Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya kuongea leo kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninachoifurahia Serikali ya CCM kwa kutoa tozo za ng’ombe au wafugaji. Hata hivyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, katika sekta ambazo umeisahahu ni Sekta ya Uvuvi. Sisi wavuvi; mimi mvuvi, ndiyo; sisi wavuvi kuna tozo moja tunatozwa dola 1.5 royalty levy, ni shilingi 3,300 kwa kilo ya dagaa. Na alivyokuja Waziri Kilwa na wavuvi wa Kilwa tuliomba sana hii tozo ipungue, kwa sababu unapoteza dola 1.5 sawasawa na kila kilo moja ya dagaa shilingi 3,500 mvuvi atakuwa hapati bei nzuri na wala hatuwezi kuuza nje ya nchi hawa dagaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na sababu kubwa kule Ziwa Victoria dagaa hao hao wanatozwa 0.16, shilingi 300 kwa kilo. Kwa hiyo dagaa wa Pwani shilingi 3,600 kwa kilo, dagaa wa Victoria shilingi 300 kwa kilo. Ina maana kwamba dagaa wa Pwani hawatakuwa tena na soko kwa sabbau hawatakwenda nje. Tunaomba sana kwamba hii tozo ibadilishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili, wavuvi wa Kilwa wamechomewa nyavu zao. Walikata leseni, wana vyombo vyao halali, nyavu zao ni milimita nane, za halali za kisheria, na mtu ukikata leseni ina maana kwamba mtego wako umekaguliwa na ni halali kuvulia. Sasa cha ajabu zaidi ni kwamba tuliiomba Serikali kwamba hizi nyavu zisichomwe mpaka hiyo kanuni ya milimita nane ipitishwe; Waziri akakubali kwamba nyavu zisubiri. Alivyotoka pale Kivinje kufika Dar es Salaam tu siku ya pili nyavu zikachomwa. Zile nyavu milimita nane zikachomwa halafu mwezi wa tano zikaruhusiwa tena milimita nane zivue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naona ajabu, halafu mnasema Serikali hii ya wanyonge. Kwamba milimita nane tuliomba zivumiliwe Waziri akasema zisichomwe mpaka sheria irekebishwe na alituahidi kwamba itarekebisha mwezi wa tano. Akitoka pale Kivinje anavyotuahidi akifika Dar es Salaam tu kachoma. Alivyochoma mwezi wa tano anaziruhusu zilezile nyavu alizochoma zivue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana kwa kuwa wavuvi walikuwa na leseni zao, vyombo vyao halali na nyavu zao zilezile zilikuwa halali, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango ongeza katika bajeti fedha za kuwalipa fidia milioni 900. Ongeza warudishiwe hela zao kwa sababu mmewaonea, naiomba Serikali wavuvi warudishiwe hela zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitabu chako ukurasa wa 79 anasema kiongozi achaguliwe anayetoka katika ndani ya chama cha siasa kinachotetea maslahi ya haki ya wanyonge na chama hicho ni CCM. Sifa za wagombea, chakushangaza mna sifa gani ninyi CCM kwamba wanyonge ndiyo mnawatetea ninyi!

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mnasema kwamba wafanyakazi wasiongezewe mishahara kwa sababu kuna miradi mitatu mikubwa ya kiuchumi. Wakati mnawaambia wafanyakazi wasiongezewe mishahara sisi Wabunge posho yetu ya siku 30 ni mishahara ya miaka miwili na miezi sita ya mfanyakazi. Tuseme wafanyakazi wadogo wangojee sisi Wabunge tuna mishahara mikubwa na miposho mikubwa wao wangojee. Wanyonge hao, wanyonge mnawanyonga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge leo hata tukikaa miaka mia hatuongezewi mishahara wala hatuna taabu; tunakunywa maji safi na salama, tunasomesha watoto wetu, lakini wanyonge, wafanyakazi wasiokuwa na mishahara mizuri mnazuia kuongeza mishahara mnasema eti mngojee mpaka… hii CCM hii, naomba sana…

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa; Mheshimiwa Asha Abdullah Juma.

TAARIFA

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Selemani, maarufu Bwege, kwamba alikuwepo wapi mpaka sasa hivi anaona hana nafasi ya kupata katika uchaguzi ujao anasema kwamba mshahara ni mkubwa; alikuwa wapi tangu alipoingia humu Bungeni?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, endelea na mchango wako.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba muda wangu uzingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wala simuelewi anachokisema, naona kababaishababaisha maneno tu. Ninachosema Serikali ya CCM mnasema mchaguliwe kwa sababu mnawatetea wanyonge, wanyonge ni watu ambao wanapokea mishahara midogo…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: …posho yetu sisi Wabunge…

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Taarifa juu ya taarifa, mimi najibu taarifa hii kwanza. Kwa hiyo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara, kuna taarifa; Mheshimiwa Agness Marwa.

