Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru kunipa nafasi hii ili kuweza kuchangia Wizara hii kubwa namna tunavyoendesha nchi yetu kwa sababu hapa ndiyo penyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka mwaka jana kama siyo mwaka juzi, nilichangia hapa mifumo ya Serikali tunavyoendesha hasa katika ugawaji wa rasilimali. Nililalamika sana hapa Mheshimiwa Mpango ulinisikia lakini napenda kushukuru kwamba baada ya malalamiko yale, naweza sasa leo nikajidai hapa nikasema sasa Songwe tuna hospitali na kila kitu ambacho nilikilalamikia pale ikiwemo miradi ya maji. Kwa haya yote, nikupongeze sana kwa namna ulivyonisikia na namna ulivyotekeleza mambo kwenye Mkoa wetu wa Songwe na Jimboni kwetu. Naishukuru sana Serikali ya Awamu hii ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo yote yanayoendelea kutekelezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kikao alichokifanya cha wafanyabiashara two weeks ago pale Dar es Salaam. Kwa kweli kikao kile kimetupa dira na kimeleta mwelekeo mzuri wa wafanyabiashara Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge tumekuwa tukilalamika sana humu ndani na Waheshimiwa Wabunge mtaniambia, mengi ambayo tumekuwa tukiongea sasa ndiyo yaleyale ambayo aliongea na wafanyabiashara lakini Mawaziri wetu ni kama vile mna-ignore Wabunge. Tukiongea sisi hata wale watumishi wenu wanasema aah wameongea tu wanasiasa, ni siasa tu, lakini tumeongea sana humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka hata Mheshimiwa Musukuma alivyoongea pale aliongea yaleyale ambayo kila siku anaongea humu ndani na sisi tunaongea hayohayo. Hata hivyo, kwa sababu kilikuwa ni kikao special ameitisha Mheshimiwa Rais yakachukuliwa kama vile ndiyo mambo ambayo ni makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango na sisi Wabunge tukiongea mambo hapa undeni Tume ya kufuatilia yale ambayo tunakuwa tumeyaongea, mtapata faida nyingi. Tusingefikia pale kama mngekuwa mnachukua michango ya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kwamba Mkoa wa Songwe kule Jimboni kwangu, hivi ninavyoongea kuna kampuni moja inaitwa Heritage Rukwa Tanzania Ltd wale Wazungu wameenda kwao kwa sababu hawajaelewana na TPDC. Hawajaelewana nao kwa sababu hawa watu wa kampuni ya Heritage walikuja kufanya utafiti wa kuchimba mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni hii ndiyo iliyofanya utafiti wa kupata mafuta kule Uganda ambapo sasa hivi pipeline inaendelea kutengenezwa kufika Tanzania. Ni kampuni kubwa ambapo tungeweza kunufaika nayo sana. Wamefika Jimboni kwangu Kijiji cha Maleza, wameanza kufanya utafiti wao, wamechimba na wameyakuta mafuta. Baada ya pale wamerudi Serikalini kufanya negotiations katika sheria zetu ambazo zimebadilika mwaka juzi kuhusiana na masuala ya mafuta na madini. Mpaka hivi ninavyozungumza Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wale watu wameondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ifuatilie ule mgogoro ni nini hasa? Maana yake mpaka sasa hivi wameshatumia million 3.6 USD; wameshajenga madaraja na wameshafanya kila kitu. Ukiongea nao unaweza ukatoa na machozi lakini kuna watu wapo pale Shirika la Petroli sijui wamefanya nini na wale Wazungu. Naomba Serikali hebu lichukueni hili kama ni serious issue. Mheshimiwa Rais akija Songwe nitamwambia na nitamfikisha sehemu ile. Sasa kabla Mheshimiwa Rais hajafika Songwe, naomba Serikali na nyie mkae na watu wa Heritage Tanzania wapo pale Dar es Salaam muone tatizo ni nini. Hii inatupotezea umaarufu mkubwa sana wa kujipatia fedha kwa ajili ya masuala ya mafuta. Wenzetu Uganda walikubali na wamefanya na sasa hivi mafuta yamepatikana kule Uganda.

Mheshimiwa Naibu Spika, yule RAS ambaye Mheshimiwa Rais ametupa Songwe ni very creative yule kijana anaitwa David Kafulila. David Kafulila ameshawishi Mkoa wetu kupitia RCC tumeanzisha kampuni inaitwa Songwe Business Company Ltd. Wakurugenzi wa Halmashauri ndiyo wadau na ndiyo board directors kwenye kampuni ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii tayari TAMISEMI walishaturuhusu na imeshaanza kufanya kazi. Naomba kila Halmashauri au kila mkoa kama wangeweza kupitisha kwenye RCC zao tuwe na kampuni kama hizo ambazo zinamilikiwa na RAS pale mkoani, inafanya biashara kuliko kutekeleza kule Halmashauri ambako kuna bureaucracy nyingi sana. Ni jambo zuri na mtakuja kuona faida yake. Sisi baada ya miaka mitano tunaweza tusiwe tunaomba hela Serikali Kuu, RAS wetu Kafulila anafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kitu ni kikubwa sana, siku moja Waheshimiwa Wabunge nitawaletea ile Memorandum of Understanding ya RCC ya Songwe, ni jambo kubwa sana Mheshimiwa Mama Mbene anaweza akani- support hapa. Kwa hiyo, naomba hata Halmashauri zingine ziweze kufanya hivyo, hii kampuni inamilikiwa na Halmashauri zote tano za Mkoa wa Songwe na Ma-DED ndiyo board members wa kuendesha miradi ya kibiashara kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nilichangie ni kuhusu suala la EPICA, kuna kitu kinaitwa EPICA kwenye mfumo wa fedha. Nataka niseme kabisa kwa machozi makubwa, hii EPICA, of course sisi siyo wataalam wa kujua EPICA ni nini lakini angalau mimi najua. EPICA hii inasumbua sana baada ya kupitisha bajeti hii, tarehe 30 Juni, 2019 kesho kutwa baada ya bajeti kupitishwa hapa, fedha zote za kwenye Halmashauri zinafungwa. Kuanzia tarehe 1 Julai, 2019 mpaka ije ifike tarehe 30 Julai, 2019 kule kwenye Halmashauri kunakuwa hakuna mfumo kabisa wa namna ya ku-access fedha za Serikali mpaka tarehe 1 Agosti au mpaka Septemba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mwaka jana mpaka Halmashauri wananiuliza Mbunge tuna mfanyabiashara gani mkubwa hapa tunaweza kumkopa fedha tuweze kukamilisha labda mahitaji ya Halmashauri. Naomba tutafute mfumo mwingine ambao unaweza ukasaidia ili baada ya bajeti kupita, angalau tarehe 15 au hata baada ya wiki mbili Serikali ifungue mifumo yake ya fedha. Nini maana ya kujenga mkongo wa Serikali kwa Halmashauri? Kwa hiyo, mifumo ya kompyuta ifunguke mara moja ndani ya wiki mbili Halmashauri ziweze ku-access fedha ili tuweze kutumia. Najua Waheshimiwa Wabunge wenye Majimbo mtakuwa mnahangaika sana na mifumo ya fedha kuanzia Julai na Agosti kwenye Halmashauri zetu, kwa kweli mimi kule kwangu inasumbua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi mchango wangu leo ilikuwa ni hayo, hasa mfumo wa EPICA na Heritage Company, watu wa TPDC waweze kukaa na Serikali na wale Wazungu ili mambo yaweze kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)