Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dr. Immaculate Sware Semesi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa nafasi hii, nami niweze kusema machache kuhusu hoja iliyo mbele yetu. Nina masuala matano tu ya kugusia kwa ufupi yanayohusu mwenendo wa bajeti yetu na itakavyoenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza naomba Wizara husika au Serikali ichukue ni juu ya umuhimu wa kuwa na soko katika kukuza uchumi wetu. Tunazalisha malighafi mbalimbali, kwa bahati mbaya malighafi hizi kama ni kutoka kwenye Sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi au Misitu, tuna shida katika value chain yetu, haiko vizuri, usindikaji wa mazao haya hauko vizuri ambao ni competitive Kimataifa au pia katika kuvutia soko la ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna umuhimu sana wa kuangalia masoko katika Sekta mbalimbali zinazogusa Wizara au Taasisi husika na Wizara yenyewe au Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta masoko ya ndani, kuboresha soko la ndani, kuji-advertise nchi yetu kwa masoko ya nje ili tuwe na uhakika pale tunapozalisha, basi kile tunachozalisha kiweze kutuletea tija na kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mifano mbalimbali katika Sekta ya Mifugo, tuna shida katika ngozi, tumeona katika Sekta ya Mifugo, hivyo hivyo kuna shida katika uzalishaji wa maziwa. Tuna-import zaidi kuliko ku- export. Kwa hiyo, nafikiri ni wakati muafaka wa kujitathmini kwa upya na kuweka msisitizo mkubwa katika kuangalia soko linafanyaje kazi nchini ili kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili nataka niligusie ni kufungamanisha viwanda na sekta nyingine na malighafi ambazo zina-feed in kwenye hivyo viwanda na masuala mazima ya elimu. Tunataka nchi yetu iendeshwe na Sera ya Viwanda lakini viwanda hivi vina changamoto nyingi. Kwa hiyo, naomba kuishauri Serikali, Wizara husika, Viwanda na Biashara, uwekezaji, Wizara ya Fedha na Mipango hebu iangalie ina-connect vipi na Wizara nyingine husika ambazo zina feed in kwenye viwanda? Naomba sera iangaliwe kwa upya ili tuweze kuviimarisha viwanda vyetu siyo kinadharia, bali sasa tuanze kufanya hivi kivitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu nataka niligusie ni umuhimu wa mazingira na jinsi mazingira yanavyoweza yaka-shape maendeleo ya nchi kiuchumi na katika jamii yake kiafya. Nilikuwa nimepitia kitabu hiki cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika Mwaka 2018 ukurasa wa 112 kwenda 113 sura ya nane inaongelea kuhusu mazingira na hali ya mazingira nchini ilivyo. Ninaomba tu ninukuu baadhi ya aya kutoka aya ya 161 na 162, inasema kwamba, “mwaka 2018 Serikali iliendelea kusimamia mazingira kwa lengo la kupunguza athari za uharibifu wa mazingira kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kudhibiti athari za matumizi ya Zebaki (Mercury) katika uchimbaji mdogo mdogo.”

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ni mbaya sana kwa sababu asilimia kubwa ya Zebaki inatumika katika wachimbaji wadogo na asilimia kubwa ya hawa wachimbaji inayozidi asilimia 30 wameshaathirika. Hapa hatuangalii tu athari ya hawa wachimbaji wadogo wanavyotumia madini haya ya Zebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini haya yana athari kubwa sana. Huu ni mfano tu mmoja wa uhalibifu wa mazingira katika mazingira yenyewe na katika afya ya wahusika, kwa kuwa ikishaingia katika mfumo wa mazingira, madini haya siyo rahisi kutoka na yanaendelewa kurithiwa kizazi kwa kizazi kwa wanyamapori, samaki, mifumo ya maji na binadamu wenyewe; inaenda kuharibu kizazi na afya ya yule ambaye ameathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hii, mazingira ndiyo uchumi, mazingira ndiyo maendeleo, lakini kwa bahati mbaya hatuiangalii kwa jicho hilo kama Serikali ili kutuvusha hapa tulipo. Hii ipo reflected hata kwenye bajeti yenyewe ya mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa naibu Spika, tumetengeneza Mfuko wa Mazingira hapa nchini, lakini mfuko huu badi haujawezeshwa kufanya kazi ile inayotakiwa, umenyimwa fedha tangu uanze. Kwa hiyo, kuna umuhimu sana wa kuangalia mazingira na tuanze sasa ku-link mazingira na shughuli za uchumi wetu. Unapoharibu mazingira, unaharibu vyanzo vya maji, unapoharibu maliasili ina maana utaenda kugharamia zaidi katika kuboresha yale mazingira yawe katika hali ya uzalishaji. Kwa hiyo, naomba tuiangalie kwa mantiki hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo hapo kwa mazingira kwa umuhimu wake aya ya 162 inasema, “mwaka 2018 Serikali iliendelea kudhibiti uharibifu wa ardhi ikiwa ni pamoja na kukamilisha tathmini ya hali ya uharibidu wa ardhi nchini, Tathmini hiyo inaonesha kuwa takribani asilimia 75% ya ardhi yetu hapa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa rutuba na uharibifu wa ardhi.”

