Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hii hoja iliyopo mbele yetu lakini pia sambamba na hilo naomba nichukue fursa kuungana na wenzangu wote kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, Naibu Waziri Dkt. Ashatu, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii. Ndugu zangu pamoja na maneno yote naomba muendelee kuchapa kazi kwa sababu kazi mnayoifanya inaonekana. Naomba niwatie shime kwa hilo kwa hiyo msikate tamaa maisha ni mapambano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia ukurasa wa 31 hadi ukurasa wa 33 wa hotuba hii mmezungumzia kuhusu vipaumbele ambavyo vimewekwa. Naomba nipongeze sana Serikali na Wizara kwa ujumla kwa kuweka vipaumbele hivi na hasa kwenye suala zima la vipaumbele vya kilimo na viwanda. Juhudi zinaonekana pamoja na ufinyu wa bajeti lakini Serikali inajitahidi sana. Niipongeze tena Serikali kwa kuwa na hii program ya kuendeleza kilimo ya ASDP II. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo nina ushauri, kwamba Serikali imejipanga kujaribu kuona jinsi gani pembejeo zinaweza zikapatikana na kadhalika, lakini bado naomba nisisitize suala la wataalam. Kwa kweli suala la wataalam bado wataalam hawatoshelezi, huku katika maeneo ya kata na vijiji ambako ndiyo wako wakulima zaidi kwa kweli wataalam hawako wa kutosha. Kwa hiyo utakuta kwamba wanalima mazao bila kufuata zile taratibu za kitaalam, kwa hiyo, nilikuwa niiombe Serikali yangu tukufu waone umuhimu sasa wa kuona jinsi gani wataalam zaidi wanaweza kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wataalam hawa inabidi waandaliwe kuanzia katika shule za msingi ili watoto waone kwamba kilimo ni sehemu ya ajira na wasione kwamba kilimo ni adhabu. Kwa hiyo, kama wakitengenezwa kuanzia katika ngazi ya chini, naamini kabisa tutaweza kupata watalaam wengi zaidi. Ni ukweli usiopingika kwamba, kwa kuwa Tanzania yetu inakwenda kwenye uchumi wa viwanda suala la malighafi lazima lipatikane, na hizi malighafi lazima zipatikane humuhumu nchini ili kusudi wananchi wetu na wakulima wetu waweze kupata tija. Kwa hiyo, bado niendelee kushauri kwamba upo umuhimu kabisa wa kuhakikisha kwamba bajeti ya kutosha inapangwa hasa kuhakikisha kwamba wataalam wanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuhimiza mapinduzi ya viwanda lakini bado tunategemea kilimo cha mvua, na wenzangu wengi wamelizungumza hili kwamba hakika itabidi lazima tufanye mkakati wa uhakika wa kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa ni kilimo cha umwagiliaji badala ya kilimo cha mvua. Tumeona hivi karibuni jinsi gani mvua ambavyo zimechelewa na jinsi gani mazao yalivyoathirika, kwa hiyo, nitoe shime kwamba tuone kwamba suala la kilimo cha umwagiliaji kipewe kipaumbele ili kusudi sasa tuweze kupata zile malighafi kwa ajili ya kulisha hivyo viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala la uendelezaji wa suala la zao la zabibu. Niendelee kuipongeza Serikali suala zima la kupunguza ile bei ya mchuzi wa zabibu lakini bado ilikuwa ili kuliongezea hili zao la zabibu thamani isiwe ni mvinyo tu, lakini zipatikana bidhaa nyingine zinazotokana na zabibu mfano juice, pengine jam na mazao mengine ambayo yatatokana kutokana na hii zabibu. Kwa hiyo, tuhamasishe uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo na hasa kwa wanawake ili kusudi waweze kutengeneza hizi bidhaa mbalimbali ambazo zinatokana na zabibu na ikiwezekana wapewe fursa ya kutengeneza mchuzi wa zabibu hatimaye waweze kuuza katika hivi viwanda vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, zabibu hizi zinaweza zikakaushwa. Zikikaushwa zabibu naamini kabisa zitaleta sana tija kwa nchi yetu hasa Mkoa wa Dodoma kwa wakazi na wakulima wa Mkoa wa Dodoma. Kwa sababu zabibu kavu nazo zina soko zuri sana na zabibu hizi zinaweza zikailetea pato Taifa letu. Kwa sababu inaonekana kabisa kwamba zabibu hizi nyingi hazitengenezwi hapa instead