TAARIFA

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa taarifa kwa muongeaji anayeongea kwamba Serikali imesema kwamba wafanyakazi wasiongezewe mishahara kwamba Mbunge haruhusiwi kuongea uwongo Bungeni, atuelezee kwamba ni nani aliyetamka hayo matamko.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, aliyetamka ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na clip tunazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika Nchi za SADC tulikubaliana kwamba kilimo kisipate chini ya asilimia 10 ya bajeti. Leo mkulima mnyonge mnampangia asilimia 1.5, eti Serikali ya CCM ya wanyonge. Serikali ya CCM leo watu wanatekwa, wanapigwa risasi, wanyonge, hawafikishwi mahakamani, na wanaopigwa risasi wanakufa, eti Serikali ya wanyonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mkulima wa korosho kalima korosho zake mpaka leo hajalipwa, Serikali ya wanyonge. Leo wavuvi wanachomewa nyavu zao ilihali ... Serikali ya wanyonge; mnyonge gani? Leo wafanyabiashara wadogowadogo wanalipishwa shilingi 20,000 kila mtu, Serikali ya wanyonge; wanyonge gani? Nashangaa sana ninyi mtapitaje katika uchaguzi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wanalia, wavuvi wanalia, wakulima wanalia, wafanyakazi wanalia; Serikali ya wanyonge mtapita wapi? Tunajua mnataka kupita ninyi kwa kutumia rungu yenu ya dola, polisi, wanajeshi wasimamie uchaguzi ili mshinde, lakini kwa wanyonge wa nchi hii kuichagua CCM, ng’ooo! Mnyonge gani! Leo tunakula tunaomba sana Serikali ya CCM siyo ya wanyonge, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, mnyonge hapati haki mpaka mwenye nguvu atake, wenye nguvu ndio ninyi Serikali ya CCM, manawaonea wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kimechanwa kitabu juzi hapa kwa kuwa sijui kitabu cha wanyonge mmeacha tu; mikutano ya hadhara inazuiliwa kwa sababu sisi wanyonge, acheni bwana. Naomba sana Serikali ya CCM ijirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge posho yake ya mwezi mmoja mishahara ya miaka miwili na nusu ya mnyonge. Soko hilo hilo, shule hizo hizo, anaposoma mtoto wa mnyonge na mtoto wa Mbunge hapohapo; soko la mnyonge na soko la Mbunge hilohilo lakini mshahara 350,000. 350,000 kwa mwezi sisi posho siku moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania Nyerere alisema, mwisho nasema, kasema mtu mmoja hapa eti nchi yetu ina uhuru, Nyerere alisema nchi yoyote isiyoweza kujitegemea haiwezi kuwa huru. Ndiyo maana tulisema ujamaa na kujitegemea, kama hukujitegemea ujamaa hautekelezeki na tutakuwa chini ya mabeberu mpaka kiama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutwa ombaomba tu na mtu anayeombaomba hawi huru, kwa hiyo, sisi hatupo huru tuna uhuru wa bendera tu. Naomba sana…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: …naomba sana, naona kasimama mama pale.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara kuna taarifa. Mheshimiwa Jenista, naona kengele yake imegonga hapo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimesimama kabla kengele haijagonga.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge huyu ndio Waziri mwenye dhamana ya ajira, kwa hiyo Mheshimiwa Jenista Mhagama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu
Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Bungara. Amesema kwamba nchi yoyote ambayo inataka kujitawala ni lazima ijenge uchumi wake yenyewe, na ame-quote maneno ya Baba wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumthibitishia Mheshimiwa Bungara, na ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli imeamua kubeba concept ya Baba wa Taifa kuhakikisha inakuja na miradi mikubwa ya kimkakati ili kuhakikisha nchi yetu inajenga uchumi wa ndani na uchumi ule wa ndani ndiyo utakaomaliza kero nyingi za wananchi wanyonge wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huohuo, tukiendelea na miradi mikubwa ya kimkakati, miradi ile ya kuwanufaisha wanyonge kama ujenzi wa zahanati, ujenzi wa vituo vya afya, elimu bure kwa wanafunzi, hayo yote yameshakwenda kwa wananchi wanyonge. Mheshimiwa Bungara anajua hata wananchi wa jimbo lake wanapata elimu bure na kitu hicho hakikuwepo katika muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninataka kumpa taarifa Mheshimiwa Bungara.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake kwanza ni nzuri sana.

NAIBU SPIKA: Muda ulishaisha Mheshimiwa Bungara. Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka…

(Hapa Mheshimiwa Selemani Bungara alikuwa akipiga kelele)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bungara tafadhali!

Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka kuna wakati taarifa za kifedha zikiwekwa wazi huwa kuna watu wanalalamika hivi. lakini maneno kama haya yakizungumzwa pengine ni muhimu watu wafahamu ni fedha kiasi gani Wabunge wanapata ili irahisishe wananchi huko nje kuona uhalisia wa mambo haya. Kwa sababu mtu anaweza akasema jambo halafu akitoka hapo nje anadaiwa 50,000 miezi sita mtu hajalipa wakati analipwa hela ambayo ni posho ya siku moja mtu analipwa mshahara.

Kwa hiyo pengine ni muhimu Waheshimiwa Wabunge kama mnakubaliana na Mheshimiwa Spika, atangaze Wabunge tunapata kiasi gani inaweza ikarahisisha mchango wa Mheshimiwa Bungara ili wananchi wafahamu, inaweza kutusaidia kidogo maana naona Wabunge walikuwa wananiangalia hapa kama ni kweli ama vipi.