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mantiki hiyo, uzalishaji wowote wa kiuchumi katika ardhi unaenda kuharibiwa unakuwa wa chini. Utalima lakini utatumia nguvu nyingi kupata mavuno yanayotakiwa kwa sababu tayari ile ardhi haina rutuba na haina hali ya kukuwezesha wewe kuzalisha kile unachokitaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuangalie kwa jicho la ziada kuwezesha mazingira nchini kutunzwa, kwa hiyo, iwe reflected katika bajeti kuwekea hela katika kudhibiti ili mazingira haya yaweze kutulea sisi. Kwa hali iliyopo sasa hivi ni tete sana na tutatumia gharama kubwa katika kuirejesha ardhi hii au mazingira yetu ili yaweze kutuzalishia bidhaa mbalimbali na kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne ambalo nataka niligusie kwa ufupi ni umuhimu wa utafiti na data. Any informed decision lazima iwe na backup na tafiti na data fulani. Kwa hiyo, naona jambo hili bado halijapewa kipaumbele katika Serikali yetu ili kuweza kuboresha bajeti yetu iweze kujiendesha yenyewe. Tunaweza tukafanya decision fulani fulani lakini haina backup ya data nzuri, yaani lazima kuwe na takwimu nzuri ili iweze kukuelekeza kwamba mikakati yako uipangaje au priorities zako ziendaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwenendo huo basi, ninaiomba National Bureau of Statistics iwezeshwe kwa rasilimali watu na kiuchumi iweze ku- coordinate kama ndiyo Bureau yetu ya Statistics na taasisi mbalimbali kama COSTECH ziwezeshwe ku-collect data na kuzihifadhi ili tuweze ku-make sound decisions.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho naomba niligusie, tuweze kujiuliza wote kwamba hii bajeti iliyoletwa mbele yetu is it gender sensitive? Je ime-accommodate matabaka mbalimbali katika kukuza uchumi wetu? Naomba nisemee hilo kwa kutoa tu mfano kwa suala zima la taulo za kike wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 38 na 39 unaozungumzia kuhusu Sheria ya Kodi ya Mapato, inasema kwamba inaenda kupunguza kiwango cha kodi ya mapato kwenye makampuni ambayo yanaenda kuzalisha taulo za kike.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali la kujiuliza je, hii movie ya Serikali inaweza kwenda kuwasaidia watoto wa kike kuwa na uwezo wa kupata hizi taulo za kike ambayo ni muhimu sana katika afya yao na katika kujenga uchumi wa nchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najua maongezi hayo, majadiliano tunafanya pamoja na Kamati ya Bajeti, lakini ningependa tu kuweka msisitizo ijitafakari kwa upya ni nini Serikali ifanye ili taulo hizi za kike ambayo ni muhimu sana kwa afya, ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi kwa tabaka hili wa jinsia ya ‘Ke’ waweze kuangaliwa; kwa wale ambao hawako mashuleni wanaipataje kwa bei ambayo ni rafiki na ni rahisi kupata? Wale walio mashuleni, watoto wa kike wanawezaje kupata hizi taulo za kike?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kusema hayo, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)