zinaagizwa kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, zabibu za kukausha basi Serikali ione tunawezaje kupata mitambo ya kutosha ili kusudi sasa wananchi wetu waweze kukausha hizi zabibu na hatimaye Serikali yetu iweze kupata pato la kutosha. Sambamba na hilo, suala zima la zabibu za mezani. Zabibu ambazo zilizopo kwa mfano katika Mkoa wa Dodoma bado zabibu za mezani hazijaweza kupatiwa pembejeo za kutosha. Kwa hiyo, basi nione kwamba Serikali nayo ione kwamba kwenye hili suala la zabibu za mezani nazo ziweze kupatikana ili kusudi tuepuke kuagiza kutoka nje tuweze kuongeza pato letu la ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kuhusiana na Benki ya Kilimo, naipongeza sana Serikali kwa kuanzisha benki hii. Hata hivyo, bado nitoe shime kwamba benki hii iongezewe mtaji na Serikali ili kusudi wananchi wengi zaidi waweze kufaidika na hii Benki ya Kilimo mwisho wa siku wananchi waweze kupata tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikuwa nataka nizungumzie Serikali ione utaratibu wa kuweza kuweka reserve ya maji ili maji haya yaweze kutumika kipindi cha kiangazi hasa katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie kuhusu vifungashio au mifuko ambayo inatumika kwa ajili ya kuweka mazao. Kuna ile mifuko ya kawaida lakini kuna ile mifuko ambayo mazao yakiwekwa mazao yale yanaweza yakakaa kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba niitie shime Serikali kwa sababu wakulima wengi sana kwanza hawana taarifa kuhusu hii mifuko ambayo ni bora zaidi lakini sambamba na hilo mifuko hii ni bei ghali sana kwamba mfuko mmoja unafika mpaka shilingi 5,000. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali ione umuhimu sasa au wa kupunguza VAT, au wa kuona jinsi gani mifuko hii inapunguziwa bei ili mwisho wa siku wakulima wote waweze kupata tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie kuhusuana na suala la taulo za kike, taulo za kike kwa sababu wenzangu wengi sana wamelizungumzia na hii iko katika ukurasa wa 38. Pamoja na Serikali kutoa ule msamaha wa kodi ile ya VAT, nilikuwa naomba niishauri Serikali hebu kuona ni jinsi gani kama ikiwezekana tuweze kuweka bei elekezi, bei ambayo itakuwa ni affordable. Kwamba kila mtu au kila mtoto wa kike anaweza akai-afford hiyo taulo ya kike, lakini sambamba na hilo kwa kuwa kuna vifaa ambavyo vinatumika kwa ajili ya kutengeneza hizi pad, basi ufanyike utaratibu wa kutengeneza reusable pads. Nakumbuka wakati ule sisi tunasoma tulikuwa tunafundishwa jinsi ya kutengeneza reusable pads ili kusudi watoto hawa waweze kuzitumia. Kwa hili suala la reusable pads pia linawezekana ili kusudi watoto waweze kuwa na taulo kwa wakati wote bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba naomba nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kutoa ile miezi sita ya uanzishaji biashara, kwamba ile grace period. Kwa kweli hii Serikali imefanya jambo zuri sana kwani hii itasaidia sana wafanyabiashara na itasaidia baadhi ya wafanyabiashara kuanzisha biashara zao na hivyo kufanya suala la kukwepa kodi likapungua. Kwa hiyo, lakini naomba nitoe rai kwa wakadiriaji hili Mheshimiwa Mpango pamoja na kuandika kwenye hotuba yako basi hawa wakadiriaji pia wawe fair sana wasiwe wanafanya kwa ajili ya kukomoa wafanyabiashara. Kwa sababu mfanyabiashara pamoja na Serikali ni marafiki na huo urafiki inabidi lazima uendelee kwa sababu tunategemeana wote, mfanyabiashara pamoja na Serikali. Serikali inategemea kodi ya mfanyabiashara na mfanyabiashara nae anategemea Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nipongeze pia suala la dawati la malalamiko la ukadiriaji wa kodi. Niipongeze sana Serikali kwa jambo hili kwa sababu hii itasaidia sasa wafanyabiashara wengi kwenda kutoa malalamiko yako na hatimaye kuweza kupatiwa ufumbuzi. Nishukuru sana kwa kunipa fursa, naomba niendelee kuiunga mkono hoja. Ahsante sana, ahsante. (Makofi)