Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Alex Raphael Gashaza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti kuu ya Serikali na hali ya uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nichukue nafasi hii kuwapongeza viongozi wetu; Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mipango, Naibu Waziri, Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Mlinga alipokuwa akichangia alijaribu kuonyesha jinsi ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inavyofanya kazi katika kutekeleza Ilani. Wenzetu walijinasibu kwamba hiyo ni Ilani yao lakini naomba niwarejeshe kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, kuanzia ukurasa ule wa 36 – 80, kwa maana ya Sura ya Tatu inaeleza jinsi ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi itaenda kuboresha huduma na miundombinu ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara, reli, kuimarisha huduma za usafiri wa anga na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza Ilani ya Uchaguzi. Kama walivyosema kwamba walichokifanya ilikuwa ni ku-copy na ku-paste mtakumbuka wakati wa uzinduzi wa kampeni mwaka 2015, walisema kwamba Ilani yao wananchi wataikuta kwenye website, hawakuwa na Ilani mezani. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MHE. ALEX R. GASHAZA: Kwa hiyo, nimeona hili niliweke wazi ili kujua kwamba tunatekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015-2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba ifikapo 2025 tunafikia uchumi wa kati. Ili tuweze kufikia uchumi wa kati, ni lazima kujikita kuwekeza katika sekta nyeti ambazo zitatufanya tuweze kutoa ajira kwa wingi pia tuweze kukuza kipato cha Taifa na cha mtu mmoja mmoja. Lazima tuwekeze kwenye sekta ya kilimo kwa sababu hakuna namna ambavyo tunaweza tukawa na uchumi wa viwanda kama hatujawa na uwekezaji mzuri kwenye sekta ya kilimo, hatujatengeneza mazingira rafiki ya kufanya biashara, hatujaweza kuwa na vyanzo vya mitaji kwa maana ya kuwa na mikopo ya bei nafuu. Kwa hiyo, nipongeze Serikali kwamba katika mpango wake wa bajeti hii ya 2019/2020 wamejaribu kuangalia maeneo yote hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba katika sekta ya kilimo tumefanya vizuri kwa maana ya kwamba ni miongoni mwa sekta ambazo zimechangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 28.2 lakini bado unaweza ukaona kwamba tuna fursa kubwa ya kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hii ya kilimo kwa sababu yapo maeneo ambayo tulitakiwa tuweze kuyafanyia kazi hususani eneo la umwagiliaji ni asilimia isiyozidi 6 tu kwenye maeneo yanayofaa kwa ajili ya umwagiliaji ambayo tumeweza kufanya. Kwa hiyo, bado tunayo nafasi, ukizingatia kwamba kuna mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri hali ya upatikanaji wa mvua na hali ya ardhi ni vizuri sasa tukajikita kwenye kilimo cha umwagiliaji ili maeneo haya yaliyobaki takribani hekta karibu 20,000 zinazofaa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji tujikite huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kuendelea lazima pia tuwe na Taifa ambalo limeendelea na ili tuweze kuendelea lazima tuwekeze kwenye elimu, hususani elimu ile ambayo itamwezesha pia mtu mmoja mmoja kuweza kujiajiri. Leo tunaona jinsi ambavyo vijana wanamaliza chuo kikuu na kushindwa kujiajiri. Najua kwamba katika michepuo tunayoenda nayo sasa ya masomo ya sayansi, kilimo na biashara lakini nishauri kwamba katika kuboresha elimu tujikite pia katika vocational training kwa maana ya kuboresha na kupanua wigo wa kuwa na vyuo vya VETA. Pamoja na kwamba Serikali imeweza kuonyesha jitihada na kuboresha vyuo vya FDC’s kwa maana ya vyuo vya maendeleo ya Taifa takribani 54 lakini bado havitoshelezi. Kwa hiyo, nashauri kwamba tuendelee kupanua wigo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata katika masomo yale ya kawaida kwenye zile taasisi ambazo ni za sanaa na sayansi, kwa sababu tunalenga kutengeneza elimu ambayo itamfanya mwananchi au vijana wetu waweze kujiajiri basi tuone uwezekano wa kuingiza somo la entrepreneurship katika kila tahasusi. Kwa mfano, badala ya masomo ya sanaa kwa maana ya HGL, HGK unaweza ukasema HEL au HEG, hizi tahasusi zipo katika nchi za East Africa Community kwa mfano Rwanda, Uganda na Kenya. Masomo haya yanawasaidia angalau anayemaliza kidato cha nne, kidato cha sita hata chuo kikuu kuwa na basic ya somo la entrepreneurship ambalo litamfanya aweze kupambana na hali yake anapokuwa akisubiri suala la ajira anaweza akajiajiri mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa miundombinu, miundombinu ya barabara na reli ni muhimu sana kwa ajili ya kuongeza au kuinua uchumi wa Tanzania. Nipongeze kwa jitihada za kuanza ujenzi wa reli ya Standard Gauge ambayo itatoka Dar es Salaam kuja Isaka na matawi yake kwenda Tabora – Msongati - Mwanza pia kwenda Keza - Kigali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reli hii ni muhimu hususani katika eneo la Ngara ambapo kuna deposit kubwa nickel, kama reli hii ikijengwa na mgodi wa Nickel ukaweza kuanza utaweza kufanya reli hii iwe na tija kwa sababu mzigo utakaosafirishwa ni mkubwa na ambao unaweza ukasaidia katika kuhakikisha kwamba deni ambalo tunakuwa tumekopa kwa ajili ya ujenzi wa reli hii basi liweze kurudishwa kwa haraka kutokana na biashara ambayo tutakuwa tukiifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye upande wa feeder roads ambazo ziko chini ya TARURA, barabara hizi ni muhimu. Tunajua kwamba tunapowekeza kwenye kilimo, maeneo ya kilimo yako vijijini na ambako tunahitaji barabara safi na bora kwa ajili ya usafirishaji wa mazao kuyapeleka sokoni. Kwa hiyo, niombe kwamba katika maeneo ya Halmashauri zetu TARURA iweze kusimamia na kuangalia barabara ambazo ni za kipaumbele kwa kushirikiana na Halmashauri zetu ili kusudi barabara hizi ziweze kuboreshwa na hatimaye wananchi waweze kunufaika na uwekezaji katika barabara hizi kwa ajili ya kusafirisha mazao yao kupeleka sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata soko la mazao yao yameanzishwa masoko ya mipakani. Ngara ni miongoni mwa Wilaya ambayo iko mpakani mwa Rwanda na Burundi na lipo soko ambalo lilianzishwa la mpakani la Nzaza tangu mwaka 2013 lilipoanzishwa mpaka leo bado halijakamilika. Tunaomba miradi hii ambayo imeanzishwa kimkakati kwa lengo la kutengeneza masoko ya ndani basi iweze kukamilika ili wananchi waweze kupata maeneo ya kuweza kuuza biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)