Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya bajeti. Naanza kwanza kwa kuunga mkono hoja hii, nachukua nafasi hii kupongeza juhudi zinazoendelea kufanywa juu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Kiongozi wetu mahiri Dkt. John Pombe Magufuli, akisaidiwa na viongozi Waandamizi wake, Mama Samia Suluhu, Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Watendaji wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Ashatu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha walioweza kufanya kazi nzuri hii leo inatuweka hapa ambayo ndiyo roho ya Taifa letu, Wizara ya Fedha ndiyo roho, wakaweza kuwasilisha bajeti shirikishi na kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Esther ananikera. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu ujikite zaidi katika hii sekta ya uchumi, ukurasa wa sita hali ya uchumi. Kukua kwa uchumi ni jambo zuri kwa Tanzania. Pato la Taifa tumeona limekua kwa asilimia 7.0 kutoka asilimia 6.8 ya mwaka 2017. Namuuliza Waziri Je, uchumi huu na ukuaji huu ni shirikishi, yaani inclusive? Ambao umezingatia umaskini kwa kina? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukuaji mkubwa umerekodiwa katika sekta ya sanaa ambayo tumeona hapa ni 13.7 ukilinganisha na sekta ya kilimo umepata kukua asilimia 5.3 ambao hautoshi. Kama tunavyotambua sekta hii ya kilimo ina watu wengi wanaoitegemea kwa ajira, kuzalisha chakula, biashara, mazao, kwa ajili ya viwanda. Kwa maoni yangu, sekta hii ya kilimo ndiyo inauhitaji mkubwa kukua zaidi, ili iweze kuongeza, uzalishaji zaidi (productivity) ili iweze kulima kisasa, (modern agriculture) na kupanua wigo kwa kuongeza malighafi. Mheshimiwa Waziri tuangalie kwa jicho la ziada namna gani ya kuongeza bajeti kwenye hii sekta ya kilimo na je, tunaona kwa hii tuliyoipangia sasa hivi inaweza kukidhi kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kwamba, sekta ya sanaa tumeona imebeba ajira kwa vijana wengi, lakini naamini sekta ya kilimo vilevile ikifanyiwa ubora zaidi, hasa kwenye mambo ya organ, research, pamoja na kuongeza malighafi itaweza kuajiri, kupanua wigo kwa vijana zaidi watavutiwa hasa tukitia hiki kitu wanaita agri-business. Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango, ninataka kufahamu kwamba, hii asilimia Saba ya ukuaji uchumi Kitaifa kwamba, je, imeoanisha na takwimu za Zanzibar za ukuaji uchumi, maana imesema Taifa? Sasa Taifa hili ni Taifa Tanzania au Taifa upande gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri uchumi ni mkubwa. Nataka niulize huu uchumi mkubwa ambao umeanza kukua kwa zaidi kwa kasi kubwa, je, unaushikaje mkono uchumi mdogo wa Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri kwamba kutayarishwe mkakati wa pamoja (strategic growth), baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuweza kuangalia mambo haya. Katika hali ya uchumi wa Taifa ya mwaka 2018, ukurasa wa 118 kitabu kimeonesha viwango vya umaskini Tanzania Bara kwamba umepungua, mapato na matumizi 2017/2018 basic needs property survey imeonesha kutoka 28.2 hadi kufikia 26. Kwa sasa, kama mnavyojua tunatekeleza malengo endelevu ya SDG 2030 na agenda ya 2063 Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, umasikini kupungua ni hali nzuri. Tunataka tuchukue hatua, ili umasikini huu uweze kupungua zaidi. Tunaweka mikakati ipi madhubuti ya kuongeza tija kwenye kilimo tuweze kutumia bahari yetu kikamilifu, tuendeleze kujenga miundombinu, tuendeleze human development, kustawisha elimu na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba taarifa hizi za ofisi zetu za takwimu ziweze kufanywa pamoja baina ya Zanzibar na Tanzania bara. Kama vile tunavyofanya kwa sensa ya watu kwa vile taarifa hizi zinatumika kwa pamoja na zikiwa zimefanywa kwa pamoja zitaleta picture yenye faida zaidi. Nafahamu pia kwamba, tunakwenda kuwasilisha report ya hiyari ya utekelezaji wa SDG UN mwezi Julai. Pande mbili najua zinashiriki katika matayarisho, nasisitiza uanishwaji wa data na taarifa muhimu za uchumi na umasikini, napendekeza bajeti survey ifanywe mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu mikopo nafuu, ukurasa wa 10 makadirio na mapato. Natambua kwamba, Serikali inatayarisha mwongozo wa ushirikiano baina ya Tanzania na washirika wa maendeleo. Katika kufuatilia kwangu nimefahamu Zanzibar imeshiriki kikamilifu katika matayarisho ya mfumo, frame work, ingawa katika utekelezaji kumekumbwa na changamoto na nina imani kubwa Serikali hii inafanyia kazi changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Zanzibar ina miradi ambayo kwa utaratibu inapitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Mpaka sasa iko miradi kadhaa ambayo imekwama ikiwemo miradi ya maji, barabara, kwa mfano Barabara ya Wete – Chake, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na Bandari ya Mpigaduri, mingine imekwama kutokana na vipengele vya misamaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii barabara na hospitali ilitarajiwa kupata mkopo wa Saudi Fund. Kadhia kubwa ni hii ya mradi wa Zanzibar Airport, mkopo kutoka Exim Bank, mradi huu umekwama muda mrefu sana na kipingamizi kikubwa kwa maendeleo na ustawi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba mazungumzo yaendelezwe kwa speed na yakamilishwe kwa manufaa ya pande zote mbili ili Zanzibar nayo iweze kufaidi na kutumia Airports zake maana upo wivu wa maendeleo kwa sababu Airport ya huku Dar-es-Salaam imekamilika na hii yetu iliyoanza mwanzo haikukamilika, tunachukua kwamba, Zanzibar ni kisiwa na uchumi wa kisiwa unategemea zaidi bandari na uwanja wa ndege. Sasa tunaomba kwamba jitihada za ziada zichukuliwe baina ya Serikali zetu hizi mbili ili hili jambo liweze kukwamuka. Sekta hizi mbili, bandari na uwanja wa ndege, ndiyo sekta kiongozi kwa uchumi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo nafuu na misaada. Misaada ya kibajeti, mifuko ya kisekta, miradi ya maendeleo, ningependa kujua katika jedwali hili kwenye ukurasa wa 103, Zanzibar imepata kiasi gani? Pendekezo kwa mbele ni bora itakuwa vizuri kui-desegregate na kuchanganua takwimu za Tanzania Zanzibar na Bara zioneshwe waziwazi, ili tuweze kujua kila mtu anapata nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)