Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa waliyoifanya. Bajeti hii ambayo umetuletea kwenye Bunge hili kwa kweli ni bajeti nzuri, ni bajeti ambayo imeweza kuangalia zile changamoto za wananchi na kuweza kuzifanyia kazi kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, ndiyo maana nitumie fursa hii kupongeza sana Wizara kwa kazi kubwa ambayo imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia vile vipaumbele vya Serikali nilikuwa nikiangalia vipaumbele hivi katika ukurasa wa 31 na 32. Vipaumbele ambapo vumezungumziwa, kusema ukweli ni vipaumbele ambavyo ni muhimu kabisa, ambavyo vikitekelezwa nina imani kubwa kwamba nchi yetu ya Tanzania itaweza kupiga hatua kubwa katika suala la uchumi. Mimi binafsi nilikuwa nikiangalia katika kipaumbele namba tatu ambacho kimekusudia kuboresha mazingira wezeshi kwa ajili ya kuwezesha uchumi wetu kuweza kukua zaidi katika kuimarisha biashara na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba maendeleo katika sekta hii ni muhimu sana kuweza kuboresha miundombinu muhimu. Pia Serikali imekusudia kupeleka fedha hizi katika kuendeleza maeneo mbalimbali ya kiuchumi, kwa mfano, reli na barabara. Kwa kweli ni maeneo muhimu sana katika uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nilikuwa naangalia sekta muhimu ya nishati. Nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kuchukua uamuzi wa dhati kuwekeza fedha nyingi katika sekta hii ya nishati. Mwaka huu imeweza kutenga bajeti ya shilingi trilioni 2.1 ambayo imeongezeka kutoka bajeti iliyopita ya shilingi trioni 1.6.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najua kabisa kwamba tukiwekeza kwenye nishati, mwisho wa siku tutaweza kufikia azma ya Tanzania ya viwanda. Hatuwezi kuwa na viwanda bila ya kuwa na umeme wa uhakika. Vilevile katika sekta hii ya nishati nilikuwa najaribu kuangalia,

Serikali imekusudia kuangalia vijiji vya Tanzania 1,990 kwa ajili ya kupelekewa umeme na bajeti imeongezeka kidogo kwa asilimia 26 kutoka kwenye bajeti ya mwaka 2018 ambayo ilikuwa ni shilingi bilioni 412, mwaka huu tumeweza kupangiwa bajeti kwenye nishati kwa upande wa REA, shilingi bilioni 423. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kwamba bajeti hii bado iko chini sana. Kwa sababu gani? Wote ni mashahidi, umeme ni muhimu sana katika kuchochea maendeleo. Vijiji vingi vya Tanzania vinahitaji kupatiwa umeme wa REA. Ninasema hivyo kutokana na nini? Nimeona uzoefu, vijiji vingi vilivyopatiwa umeme kwenye Jimbo langu mwaka 2014, ni tofauti sana, yaani kiuchumi. Vimepanuka zaidi kiuchumi. Ni tofauti na vijiji ambavyo havina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hiyo sasa, pamoja na kwamba Serikali imekusudia kupeleka umeme kwenye vijiji 1,990, lakini bado ninaona vijiji hivi ni vichache sana, kwamba mpaka mwaka 2,020 mwezi Juni, vitakuwa vimefikiwa vijiji vya Tanzania nzima vijiji zaidi ya 10,000. Hata hivyo vijiji 10,000, ndani ya vijiji 12,000, tunaona bado kabisa Serikali inahitajika kuongeza fedha zaidi kwenye REA ili vijiji vingi vya Tanzania viweze kubahatika kupatiwa umeme. Vikipata umeme vijiji hivi, nina uhakika kwamba vitaweza kupanuka zaidi kiuchumi, kwa sababu watakuwa na uwezo wa kuanzisha hata viwanda vidogo, vikubwa na vya kati. (Makafi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshuhudia wananchi wakianzisha viwanda vidogo na vya kati kwenye maeneo ambayo yana umeme. Kwa mfano, kwenye Sekta ya Madini ambako mimi natokea, ambako wananchi wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini. Kwa hiyo, vijiji ambavyo vimepatiwa umeme vimekuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vidogo vya uchenjuaji dhahabu; vidogo, vya kati na vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara ya Fedha, hebu iangalie kuongeza umeme kwenye REA ili vijiji vingi vya Tanzania viweze kupatiwa umeme huu ambao utawawezesha zaidi kuinua kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimejaribu kuangalia bajeti hii pia kwa upande wa barabara hasa kwenye upande wa TARURA, wote tunafahamu kwamba kuna mtandao mkubwa sana wa barabara, hasa za vijijini na mijini zenye takribani urefu wa kilomita zaidi ya 100,000, lakini kwenye bajeti tumetengewa kwa ajili ya utengenezaji wa kilomita zaidi ya 21,000. Naona kwamba kwenye kilomita 100,000 tunatengeneza 21,000 tu, bado hizo kilomita ziko chini sana na wote tunafahamu kwamba barabara ndiyo injini ya uchumi. Kama hakuna barabara, maana yake ni kwamba kunakuwa hakuna maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa hasa ni vijijini ambako ndiko kuna changamoto kubwa. Barabara nyingi za TARURA ambazo zina changamoto kubwa hazipitiki. Kwa hiyo, naomba, pamoja na kwamba nimeangalia bajeti iliyotengwa, tena mwaka huu wamepunguza kuliko ile ya mwaka 2018. Nimeona wamepunguza, ya mwaka 2018 ilikuwa shilingi bilioni 243, lakini mwaka huu bajeti ya ni shilingi bilioni 224. Ninaona kwa kweli bajeti ni kidogo sana kwa upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii sasa kuishauri Serikali inapofanya marekebisho kwenye bajeti sasa, iangalie hata kuwezesha, kuongeza kidogo bajeti kwenye TARURA. Hii itawezesha barabara za vijijini ziweze kupitika vizuri, ambako ndiko Watanzania wengi waliko. Wote tunafahamu zaidi ya asilimia 70 au tuseme kuanzia asilimia 60, 65, Watanzania wanaishi vijijini na ndiko ambako sasa shughuli nyingi za kiuchumi zinafanyika, ukisema ufugaji unafanyika kijijini mara nyingi; ukisema kilimo, kinafanyika vijijini, ukiangalia hata shughuli za uchimbaji wa madini ni vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali hebu iangalie TARURA, iongeze bajeti ili hatimaye wananchi walio wengi waweze kufanya kazi zao vizuri, wasafirishe mazao yao kutoka hatua moja kwenda sehemu nyingine, ili hatimaye sasa uchumi wetu wa Taifa uendelee kukua zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nilikuwa naangalia pia katika kipaumbele namba mbili cha Serikali, ambapo kimekusudia kwa maelezo kwamba ni ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Naipongeza sana Serikali kwa sababu imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba uchumi unakua lakini pia na maendeleo ya watu yanakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekusudia kufanya mambo makubwa sana. Kwa mfano, kwenye Sekta ya Afya, Serikali imekusudia kujenga hospitali nyingine 27, ambapo za mwaka 2018 zilikuwa Hospitali za Wilaya 67. Kwa hiyo, zimeongezeka zaidi. Napongeza kwa kweli kwa kazi kubwa ambayo Serikali imekusudia kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hivyo, Serikali inakusudia kujenga vituo vingine vya afya kama 52, jambo ambalo mimi binafsi nalipongeza kuona kwamba Serikali imekusudia kuleta mabadiliko ya kipekee katika Taifa letu la Tanzania hasa katika Sekta ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu. Kwanza nimeletee salaam kutoka kwa wananchi wa Busanda, hasa kwa kutupatia Hospitali Katoro pale ambapo kumekuwa na changamoto ya siku nyingi, alipokuja kwenye maazimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Yeye mwenyewe amesema hospitali itajengwa na tayari anashughulikia suala la fedha ili ziweze kwenda kwa ajili ya kuanza kufanya shughuli za ujenzi wa hiyo Hospitali ya Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi binafsi kwa niaba ya wananchi na wananchi wenyewe wamenituma nikupongeze kwa kweli kwa kazi hiyo na kwamba tuko tayari kuunga mkono Serikali kwa ajili ya shughuli zinazoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)