Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Halima Abdallah Bulembo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya makadirio ya Serikali ya mwaka wa fedha mwaka 2019/2020

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ya nne ya Serikali ya Awamu ya Tano, imeonesha msimamo madhubuti wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Rais John Pombe Magufuli kwa kuendeleza miundombinu ya msingi ili kuwezesha uchumi imara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana wakati nachangia Bajeti Kuu ya Serikali nilizungumzia umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya vijana kujiajiri. Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Serikali wa kuamua kufuta kodi kwa muda wa miezi sita; suala hili litapelekea vijana kupata chachu kubwa ya kuweza kujiajiri. Natoa wito kwa vijana wote nchini kuchukua fursa hii; Serikali ina mifuko mbalimbali inayosaidia vijana kutoa mitaji. Mpaka sasa Serikali kupitia vikundi vinavyoendeleza vijana vikundi 775 vimeshapewa mitaji jumla ya bilioni 4.2, kwa hiyo naipongeza sana Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa; nimesema mara kadhaa hapa Bungeni kwamba Mkoa wa Kagera ndio mkoa pekee unaopakana na nchi nyingi Afrika Mashariki. Mkoa wa Kagera unapakana nan chi za Uganda, Rwanda pamoja na Burundi. Vilevile kupitia Ziwa Victoria Mkoa wa Kagera unaifikia Kenya. Nilikuwa naiomba Serikali yangu sikivu ije na mkakati wa makusudi wa kuufanya Mkoa wa Kagera kuwa kituo kikubwa cha biashara. Najua sasa hivi Serikali inatekeleza miradi mikubwa kama barabara, reli na umeme, lakini pia hili la biashara ni kubwa kwa sababu itapelekea nchi yetu kunufaika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi anazozifanya kutokana na kupinga suala zima la rushwa. Hapo zamani tulipata kusikia kwamba kuna kipindi bajeti ya Serikali asilimia 30 ilipotea kupitia manunuzi. Kwa sasahivi hadithi hii haipo fedha zikipangwa kwenda kwenye shughuli za umma zinafika kwenye shughuli za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumalizia kwa hadithi moja, hii hadithi inasikika sana TBC, nadhani wengi wetu tunaijua. Kwamba kulikuwa kuna binti mfalme yupo kilimani kunahitajika mchumba kwenda kumuoa, na sharti lilikuwa, utakapokuwa unakwenda chochote utakachokisikia usigeuke nyuma, pembeni wala nyuma. Kwa hiyo watu wakawa wanapita wakifika katikati wanasikia woowoowoo akigeuka kushoto, kulia anageuka jiwe, kushoto kulia anageuka jiwe. Sasa kuna kijana mmoja ambaye alikuwa jasiri yeye hakugeuka nyuma alitembea moja kwa moja mpaka kule kilimani akamfikia huyo binti mfalme.

Waheshimiwa Wabunge nataka niwaambie kiongozi bora ni yule anayesimamia anachokiamini. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli huu ni mwaka wa nne sasa amesimamia kwenye miradi mikubwa anayoitengeneza. Hajatikiswa na kelele za ndani wala za nje, yeye amesimama imara anaelekea kule kukamilisha miradi yake mikubwa, anaenda kumfata binti mfalme, binti mfalme huyo ndiye Tanzania ya viwanda; kwamba atakapokamilisha miradi hii Tanzania ya viwanda itakuwepo. Kwa hiyo naomba sana kumpongeza Mheshimiwa Rais na aendelee na msimamo wake huo na nina wapongeza Mawaziri wote wanaomuwezesha yeye kufikisha lengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.