadaye wakulima wetu wanaweza kuendelea kulima kilimo cha kumwagilia ambacho kina uhakika wa kupata maji na hivyo tukaweza kusonga mbele zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule jimboni nina bwawa moja ambalo kimsingi lina shilingi bilioni moja lakini bado halijakamilika linahitaji shilingi milioni mia nne (400) tu. Kwa msingi huu, kama Serikali ikijelekeza moja kwa moja katika eneo hili la mabwawa ikamalizia mabwawa yote ambayo imeshaamua kuyajenga basi asilimia tatu kwenda nne itakuwa tano kwenda sita. Kwa hiyo, naomba sana Serikali ijielekeze upande huu kwa sababu ndiyo maeneo ambayo ukigusa utakuwa umesaidia pia katika eneo hili la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli nishukuru sana Serikali na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa eneo hili la afya. Kwa eneo la afya mambo yameenda vizuri hata kama siyo kwa asilimia 100, vituo vya afya na hospitali zimejengwa lakini niombe sasa tujielekeze katika vifaa tiba. Tukishapata vifaa tiba Tanzania itakuwa imesaidika sana kwani Watanzania watapata afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, tuongeze pia watumishi, wafanyakazi wakishapatikana kwenye maeneo haya basi Tanzania tutasonga mbele. Sehemu ambayo ina mkosi yaani inasababisha kushuka kwa uchumi wa kawaida wa mtu mmoja kule vijijini ni habari ya afya kwa sababu ni ghali lakini tukijielekeza kwenye vifaa tiba na watumishi Tanzania itakwenda mbele sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nataka kusemea habari ya miradi ya maji, tunajua wazi kwamba miradi ya maji tumeiahidi kwenye ilani ya Uchaguzi na kwa maeneo mengi imetekelezwa lakini yako maeneo machache ambayo kimsingi utakumbuka wakati wa kampeni tulisema tunamtua mama ndoo kichwani. Hii inawezekana ikiwa tu pale ambako miradi hii itatembelewa kwa ukaribu sana na Watendaji wa Serikali. Iko miradi mingine imekaa kwa muda mrefu na hata kwenye jimbo langu lipo na iko mingi lakini tukielekeza maeneo haya tukaweka usimamizi wa kutosha ni wazi miradi hii itakwisha na Tanzania wananchi watapata maji na asilimia ambayo inaonekana hapa itaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalopenda kusema ni habari ya mgawanyo wa TARURA na TANROADS kwa 30% kwa 70%. Niombe, ipandisheni asilimia hii kutoka 30 kwenda hata 40% au 50% ili walau barabara za vijijini zikaweza kupitika na baadaye malighafi kwa sababu inatoka vijijini iweze kufika mjini. Tukifanya hivyo basi ni wazi kwamba uchumi wa Tanzania utapanda na hali kadhalika barabara zetu zitakwenda mbele. Mheshimiwa Mpango nikuombe sasa, kuna barabara ya Mbulu – Haydom – Sibiti; hii kwa kweli mara nyingi nimejaribu kuisema nimeiomba kweli kweli, nimeona mambo yameshakuwa mazuri, imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, imeanza kuwekewa fedha, mwaka huu nikuombe ionekane walau kwenye mipango yako basi. Ikiwekewa fedha na katika hali hiyo ukituwekea fedha bwana utakuwa umefufua eneo ambalo kwa kweli kwa uchumi wa Kanda yetu kule utakuwa umefungua sana na nina hakika katika hali hiyo mambo yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ajili ya elimu bure. Eneo hili la elimu bure hata kama hauoni kwa macho hakika sasa hivi ukiangalia wanafunzi au watoto wengi wameandikishwa shuleni wengi sana. Hebu fikiri kama Mheshimiwa Rais asinge support hii elimu kuwa bure watoto wangapi wangebaki kule vijijini hawana namna ya kujitosa katika elimu. Kwa hiyo ukiangalia kiwango kile cha watoto waliojiandikisha mwaka wa awali, ni wazi kwamba tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa sababu amefanya kazi kubwa sana. Na hii ndugu zangu wapendwa kama hamuoni mtaona wapi? Ni vema tukawapongeza pia Serikali hii, kwa kweli Rais huyu ameamua kufanya kweli na hii kweli yake tumpe big up sana na iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa kweli nielezee habari ya REA, ukweli ni kwamba Serikali inafanya vizuri kwa upande wa REA. Kwa kweli katika hali hii Tanzania itakwenda mbele, sisi vijijini sasa hivi tunapata umeme ni wazi kwamba tuipongeze na kuisaidia Serikali yetu iweze kwenda mbele zaidi. Zipo changamoto chache, kuna maeneo machache tu ambako REA haikufika wakandarasi wanakosa fedha, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango elekeza mipango hii pale ili REA nao iende mbele zaidi vijiji viwe vingi na hatimaye pawe na kile kinachoitwa ujazilizo katika maeneo yetu. Maana yake maeneo ya vijijini sasa hivi kwa bahati mbaya sana imefika kwenye maeneo ya Kata tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri pamoja na mipango hii ikielekea na namna hii kufika mwaka 2020/ 2021 tutakuwa tumefika maeneo mengi sana na wananchi watakuwa wamepata umeme. Leo hii Television zinaonekana vijijini jambo ambalo kwa miaka iliyopita ilikuwa hakuna, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais nakuombea Mungu akubariki sana uendelee mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana ahsante sana kwa mchango naunga mkono hoja.